2017-11-07 16:30:00

Ujermani: Mkutano wa Cop23 unafanyika mjini Bonn kuhusu Mazingira


Mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi unaanza rasmi tarehe 6 Novemba 2017 mjini Bonn, Ujerumani kujadili jinsi ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Paris yanayolenga kuzileta nchi pamoja kupunguza viwango vya joto duniani. Waziri mkuu wa Fiji Voreqe Bainimarama ameufungua rasmi mkutano huo wa Cop23  kwa kusema  kuwa anataka hatua za dharura kuchukuliwa kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani kama sehemu ya yaliyofikiwa katika makubaliano ya Paris na hilo linahitaji kila mmoja kuwa na nia njema kulifikia.

Bainimarama ameonya kuwa nchi yake na nchi nyingine za visiwa vya Pacifik ziko katika hatari kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji baharibi na mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa. Na licha ya kuwa Fiji bado haijakumbwa na vitisho vikubwa kama nchi jirani, tayari inakabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks amezungumzia umuhimu wa kuyalinda mazingira na kuahidi nchi yake itatoa msaada wa kifedha kuyalinda mazingira.

Takriban watu 25,000 kutoka nchi 195 wanahudhuria mkutano huo wa mazingira unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Ujerumani ndiyo mwenyeji wa mkutano huo wa kujadili mabadiliko ya tabia nchi ujulikanao Cop23, licha ya kuwa Fiji ndiyo inashikilia urais. Wanadiplomasia, wanamazingira, wanaharakati, na wanasiasa wanakutana hapa mjini Bonn kwa kipindi cha wiki mbili zijazo kujadiliana ni namna gani watayaokoa mazingira kwa kupunguza viwango vya joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili. Kadhalika, makubaliano hayo yanalenga kushajaisha uwezo wa nchi mbali mbali kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Ili kuweza kufikia malengo hayo, kunahitajika fedha za kutosha, matumizi ya teknolokjia mpya, na nchi zinazoendelea kusaidiwa pia kuyafikia malengo yake. Mkutano huo wa mazingira unatarajia kuwa nchi zote husika zitachukua hatua za ziada kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatekelezwa kikamilifu. Mwaka ujao, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizotia saini makubaliano ya Paris yatafanya tathmini ya hatua za pamoja zilizofikiwa.
Mkutano huu unaokuja miaka miwili tangu kufikiwa makubaliano ya Paris, unafanyika wakati kuna mashaka baada ya Rais wa Marekani Donald Trump mwezi Juni mwaka huu kutangaza nchi yake itajiondoa kutoka makubaliano hayo licha ya ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa serikali ya Marekani kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwa athari za mabadiliko ya tabKimsingi masuala matatu makuu yanayoshughulikiwa ni kuwianisha vipengele vya makubaliano ya Paris, utekelezaji wake na kile kinachojulikana mfumo wa kiutendaji. Ifikapo mwaka 2020 nchi ziwe zimeweza kuimarisha ahadi zake za kupunguza viwango vya joto duniani kwa kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Takriban viongozi 20 wa nchi wanatarajiwa kuhudhuria akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ni miongoni mwa viongozi mashuhuri watakaohutubia mkutano wa Cop23. Nchi 49 tayari zimeongeza mikakati yao ya kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani na inakadiriwa ifikapo mwaka 2030, idadi ya nchi ambazo zitakuwa zimepiga hatua inatarajiwa kufika 57, zikiwemo China, Brazil, Marekani na Mexico.
Shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO limewasilisha ripoti pia tarehe 6 Novemba  katika mkutano wa mazingira wa Bonn inayoonesha kuwa mwaka huu wa 2017 ndiyo unaotajwa kushuhudia viwango vya juu zaidi vya joto duniani kwa zaidi ya nyuzi 1.1 hiyo ikiwa hali mbaya ya hewa ambayo haikutarajiwa katika nchi zinashuhudiwa.

Sr Angela Rwezaula 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.