2017-12-05 15:59:00

Papa:Tukubali unyenyekevu na kudhalilishwa ili kufanana na Yesu!


Unyenyekevu ni kipawa muhimu cha maisha ya mkristo. Ni maneno ya msisitizo wa Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, siku ya Jumanne 5 Desemba 2017 katika Kikanisa cha Mtakatifu Marta mjini Vatican. Mahubiri yake yameangazwa na somo la kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Isaya, Baba Mtakatifu anakumbusha kuwa, kila mkristo ni kama kichupikizi kidogo mahali ambapo atatua Roho wa Bwana, Roho wa hekima na maarifa, roho wa shauri na nguvu, roho wa ujuzi na ya kumcha Bwana. 

Anasisitiza kuwa, hizi ni zawadi za Roho Mtakatifu, kutoka katika udogo wa chipukizi, kufikia utimilifu wa Roho. Hiyo ndiyo ahadi, huo ndiyo Ufalme wa Mungu na ndiyo maisha ya mkristo. Kuwa na dhamiri ya utambuzi kwamba, kila mmoja wetu ni chipukizi cha mzizi ambayo ni lazima ikue kwa  nguvu ya Roho Mtakatifu, hadi kufikia utimilifu wa Roho Mtakatifu ndani mwetu. Je ni zoezi gani la mkristo anapaswa kufanya? Kwa urahisi ni kulinda chipukizi ili kikiue ndani mwetu na kukitunza vema,katika makuzi ya kulinda Roho hiyo.

Je ni mtindo upi wa maisha ya kikristo? Ni mtindo wa unyenyekevu alioufanya Yesu: Inahitajika neema na unyenyekevu ili kuamini kuwamba kichipukizi ni zawadi ambayo ni ndogo itafikia utimilifu  wake wa kuwa zawadi kamili za Roho Mtakatifu. Inahitaji  unyenyekevu kuamini kwamba Baba, Bwana wa mbingu na Dunia, kama Injili isemavyo leo hii, amewaficha wenye hekima na elimu na kuwaonesha walio wadogo. Na unyenyekevu ni kuwa mdogo kama kichipukizi kidogo kinachokua kila siku, ni kichipukizi kidogo kinachohitaji Roho Mtakatifu ili kuweza kwenda mbele, kuelekea katika ujazo wa maisha yake.

Akiendelea kufafanua zaidi juu ya unyenyekevu anasema, mwingine anaweza kufikiria kuwa ni  mnyenyekevu ni kuwa na elimu, ukarimu au kufunga macho wakati wa kusali, lakini kumbe huo siyo unyenyekevu: Kuna ishara mojawapo ya kuonesha unyenyekevu huo, Baba Mtakatifu anaitaja ishara hiyo kuwa, ni kukubali udhalilifu. Unyenyekevu bila kudhalilishwa, siyo unyenyekevu. Mnyenyekevu awe mme na mke ni mwenye uwezo wa kuvumilia madhalilisho kama aliyovumilia Yesu, aliyedhalilishwa kwa madhalilisho makubwa! Amesisitiza Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu ameonesha hata mfano wa watakatifu wengi, kwamba si tu kukubali kudhalilishwa bali walionesha hata kufanana na Yesu. Na hivyo Bwana aweze kutupatia neema ya kutunza chipukizi kidogo kuelekea katika utimilifu wa Roho, na tusisahau mizizi na kukubali kudhalilishwa.

Sr Angela Rwezaula.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.