2017-11-02 15:49:00

Papa:Katika sala ya Baba Yetu,Jina la Mungu linatakaswa na kutukuzwa!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna nyakati anapokwenda kusali, anajikuta anauchapa usingizi kisawasawa hali akiwa anasali sababu ya uchovu mwingi. Ingawa asingependa hilo litokee, lakini anatambua kuwa hali hiyo inamkuta kufuatia uhalisia wa udhaifu wa binadamu anapokuwa amechoka sana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, suala hili linamfanya ajisikie kama mtoto mdogo aliyebebwa kwenye mikono ya baba yake mzazi, hivyo anajiaminisha kwenye mikono ya Mwenyezi Mungu. Ilikuwa ni sehemu ya mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Padre Marco Pozza, wakati wa kipindi cha “Padre nostro”, sala ya Baba yetu, siku ya Jumatano tarehe 1 Novemba 2017, kwenye kituo cha luninga cha Tv2000.

Kituo cha luninga Tv2000 kinamilikuwa na kuendeshwa na Baraza la maaskofu nchini Italia, ambapo hivi karibuni kimeweka kipindi hicho cha “Padre nostro”, katika kuenzi sala ya Baba yetu na maisha ya sala kwa mkristo. Kipindi hicho kitakuwa na sehemu tisa, na kinarushwa kila Jumatano, majira ya saa 3 usiku, kwa saa za Ulaya. Kipindi huongozwa na Padre Marco Pozza, ambaye ni Padre Mhudumu wa gereza la wafungwa huko Padua, na kwa kawaida kunakuwa na wageni waalikwa, walei waliobobea kwenye masuala ya utamaduni wa taifa pamoja na maonesho.

Jina la Mwenyezi Mungu linatakaswa na linatukuzwa kwa namna nyingi, ikiwa ni pamoja na pale ambapo wanadamu wanapojitambua na kujisikia watoto mikononi mwake Baba wa wote, Baba wa milele, anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hata hivyo inasikitisha kuona kwamba wengi hujitambulisha kuwa wakristo, wana wa Mungu, lakini kiuhalisia wanaishi kana kwamba hawamwamini wala kumtambua Mungu. 

Wengi hudai kuwa wakristo, watoto wa Mungu, lakini hutenda mambo ya uovu na ukatili bila kujali binadamu wenzao kama ndugu. Chuki, kinzani, vita, mafarakano, ushindani, dhuluma, na uonevu vimetawala nyoyo za watu kwenye kila sekta na fani: siasa, uchumi, biashara, kazi, ndoa na familia, na kadhalika. Baba Mtakatifu anawaalika wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, walitakase na kulitukuza jina la Bwana kwa kutenda mema, kuwa wenye upendo na kujali, wakimtambua Mwenyezi Mungu kuwa Baba wa kweli na mwenye upendo na huruma kwa wanadamu wote, ambao wanapaswa kuishi kidugu.

Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.