2017-11-13 10:49:00

Papa:Imani na matendo ya Upendo ni misingi ya utayari wa kukutana na Mungu!


Ili kuweza kuingia katika ufalme wa Mungu ni lazima kujitayarisha kukutana na Bwana . Haitoshelezi kuishi maisha ya imani tu iwapo hayaambatani na matendo ya upendo kwa jirani. Huo ni wito wa Baba Mtakatifu wakati wa mahubiri yake katika sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili 12 Novemba 2017 kwa mahujaji wote katika viwanja vya Mtakatifu Petro mjini Vatican, akitafakari Injili ya Siku kuhusu wanawali kumi, watano wakiwa na taa zenye mafuta na wengine watano kutokuwa na mafuta. Baba Mtakatifu Francisko anashauri kwamba,hakuna kusubiri wakati wa mwisho kujiandaa  katika maisha yetu ya kushirikiana na neema ya Mungu, ni lazima kuanza sasa hivi...

Kesheni, maana hamjuhi siku wala saa kama Injili inavyoeleza ya Jumapili ya 32 ya Mwaka A waKanisa, Baba Mtakatifu anasisitiza kuwa, Yesu anafundisha kukesha  akiwa na maana ya kwamba hatupaswi kulala tu, bali tunahitaji kujiandaa kila wakati. Ni lazima kujiandaa na kuwa tayari kukutana na Bwana kila siku kana kwamba ndiyo siku ya mwisho. Akitoa ufafanuzi juu ya taa anasema, taa ni ishara ya imani inayoangaza maisha yetu, mafuta ni ishara ya upendo ambayo inaimarisha na kukuza  matunda ya  kweli ya mwanga wa imani. Hiyo ni kwa sababu  ukikosa upendo wa dhati, unakosa hata mwanga wa kweli katika maisha yako ya kila siku.

Akisisitiza zaidi anasema, iwapo tunajiachia kwa kile kinachojitokeza katika macho yetu, kujifurahisha kwa manufaa yetu, maisha yetu yanazidi kuwa tasa, na ukosefu wa uwezo wa kutoa maisha kwa ajili ya wengine, vilevile hatuwezi kukusanya mafuta ya ziada kwa ajili taa za imani yetu na mwisho wakea taa hizo zitazimika wakati Bwana anakuja kwa mara nyingine tena.

Kwa njia hiyo  anafafanua hata hali ambazo zinaweza kutufanya tuwe tayari kukutana na Bwana na kusema kuwa, haitoshelezi kuwa na imani, maana maisha ya Mkristo yanapaswa daima kuwa na utajiri wa upendo, yaani kutoa upendo kwa jirani. Iwapo tunakesha na kujaribu kutilimiliza yaliyo mema au ishara za upendo, katika  kushirikishana, kufanya huduma kwa jirani aliye katika matatizo, hiyo ndiyo inaweza kutufanya tuwe na utulivu wa kusubiri Bwana arusi atakapokuja.

Anaongeza kusema kuwa, Bwana anaweza kufika wakati wowote, hata tukiwa  katika usingizi wa kifo kwani hatuwezi kuogopa kwa maana tumeweza kukusanya mafuta ya ziada kwa njia ya matendo mema ya kila siku. Hivyo ni kusema kuwa imani yetu inatokana matendo ya upendo na matendo ya upendo yanahifadhi umani ya kweli.

Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko ametukumbusha kuwa Jumamosi 11 Novemba 2017 huko Madridi alitangazwa mwenye heri  Queralt Loret na wenzake 20 wafia dini pia  José Maria Fernández Sánchez na wenzake 38 wafia dini katika nchi ya Hispania. Hawa wote waliuwawa kwa sababu ya kutetea imani yao wakati Wakristo wanateswa  kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Hispania kati ya mwaka 1936 -1937. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anaongeza kusema kuwa, tumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya mashahidi wa hawa wa kuigwa wa Kristo na Injili yake.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.