2017-11-15 16:37:00

Papa:Sala ni kukutana na Upendo wa Mungu kwa njia ya Neno,Mwili na Damu


Tunaendelea na Katekesi juu ya Misa Takatifu na ninapendelea kuanza na  mantiki rahisi ambayo inasaidia kuelewa uzuri wa maadhimisho ya Ekaristi. Misa ni sala, zaidi ya hayo ni sala kuu, iliyo ya juu zaidi na ya ukuu wake, wakati huo huo ni ya “dhati”. Kwa maana ni kukutana na upendo wa Mungu kwa njia ya Neno, Mwili na Damu ya Yesu.

Ni Maneno ya takafakari ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoanza nayo wakati wa katekesi ya Jumatano 15 Novemba 2017 katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa mahujaji wote kutoka pande zote za dunia. Katika kuelezea nini maana ya maadhimisho ya   misa, anaendelea kusema, kwanza ni lazima kujiuliza swali nini maana kweli ya sala?  Akitoa jibu anasema, hawali ya yote ni mazungumzo na uhusiano binafsi na Mungu. Binadamu ameumbwa ili awe na uhusiano ambao tayari ni utimilifu wa kukutana na Muumba wake. Kwa namna hiyo njia ya maisha ni kukutana na Bwana mwisho wake.

Katika Kitabu cha Mwanzo kinaonesha kuwa, binadamu aliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ambaye ni Baba,Mwana na Roho Mtakatifu. Huo ni uhusiano kamili wa upendo ambao ni umoja. Kwa hali hiyo tunaweza kutambua sisi sote kuwa tumeumbwa ili tuweze kuingia katika uhusiano kamili wa upendo na unaoendelea kutolewa  ili tuweze kufikia ule utimilifu kamili. 

Musa alipokuwa mbele ya kichaka kinachounguzwa, alimwuliza Mungu, jina lake, na Mungu akajibu ”Mimi ndiye niliye” (Kut 3,14). Hayo ndiyo maelezo katika uasili wake, kwa maana ya kuonesha uwepo hai, wakati huo huo  Mungu aliongeza kujidhihirisha ni nani, “Mwenyezi Mungu wa Babu zenu, Mungu wa Hibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Baba Mtakatifu anasema, hata Yesu alipowaita Mitume wake, anawaita ili waweze kukaa naye. Hii ni neema kubwa ya kuweza kujieleza katika ekasti   ambao nifursa nzuri ya kukaa na Yesu na kwa njia Yake na Mungu na kwa ndugu.

Katika mazungumzo na Bwana kuna kipindi cha ukimya, kwa maana ya kufanya  ukimya na Yesu. Tunapoudhuria misa, wakati mwingine tunafika mapema Kanisani lakini na kuanza mazungumz na wengine, badala ya kutulia kwa utulivu. Lakini tambua kuwa siyo wakati wa mazungumzo, ni kipindi cha ukimya wa kujiandaa ili ufanye mazungumzo ya kweli. Ni kipindi cha kujitafakari ndani ya moyo ili kuweza kukutana na Yesu. Ukimya ni muhimu sana! Baba Mtakatifu anawakumbusha kama alivyo waeleza wiki iliyo pita kuwa, ”hatuendi misa kama tamasha, bali tunakwenda kukutana na Bwana, kujiandaa kwa kusindikizwa na ukimya ili kukaa na Yesu.

Kusali kwa mazungumzo ya kweli ni kutambua kukaa kimya pamoja na Yesu. Na kutoka katika fumbo la ukimya wa Mungu, ndipo linazaliwa  Neno ambalo linajikita katika mioyo yetu. Yesu mwenyewe anatufundisha jinsi gani kwa hakika inawezakana kukaa na Baba anatuonesha kwa njia ya sala yake.  Injili zote zinaonesha jinsi gani Yesu anakwenda mwenyewe faragha kusali; Mitume walipoonda uhusiano wake wa kina na Baba yake, walijisikia shahuku ya kutaka nao kushiriki na wakamwomba Bwana awafundishe kusali (Lk11,1). 

