Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Ni ukweli usiopingika kwamba wewe unapendwa nawe basi penda!

Ina ya Nne ya Upendo ni upendo wa kimungu. Huu huitwa agape. Ni upendo anaouonesha Mungu kwa viumbe vyake vyote.

28/10/2017 09:28

Leo tunaadhimisha Dominika ya 30 ya Mwaka A wa Kanisa. Maandiko Matakatifu yanaweka mbele yetu dhamira ya Upendo ili kutusindikiza katika tafakari yetu ya  siku ya leo. Ni ukweli usiopingika kwamba Upendo ndio neno linaloongelewa zaidi kuliko maneno mengine yoyote. Tunalisikia katika mahubiri, katika ushauri, katika wosia, katika nyimbo, katika kazi za wasanii na maeneo mengine mbalimbali. Pamoja na kuwa neno linaloongelewa zaidi ya maneno mengine, upendo hugeuka kuwa kitu kinachokosekana zaidi ya vingine katika maisha ya mwanadamu katika ujumla wake.

“Mungu ni Upendo” anaandika Mtume Yohane na kutualika sote tupendane kwani yeye anayependa ni mwana wa Mungu na yeye asiyependa hamjui Mungu (Rej. 1Yoh 4:7 - 8). Ni Mungu aliyetangulia kutupenda na akawekeza kwetu upendo. Daima anatualika nasi tupende.
Karibu basi mpenzi msikilizaji wa Radio Vatikano katika tafakari hii fupi juu ya upendo kulingana na masomo ya dominika ya leo. 
Amri ipi ni kuu?.

Katika injili tunakutana na swali ambalo mwanasheria anamuuliza Yesu ili kumjaribu, “...katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Hii si mara ya kwanza Yesu kuulizwa swali la kumjaribu na mara zote waliomjaribu wameondoka wameinamisha vichwa! Wanasheria hawa walipaswa kujifunza kutoka kwa waliotangulia, lakini kama tujuavyo chuki na wivu huondoa busara walienda nao kumuuliza. Tena cha kushangaza zaidi, wale wasiofuata hata sheria ndogo wanauliza sheria kubwa ni ipi! Haidhuru, Yesu anatoa jibu.

Jibu la Yesu
Kutoka katika amri kumi Mungu aliwapa waisraeli mlimani Sinai, wanasheria wa kiyahudi walizichanganua na kuzifanya zifikie amri 613. Zote hizi wayahudi walipaswa kuzishika. Walipomuuliza Yesu swali huenda walitegemea Yesu ataje mojawapo kati ya hizo amri 613. Yeye hakunukuu hata mojawapo ya hizo bali aliwajibu “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yako yote na kwa akili yako yote” na pia “mpende jirani yako kama nafsi yako”. Hapa Yesu anatuambia Upendo ndio ufupisho wa amri zote na upendo ndio kilele cha amri zote. Yote yanapaswa kuanza na upendo, kufanywa kwa upendo na kwa lengo la upendo.

Upendo upi?
Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika barua yake Deus Caritas Est anafafanua kuwa zipo aina nne za upendo.
i. Kwanza ni aina ya upendo kama ulio kati ya ndugu au wanafamilia. Huitwa Storge. Upendo kati ya mzazi na mwanae, kati ya dada na kaka na kati ya ndugu.
ii. Pili ni aina ya upendo ulio kati ya wapenzi: wachumba au mke na mume. Huu ni upendo ambao pia unaambata na tamaa kati ya wapendano. Huitwa Eros.
iii. Tatu ni aina ya upendo ulio kati ya jamaa au katika jumuiya: upendo kati ya mkristo na mkristo mwenzake, upendo katika jumuiya ndogondogo, katika jumuiya za kitawa, mapadre nk. Huitwa Filia.
iv. Nne ni upendo wa kimungu. Huu huitwa agape. Ni upendo anaouonesha Mungu kwa viumbe vyake vyote. Kama asemavyo mwinjili huwanyeshea mvua waovu kwa wema na kama asemavyo mzaburi hushibisha kila kilicho hai matakwa yake.

Katika aina ya kwanza hadi ya tatu, mtu humpenda mwingine akiwa na sababu; ni ndugu yangu, ni mke/mume, ni mkristo mwenzangu, ni mtu wa kabila langu na kadhalika. Pia mtu humpenda mwingine kwa sababu ya alichonacho (alichotoa au anachoweza kutoa) iwe ni kitu, mali au hisani. Katika aina ya nne, Mungu anatufundisha kupenda si kwa sababu nyingine yoyote ile ila tu kwa kuwa sote ni wanawe na tunabeba sura na mfano wake. 
Katika uchambuzi huu Baba Mtakatifu Mstaafu, Benedikto alitualika tusafiri daima kuelelea upendo wa agape. Tupendane si kwa sababu ya maslahi fulani ila kwa sababu sote ni wana wa Mungu na Mungu anatupenda sote. Upendo huu wa agape pia unapaswa kuwa ndio msingi katika aina nyingine tatu za upendo. Unapaswa kuwa hivyo kwa sababu bila ya huo mahusiano hayo pia hugeuka kuwa yenye ubinafsi, ya kimanufaa na ya kiubaguzi hasa kwa wasio nacho na wasiojiweza hata kati ya wanafamilia, wanandoa na wanajumuiya mbalimbali.

Mungu kwanza
Yesu anapojibu anaweka upendo kwa Mungu katika nafasi ya kwanza. Ndio kusema kuwa yeye asiyempenda Mungu hawezi kuiona sura ya Mungu kwa jirani yake na hawezi pia kuiona sura ya Mungu ndani yake. Kwa jirani hataguswa na mahitaji wala mahangaiko yake na hata kwake mwenyewe ama ataishia kujikatia tamaa ama atakuwa na majivuno akihesabu mafanikio yake kuwa ni matokeo ya juhudi zake mwenyewe.
Kumpenda Mungu ni kujiweka chini ya maongozi yake daima na tena ni kumpa haki yake anayostahili; kuabudiwa, kuheshimiwa, kutukuzwa, kusifiwa na zaidi ya yote kushika amri zake katika maisha yetu. 

Mpenzi msikilizaji wa Radio Vatican, tuimalizie tafakari yetu kwa kuwaangalia baadhi ya maadui wa upendo. Hawa ni chuki, wivu na kuwatia wengine katika majaribu. Maadui hawa ndio tunaowaona waliwajaa wanasheria walioenda kumuuiza Yesu swali. Lengo lao lilikuwa ni kumjaribu ili wamuangamize; kwa nini wamuangamize huenda ni kwa sababu walimchukia na tena walimuonea wivu kwa sababu yeye alikuwa na wafuasi wengi kuliko wao.
Hatuwezi kuufikia upendo wa kweli kama bado tunaruhusu kutawaliwa na chuki kwa wenzetu, kama bado tunawaonea wivu kwa majaliwa mbalimbali waliyonayo na kama mioyoni mwetu tunakusudia kuwatia majaribuni ili kuwaangamiza.

Mungu mwenyezi aliye asili ya upendo aongoze hatua zetu tuufikie upendo wa kweli ndani yetu, tumpende Yeye kama anavyostahili na tuwapende wenzetu kama anavyotupenda. Mama Bikira Maria, msaada wa wakristo atuombee na kutusaidia daima.
Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. William Bahitwa

 

28/10/2017 09:28