Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kanda ya Mashariki kufanyika Zanzibar 2019

Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tanzania ameongoza hivi karibuni hitimisho la Kongamano la Ekaristi Kanda ya Mashariki

23/11/2017 09:17

Maaskofu wa Kanisa Katoliki Kanda ya Mashariki nchini Tanzania,wamesema ili kuendeleza Ibada na heshima kwa Ekaristi Takatifu wameridhia kufanya Kongamano la Ekaristi Takatifu kila baada ya miaka mitatu, kwa njia hiyo Kongamano mwaka 2019 litafanyika katika Jimbo Katoliki Zanzibar.
Hayo yametolewa hayo wakati wa kilele cha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kanda ya Mashariki lililofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Tanzania. Wakati wa maadhimisho hayo, Kardinali Polycap Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam  amesoma maazimio hayo na kuthibitisha kuwa,Kongamano la Ekaristi Takatifu mwaka huu,limekuwa ni neema na baraka kwa waamini wote walioshiriki maadhimisho hayo na kwa Kanisa kwa ujumla.

Na katika kuendeleza neema na baraka hizo za Mungu kwa taifa kama Maaskofu wa Kanda ya Mashariki, baada ya kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa waamini, makleri na wanakongamano wote, wamekubaliana kufanya  Adhimisho la Kongamano la Ekaristi katika Kanda ya Mashariki kila baada ya miaka mitatu. Kutokana na hilo azimio Kongamano la pili la Ekaristi Takatifu  katika Kanda ya Mashariki litafanyika Jimbo Katoliki Zanzibar Juni 2019. Hata hivyo ametoa pia sababu ya kutofanyika 2020 kwamba, ni mwaka wa uchanguzi Mkuu katika nchi ya tanzania ambapo wasiweze kuchangnanya mambo mawili pamoja. 

Halikadhalika amesema,ili kuendeleza ibada na heshima kwa Ekaristi Takatifu maaskofu hao wameazimia kuwepo na kuendelezwa kwa makanisa ya kuabudu daima Ekaristi Takataifu, ambamo Ekaristi Takatifu itawekwa na kuabudiwa kwa masaa 24 kila siku. Makanisa hayo yajengwe kwenye majimbo yote ya Kanda ya Mashariki na waamini wanaombwa kujitokeza kwa wingi kwenda kuabudu Ekaristi Takatifu ili  waweze kuchota  neema ya ukombozi. 
Maazimio mengine yaliyotolewa ni kwamba ili kuendeleza malezi ya kiimani kwa watoto na kuwezesha kutambua na kuthamini nafasi ya Ekarist i Takatifu katika maisha ya kikristo washiriki wa kongamano hilo wameazimia kuzifanya familia na parokia zao kuwa vituo vya katekesi na mafundisho endelevu na kina  ya imani kuhusu Ekaristi Takatifu kwa watoto wao.

Hivyo wito ni kwa kwa mapadri, watawa, makatekista, wazazi na walezi wote kusitawisha utume wa Utoto Mtakatifu na kuwawezesha watoto wote kuwa washiriki wa Shirika hilo la  Utoto Mtakatifu ambalo ni chombo muhimu cha kukuza imani na moyo wa umisisonari kwa watoto wetu.
Na wakitazama juu ya familia Kardinali Pengo,amesisitiza juu ya Wanandoa wanaojiandaa kupokea sakramenti ya ndoa na wale ambao tayari wamepokea Sakramenti hiyo wapewe katekesi na mafundisho ya kina kuhusu Ekaristi Takatifu ili watambue kuwa furaha na upendo wa ndoa zao zinategemea moja kwa moja muungano wao na Yesu wa Ekaristi. Bila Ekaristi Takatifu hakuna uhai wa kimungu ndani ya familia. Kadhalika ili kuwezesha waamini kuwa na ibada za mara kwa mara za Ekaristi Takatifu, parokia zote katika Kanda ya mashariki zinapaswa kuwa na utaratibu wa kufanya ibada na kuabudu Ekaristi Takatifu mara moja kwa juma. Waamini wajitokeze kwa wingi kushiri ibada hizo.

Kilele cha Kongamano hilo kilikuwa cha namna yake ambapo palikuwa na maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Tanzania hadi Msimbazi kwa maadhimisho hayo.
Kongamano hilo lilianza tarehe 10-12 Novemba 2017, na kuudhuriwa na maelfu ya waamini wakiwemo maaskofu, mapadri na waamini walei kutoka majimbo yanayounda Kanda hiyo ya Mashariki ambayo ni Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Ifakara, Tanga, Morogoro, Zanzibar na Mahenge. Mkuu wa Kanda hiyo ni Askofu Mkuu Polycarp Pengo.

 

23/11/2017 09:17