2017-12-10 11:59:00

Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio! Toba na wongofu wa ndani!


Tuanze tafakari yetu tukisikiliza mfano wa mtoto ambaye mgeni anaenda nyumbani kwake na kumwuliza kama baba yupo. Anasema ndiyo. Mgeni anasema naweza kuongea naye. Na mtoto anajibu kwa sauti ndogo kabisa hapana. Mgeni anaendelea mama yupo? Jibu ni ndiyo lakini pia mtoto anaendelea kumjibu mgeni kuwa hawezi kuonana naye. Mgeni anaendelea; je yupo mtu mwingine ye yote ninayeweza kuongea naye? Mtoto anajibu ndiyo – yupo polisi. Na mgeni anataka kuongea naye na mtoto anajibu hapana kwa vile anaongea na mzima moto. Na mgeni anauliza ulizuka moto? Mtoto anajibu hapana ila wananitafuta.

Hakika katika mazingira kama haya yaonekana wazi kuwa mtoto huyu amejificha na anatafutwa na wazazi wake. Asipotoka nje na kuonekana hakika hatapatikana. Ndicho kinachoonekana leo katika masomo yetu na tafakari yetu ya leo. Mungu yupo amejionesha, anatutafuta na anataka tukutane naye. Ila pengine mazingira yetu hayatoi nafasi ili kukutana naye. Nabii Isaya katika somo la kwanza anatoa tangazo la ukombozi kwa Waisraeli na wito wa kumrudia Mungu. Je sisi bado tumejificha? Bado tuko utumwani? Bado tuko gizani?

Katika Biblia – jangwa yaonesha sehemu iliyo wazi, panapoonekana. Kwa maana hii haja ya kuwa wazi ni muhimu, ni lazima wahusika watoke nje ili waonekane. Leo Yohane mbatizaji anashuhudia wazi kuwa aliiishi alichofundisha – anaenda jangwani. Kwa njia ya maisha yake na ushuhuda wake anaweka mambo hadharani. Sote tunaitwa tutoke ndani yetu tuende nje – tuende kukutana na Mungu. Mwaliko wa kujuta na kuungama dhambi zetu huku tukimgojea huyo ajaye tukiwa tuko tayari. Ni kipindi cha kutambua mahitaji yetu na ya Mungu. Mtume Paulo katika somo la pili anasema kuwa anayekesha mara nyingi aweza kuona siku zinakawia. Anasema wazi kuwa Bwana anatupa sisi nafasi ya kukiri dhambi zetu na kumgeukia. Mt. Augustino anasema Mungu ametuumba sisi kwa ajili yake. Mioyo yetu haitatulia ila kwa bwana. Hivyo wito wa kutoka ndani na kwenda nje uko wazi hapa. Yohani mbatizaji amefanya hilo na akavuta watu.

Katika somo la Injili twaona kuwa ujio wa Yesu Kristo unatayarishwa au kuonekana na nabii muungamaji. Kwa ujio wake mioyo ya watu inapata nafasi ya kuandaliwa kwa ujio wa Bwana. Yohani anaita watu watoke, waonekane katika uwazi ili Mungu awapate. Kinachotakiwa ni metanoia – kubadilika kutoka ndani. Yohana atuita – na anafanya jambo – yeye anaenda jangwani – anafanya anachosema na watu wanamfuata – wanapata wanachohitaji. Wito wetu leo – tuwe mwanzo wa Injili = Habari Njema – tuangalie mahitaji yetu ya leo – tunahitaji msamaha katika nini? Tunahitaji kutangaza habari gani ili ilingane na mahitaji ya ulimwengu wetu wa leo? Ili hiyo habari njema iseme zaidi miongoni mwa watu? Yesu ndiye kamisaa, Yohana mbatizaji refarii na sisi washika vibendera – tuko pamoja au tumeangalia vitu vingine tu? Ubinafsi wetu tu?

Mwinjili Marko – anaanza Injili akitangaza uwepo wa Mungu kati yetu – sisi tunaalikwa kuwa wajumbe wa uwepo wa Mungu hapa duniani. Kipindi cha majilio kimewekwa ili tuweze kumwona tena Yesu kati yetu. Majilio ni mwanzo wa mwaka mpya wa Liturujia ya Kanisa. Tunapoanza mwaka mpya, tunatafakari ujio na kuzaliwa wa Kristo pale Betlehemu na zaidi sana tunaangalia yajayo – yaani Kristo atakapokuja tena. Katikati ya mihimili hii miwili – tunakuta maana ya maisha yetu kama wakristo. Kipindi cha majilio kinatupa mwanga au kioo cha kutazama tulikotoka na haja ya kutazamia kwa matumaini kule tuendako - maisha na matumaini yajayo tuliyopewa na Kristo. Majilio huunganisha kumbukumbu zetu – tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu akakaa nasi na tunahuisha matumaini yetu – kwamba Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu.

Kumbukumbu: tunakumbuka nini? Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu – tunatafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu –akaupa umaana uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu – akatuonesha maana ya maisha – Eti Mungu akawa mwanadamu. Tumshukuru Mungu. Matumaini: tunatumaini nini? Tunatumaini ujio mtakatifu aliotuahidia, jumuiya kamilifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu. See Pope Benedict XVI ( Joseph Card. Ratzinger) ‘Seek that what is Above’ 1986 …Memory Awakens Hope. Hatuna budi kuwa kama mpiga violini maarufu kwa jina Paganini ambaye anakiri kugundua, tena baada ya kupiga muziki kwa muda mrefu kuwa mpiga muziki ni yeye na si kile chombo anachotumia. Muziki unatoka ndani yake na si katika chombo. Chombo chatumika kama kifaa tuu. Hivyo nasi pia hatuna budi kutambua haja ya kuwa wachezaji wa mchezo, watangazaji wa hiyo habari njema na si kinyume chake. Yohani mbatizaji atutafakarishe sana kuhusu nafasi na wajibu wetu katika kuutangaza ujio na uwepo wa ufalme wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.