2017-12-02 17:09:00

Papa:Vijana wajifunze hekima kutoka kwa Mungu na urithi wa babu na wazazi wao!


Kama ilivyokuwa nchini Myanmar hata ziara nchini Bangladesh imemalizika na mkutano  kati ya vijana na Baba Mtakatifu. Mbele ya Baba Mtakatifu Vijana wamecheza ngoma za utamaduni wao na rangi mbalimbali, kwa nyimbo nzuri na furaha kwa vijana karibia elfu saba waliokuwa katika uwanja wa Jengo la  Chuo cha Mama Yetu huko Dhaka. Mkusanyiko huo wa wanachuo si wakatoliki tu bali hata wengine kutoka madhehubu ya waislam na dini nyingine nyingi zilizomo katika nchi ya Bangladesh.

Baba Matakatifu akianza hotuba yake amesema, anahisi kuwa kijana kila mara anapokuna na vijana. Ameyasema hayo kutokana na hali ya uchangamfu wao, kama walivyo kuwa  wamejaa katika uwanja huo wakicheza na ili wawe tayari kujiweka katika mchezo wa maisha. Na kwa njia hiyo hotuba yake imejikita zaidi juu ya safari ya maisha katika utambuzi wa hekima ya Mungu.

Baba Mtakatifu amewatia moyo na kusema, ni lazima kwenda mbele hasa wanapohisi kuelemewa na matatizo na huzuni kwa kufikiri kuwa upeo wa Mungu hauonekani! Akifafanua zaidi: katika kuzunguka bila mtazamo, ni bora kuchagua njia ya haki hasa ya msingi wa hekima inayotokana na imani. Hiyo ni kama vile Mungu ameweka ndani ya roho zetu programu moja (software) inayosaidia kuchagua programu za Mungu, hivyo ni lazima kufanya rejea mara kwa mara (updated)na kumsikiliza Bwana!

Hiyo ni hekima inayotazama upeo wa mababu na wazazi kwa maana waliweza kutoa jibu kwa matumaini kwa Mungu: ili kuipata hekima hiyo lazima kutazama ulimwengu, hali zetu na matatizo yetu, lakini yote hayo ni kwa njia ya  kutazama kwa macho ya Mungu, kuwasikiliza wengine kwa masikio ya Mungu, kuwapenda  wengine kwa moyo wa Mungu na kuthamini mambo kwa thamani ya Mungu.

Hekima ya Mungu inasukuma na kupinga uongo wa ahadi za furaha ambazo zinapelekea ubinafsi tu na kusaidia kuwakaribisha au kuwapokea wale ambao wanatenda au kufikiria tofauti na sisi. Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa: ni lazima kutoa ubinafsi wa kijifungia katika ulimwengu mdogo, au ubinafsi huo ndiyo ukawa msingi wa kwaheri ya kuonana. Akifafanua hiyo, anasema, iwapo watu, dini fulani na jamii inageuka kuwa dunia ndogo, hupoteza ubora wake na kutumbukia ndani ya mantiki za kujidai na kutawala, mimi ni bora na wewe ni mbaya.

Amesisitiza hayo kujibu maswali na kuwalenga vijana wawili, Upasana na Anthony kwa maneno ya kwanza waliyosema. Kwa njia hiyo msingi wa ujumbe wake ni hekima ya Mungu ambayo inafungulia upeo kwa wengine na kusaidia kutazama upeo ziadi, kuliko kukaa katika usalama wa uongo. Na kwa kufanya hivyo hekima itasaidia  usiwe kiziwa mbele ya mawazo makubwa ambayo yanasaidia kuishi maisha ya hadhi. 

Baba Mtakatifu amefurahi pia kusikia kuwa, pamoj na uwepo wa vijana Katoliki katika chuo hicho, ni mchanganyiko wa vijana wa madhehu mengine. Kwa njia hiyo anasema, kukutana kwao pamoja ni kuonesha ari waliyo nayo ya umoja mahali wanaweza kusaidiana na kuazimia kuwa na umoja pamoja na tofauti za kidini. Uzoefu huo umemsaidia kuonesha kwa vijana, uzoefu wake alipokuwa Buenos Aires kwamba kuna kikundi kimoja cha wanafunzi walikuwa wakifanya ujenzi katika eneo moja maskini kwenye parokia. Vijana hao walikuwa ni wakatoliki katika jumuiya ya wayahudi, wote walikuwa wakifanya kazi pamoja kwa ajili ya wema wa pamoja. Walianzisha urafiki wa kijamii, pia kuwa na maazimio ya kusema hapana kwa kile ambacho kingeweza kuleta mabadiliko katika mtazamo wa malengo na maazimio yao.

Na mwisho anasema hekima ya Mungu inasaidia kutambua wema wa urithi kiutamaduni: Kwa kufafanua; utamaduni wao unafundisha kuheshimu wazee na hivyo anawashauri wasitumie muda mrefu kukaa katika simu za mkononi wakidharau ulimwengu ulio wazunguka. Ni lazima kufanya mazungumzo na wazazi, bibi na babu ili kuweza kutambua sehemu msingi ya kizamani; hiyo ni kuifanya hija au kusafiri katika nyakati wakati huo huo, ni hali halisi mbayo ni kubwa katika maisha ya kizazi cha sasa na endelevu! 

Wakristo wanapata matumaini kwa njia ya kukutana na Yesu katika sala, Sakramenti. Aidha  kukutana na Yesu katika watu maskini, wagonjwa na wanaoteseka. Kwa neno moja anasema, Yesu anajionesha kwa njia ya mshikamano na Mungu! Akiwatazama nyuso zao zimejaa furaha na matumaini  kwa ajili yao na kwa ajili ya nchi yao, kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya Jumuiya nzima na hivyo Mungu abariki Bangladesh.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.