2017-10-31 15:50:00

Sikukuu ya Watakatifu wote:Utakatifu si kwa ajili ya wachache,ni kwa wote!


Kanisa limeweka siku ya leo kwa ajili ya kuwaadhimisha Watakatifu wote. Tunafahamu kuwa ipo orodha rasmi ya watakatifu ambao Kanisa limewatangaza na limepanga maadhimisho yao katika siku mbalimbali ndani ya mwaka wa kiliturujia wa Kanisa. Pamoja na orodha hiyo, Kanisa linatambua pia wapo waamini ambao baada ya maisha yao hapa duniani wamepewa tayari tuzo la utakatifu huko mbinguni. Hawa ni maelfu kwa maelfu na miongoni mwao huenda wamo wazazi wetu, bibi na babu zetu, watoto wetu, ndugu, jamaa na wengine wengi ambao wameishi kwa kumtafuta Mungu na kutimiza mapenzi yake katika maisha yao.

Kwa kuwaadhimisha watakatifu hawa ambao  ni umati usiohesabika kutoka kila taifa, kabila, jamaa na lugha, Kanisa linaweka karibu zaidi nasi sura ya utakatifu. Utakatifu sio nafasi waliyotengewa wachache au kundi maalum la watu pekee bali ni nafasi ya wote ukiwamo na wewe unayenisikiliza muda huu. Mungu ametuumba ili tuufikie utakatifu, yaani tuishi naye milele. Ndivyo katekisimu yetu kwa njia ya maswali inavyotueleza; Kwa nini Mungu ametuumba? -Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende na tumtumikie tupate kufika kwake mbinguni.

Maisha ya watakatifu tuliopata kuwafaham, ama kupitia kusoma historia za maisha yao au wale tuliowaona, mfano  Mtakatifu Yohane Paulo II, Mtakatifu Mama Teresa wa Kalkuta na wengine wa nyakati zetu, yanatufundisha kuwa zipo aina nyingi sana za kuufikia utakatifu aliotuitia Mwenyezi Mungu Baba yetu. Aina hizi zimesambaa katika kila mazingira kama vile, mfumo wa maisha, miito, kazi na hata katika tabia mbalimbali tulizonazo wanadamu.  Mojawapo ya njia hizo ni hii inayoelezwa katika kitabu cha Ufunuo kama tulivyosikia katika somo la kwanza kuwa ni sifa waliyokuwa nayo wale maelfu waliosimama mbele ya kiti cha enzi.  Watu hao “...wametoka kwenye dhiki kuu nao wamefua mavazi yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo” (Uf.7:14).

Mababa wa Kanisa wamefafanua kifungu hiki katika tafsiri mbili. Ya kwanza ni kwamba watu hao ni wafiadini waliokufa kwa kuteseka kwa ajili ya imani yao na kuwa hiyo dhiki kuu ni madhulumu wanayopitia wafuasi wa Kristo. Tafsiri ya pili ya mababa wa kanisa ni kuwa damu ya mwanakondoo ni nguvu ya sadaka ya Kristo Msalabani inayowatakasa wote wanaojiweka chini yake. Tafsiri hizi mbili zinaweka mbele yetu kifodini (ushuhuda) na toba (utakaso tuupatao kwa njia ya Kanisa).  Kumbe ushuhuda na toba vinawekwa kwetu leo na maandiko matakatifu kama njia tunayopaswa kuitumia ili kuufikia utakatifu tulioitiwa.

Ndugu msikilizaji, katika maneno rahisi kabisa, shahidi ni yule mtu anayethibitisha usahihi wa maelezo, jambo au matendo ya mtu mwingine. Kwa ubatizo wetu sisi tumemvaa Kristo na ndio maana tunaitwa Wa-Kristo. Jina na cheo hiki kinatuwajibisha kuonesha picha sahihi ya Kristo katika maisha yetu, na huku ndiko kutoa ushuhuda.

Papa Fransisko hukazia kuwa Ukristo sio dini ya fikra, teolojia, vitu vizuri au amri pekee bali ni watu wanaomfuasa Kristo na kumshuhudia katika maisha yao. Kwa Papa Fransisko mkristo anapaswa kutoa ushuhuda huu kwa namna tatu; kwa maneno yake, kwa namna moyo wake ulivyo na kwa mikono yake. Hata katikati ya changamoto zinazoibuka kila kukicha dhidi ya imani yetu, tusichoke, tusikate tamaa, tusiogope na tusione aibu kuwa mashahidi wa Kristo katika maeneo ya kazi, biashara, siasa, familia na maisha yetu kwa ujumla wake.

Ni muhimu njia hii ya ushuhuda kuambatana na njia ya toba; njia ya msamaha, wongofu na upatanisho kwa Mungu na kwa jirani. Hii ni kwa sababu sote tu wadhambi, na kadiri tunapozidi kukaa katika dhambi ujasiri wetu kutoa ushuhuda unapotea na unapotoka. Njia ya kuelekea utakatifu ni njia ya kujitakasa kila wakati. Tusione haya kuijongea sakramenti ya kitubio, kama ni kuona haya basa tuone haya kuingia dhambini.

Bikira Maria Mama yetu aendelee kuwa kioo na taa yetu tunaposafiri kuelekea utakatifu ambao yeye anaushiriki kwa mastahili ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. William Bahitwa
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.