Kama soma la kwanza lilivyo kuwa linaeleza katika Katekesi, Yesu aliwajibu kuwa, ili kuweza kujifunza kusali lazima watambue kutamka “Baba” maana yake ni kujiweka mbele yake kwa matumaini kama mwana. Ili kuweza kujifunza ni lazima uwe na utambuzi ya kwamba sisi sote tunahitaji kufundishwa naye na kusema kwa urahisi ”Bwana nifundishe kusali”.

Hiyo ndiyo hatua ya kwanza: yaani ya kuwa mnyenyekevu, kujitambua kuwa mwana, na kupumzika kwa Baba na kumwamini Yeye peke yake. Ili kuweza kuingia katika ufalme wa Mungu ni lazima kuwa mdogo kama watoto. Kwa maana ya kwamba watoto wanajikabidhi moja kwa moja bila kujibakiza, wanatambua kuwa huyo mtu atawaangaikia wao, juu ya chakula, kuvaa na mahitaji mengine kama Injili ya isemavyo(Mt 6,25-32). Baba Mtakatifu anabainisha, hiyo ndiyo tabia ya kwanza ya kutambu,imani na matumaini kama mtoto mdogo akiwalekea wazazi wake; yaani kuwa na utambuzi kuwa  Mungu anakukumbuka na kukutunza!

Hatua ya pili ni ile ya utayari, hiyo ni dhahiri kama ya watoto wadogo, ni kwa maana ya kujiachia katika mshangao. Watoto daima wanauliza maswali mengi kwa maana wanataka kugundua ulimwengu; wanashangazwa hadi kile  kidogo sana kwa maana kila kitu ni kipya kwao. Ili kuingia katika ufalme wa Mungu, Baba Mtakatifu anasisitiza ni lazima kujiachia katika mshangao. 
Hata hivy Baba Mtakatifu anatoa maswali akisema, je  uhusiano  wetu na Bwana, katika sala unatuacha katika mshangao? Je tunajiachia katika mshangao? 

Hiyo ni kwasababu   kukutana na Bwana daima ni kukutana uhalisia hai. Je tunajiachia kushangazwa au tunafikiria tu kwamba sala ni kuongea na Mungu kama wafanyavyo kasuku?  Hapana kusali ni kufungua moyo na kujiachia katika mshangao. Kukutana na Bwana aliye hai siyo kukutana na jumba la makumbusho. Ni kukutana na Bwana aliye hai na tunapokwenda katika misa siyo katika jumba la makumbusho, bali tunakwenda kukutana na Bwana.
Akiendelea na tafakari , Baba Mtakatifu anasema, katika Injili wanaongelea juu ya Nikodemus (Yh3,1-21) mtu mzima, mwenye madaraka huko Israeli ambaye alikwenda kwa Yesu kumjua ni nani . Naye Bwana alizungumz naye juu ya haja ya  kuzaliwa upya. Lakini ina maana gani? tunaweza kuzaliwa tena kwa upya? tunaweza kurudia haki ya furaha na mshangao wa maisha? Hayo ndiyo maswali msingi  ya imani yetu ,na ndiyo shahuku ya kila mwamini wa kweli, kwa maana ya kuwa na  shahuku ya kuzaliwa upya, kuanza furaha mpya tena. Baba Mtakatifu amewauliza umati mzima iwapo wanayo shahuku hiyo!

Hiyo ni kutokana na kwamba unaweza kupoteza kwa urahisi furaha na shahuku hiyo kutokana na  shughuli mbalimbali , mipango mingi ya maisha na mwisho hakuna muda, na tunapoteza kile ambacho ni msingi hasa maisha ya kiroho. Kwa hali hiyo Bwana anatushangaza  na kutuonesha kuwa Yeye anatupenda  hata katika maidhaifu yetu. Yesu Kristo ni mwathirika kwa maana ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote. (1Yh 2,2). Hiyo ni zawadi ya kweli na kitulizo ambacho kinatolewa katika Ekaristi, ni karamu ya arusi ambayo Bwana arusi anakutana na udhaifu ili kuweza kuturudisha katika wito wa kwanza ule wa kuwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anamalizia, hiyo ndiyo Ekaristi na ndiyo sala.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.