2017-11-24 09:29:00

Papa:Kwa sala tupande mbegu ya amani katika ardhi ya Sudan Kusini na DRC!


Kwa sala tunataka kupanda mbegu ya amani katika ardhi ya Sudan ya Kusini na ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, na kila ardhi iliyojeruhiwa na Vita. Nilikuwa nimeshapanga kutembelea nchi ya Sudan ya Kusini, lakini haikuwezekana, pamoja na hayo  tunatambua kuwa sala ni muhimu kwasababu ni yenye nguvu: sala na imani na kazi ya Mungu ambaye kwake yeye hakuna lisilowezekana. Ni katika maneno ya Papa Francisko kwenye  mkesha wa sala ya kuombea nchi hizo, iliyofanyika tarehe 23 Novemba 2017 saa 11.30 jioni masaa ya Ulaya katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican.

Akiendelea na tafakari lake wakati wa mkesha huo, Papa amewashukuru kwa moyo wote waliojikita kupanga, kuandaa kwa  juhudi  zote hadi kufanikisha mkesha huo. Ameendelea kusema: “Kwani Kristo mfufuka ametualika Aleleluya” ni maneno ya wimbo katika lugha ya kiswahili yaliyosindikiza maandamano ya kuingia Kanisani, wakiwa wameshika picha kutoka nchi mbili kwa nmna ya pekee tunazo ombea. Kama wakristo tunaamini na kutambua kuwa amani inawezekana kwasababu Kristo amefufuka. Yeye anatoa zawadi ya Roho Mtakatifu ambaye tumemwomba.

Papa anaendelea kusema: Na kama alivyokumbusha Mtakatifu Paulo, Yesu Kristo ni amani yetu (Ef 2,14). Yeye msalabani alichukua ubaya wote wa ulimwengu ikiwa ni pamoja na  dhambi zinazozalisha na kuendeleza vita: kiburi, uchu, tamaa ya madaraka, uongo … vyote hivyo  Yesu alivishinda kwa njia ya ufufuko. Na hata alipowatokea marafiki zake aliwambia “Amani kwenu” (Yh 20,19.21.26). Lakini hata leo hii jioni anarudia kusema hayo “Amani kwenu”.
Papa ameendelea na sala akisema, bila wewe Bwana, hata sala zetu na matumaini ya amani ni bure. Lakini Wewe unaishi na unafanya kazi ndani mwetu kwa ajili yetu, pamoja nasi maana  wewe ni amani yetu. Bwana mfufuka avunje kuta za uadui ambazo leo hii zinagawana ndugu na  kwa namna ya pekee katika nchi ya Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Awe kimbilio la wanawake waathirika wa migogoro katika sehemu za kivita na kila sehemu ya dunia.

Awaokoe watoto wanaoteseka kwasababu ya migogoro ambayo wao hawatambui, lakini inayowaibia utoto wao na awakati mwingine hata maisha. Ni jinsi gani upo unafiki wa kujifanya kuwa kimya au kukataa kuwa kuna vifo vya wanawake na watoto! Baba Mtakatifu anasisitiza “hapa ni kuonesha uso mbaya zaidi wa vita!

Bwana awasaidie  wadogo wote na maskini wa ulimwengu ambao wanaendelea kuamini na kutegemea ufalme wa Mungu kuwa huko karibu, na uko kati yetu ambao ni wa haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu (Rm14,17). Awasaidie wote ambao siku baada ya siku wanajikita kupambana na ubaya kwa  wema, kwa ishara na maneno ya udugu, wa heshima wa kukutana na wa mshikamano.

Bwana aimarishe kwa watawala na katika viongozi, wahusika wote ili wawe na  roho nzuri, haki, uthabiti na ujasiri katika kutafuta amani kupitia mazungumzo na majadiliano. Na mwisho Baba Mtakatifu amemalizia akitoa maombi kwamba: Bwana awezeshe kila mtu kuwa mtendaji wa amani kila mahali tulipo, katika familia, shuleni, kazini, katika jamuia, katika kila mazingira; "kwa kuoshana miguu kila mmoja, kwa mfano wa Mwalimu na Bwana. Kwake yeye ni utukufu na sifa, leo na hata milele Amina.

Hata hivyo katika sala kwa ajili ya uongofu wa kushinda sintofahamu na mgawanyiko, ndiyo sala iliyofungua maadhimisho ya mkesha huo katika Altare ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, ikifuatiwa sala kwa ajili wanawakeawaathirika wa migogoro, kwa ajili ya wale wanaosababisha vita na wahusika wa Jumuiya ya kimataifa au mahalia. 

Vile vile hata kwa ajili ya waathirika wasio kuwa na hatia au kwa ajili ya wale wanaojikita mstari wa mbele kusaidi watu wa Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo. Katika mkesha huo, kila aina ya sala imesindikizwa na somo la Biblia kutoka katika Agano Jipya na nyimbo za lugha mbalimbali. Kabla ya sala ya mwisho ya Baba Yetu, imetanguliwa na sala ya Mtakatifu Francisko wa Asizi juu ya amani ambayo wamesali kwa pamoja: “Bwana nifanye niwe chombo cha amani":

Ee Bwana unifanye niwe chombo cha amani yako, Palipo na chuki nilete mapendo;Palipo na makosa nilete msamaha, Palipo na shaka nilete imani. Pasipo na matumaini nilete tumaini; Palipo na giza nilete mwanga, Palipo na huzuni nilete furaha.

Ee Bwana unisaidie nitamani sana: Kufariji kuliko kufarijiwa; Kufahamu kuliko kufahamiwa; Kupenda kuliko kupendwa; Kwa kuwa: Ni katika kutoa ndipo tunapokea; Ni katika kusamehe ndipo tunaposamehewa. Ni katika  kifo ndipo tuna zaliwa katika uzima wa milele.
                          AMINA  

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.