Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Kitabu cha Ask.Marchetto ni utafiti wa kutafsiri Mafundisho ya Mtaguso wa II!

Kitabu cha Askofu Mkuu Marchetto kizungumzia mabadiliko mbalimbali ya utume na maisha ya Kanisa kwa ujumla, hususani mahusiano kati ya Kiti cha Khalifa wa Mtume Petro na Upamoja wa Sinodi ya Maaskofu. - ANSA

27/10/2017 10:53

Siku ya Jumatano, tarehe 25 Oktoba 2017, kwenye ukumbi wa Campidoglio jijini Roma, kimetambulishwa kitabu La Riforma e le Riforme nella Chiesa. Una risposta, kilichoandikwa na Askofu mkuu Agostino Marchetto. Kitabu kinachozungumzia mabadiliko mbalimbali ya utume na maisha ya Kanisa kwa ujumla, hususani mahusiano kati ya Kiti cha Khalifa wa Mtume Petro na Upamoja wa Sinodi ya Maaskofu. 

Wakati wa utambulisho wa kitabu hicho, Padre Dario Viganò, Mwenyekiti wa Sekreteriat ya Mawasiliano ya Vatican, ametoa hutuba yake akionesha ni jinsi gani maisha ya Askofu mkuu Marchetto yalijikita sana mbali ya shughuli nyingi za kitume, lakini pia utafiti juu ya kutafsiri vizuri Mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatican.

Monsinyo Viganò anasema kwamba, kufahamu vizuri Mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatican ni hali ya kujiweka sawa kupokea na kufaidi zawadi hiyo yenye neema nyingi ambayo Mwenyezi Mungu amelitunukia Kanisa. Akitoa mfano wa kumzawadia rafiki Computer na asijue kuitumia, amesema, kutofahamu vema zawadi ya Mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatican, ni sawa na kuwa na zawadi usiyoijua thamani yake na hivyo kutofaidi matunda ya zawadi husika.

Katika kutafsiri Mtaguso wa Pili wa Vatican, mtu anakumbana na miale miwili ya moto mmoja. Miale hii ni Upyaisho na Desturi, Mabadiliko na Uhifadhi wa Tamaduni (conservatism). Miale hii haipaswi kuonekana kama nguvu mbili zinazovutana, bali utajiri wa moto mmoja wa Roho Mtakatifu, anayelitengeneza na kulidumisha Kanisa katika utume wake, akiliongoza kuelekea Mji Mtakatifu katika Paradiso. Ni katika kutambua hilo, Askofu mkuu Marchetto amefanya utafiti ili kutoa mwanga zaidi juu ya mahusiano kati ya Upamoja wa Maaskofu katika Mtaguso au Sinodi na Kiti cha Khalifa wa Petro, yaani nafasi ya Baba Mtakatifu katika Upamoja huo, ambapo Baba Mtakatifu hawi mwenye madaraka ya pekee dhidi ya wenzake kama mamlaka za kidunia zilizvyo, bali anakuwa wa kwanza kati ya walio sawa.

Katika mtazamo wa haraka haraka, kuna ugumu wa kuelewa mahusiano na nafasi za mababa hawa ndani ya mamlaka za Kanisa. Hata hivyo katika ukweli wa maisha ya kikristo, kwa kawaida kuna ugumu kuelewa ushabiiano wa uhalisia wake. Mfano, kutafuta ushabiiano kwenye Mafundisho ya Mungu Mmoja Nafsi Tatu, au Kristo Yesu Mungu-Mtu, au Mama Maria kuwa Mama wa Yesu na wakati huo huo kubaki Bikira. Mafundisho haya kwa akili za wasomi wa dunia yanaonekana kama umaskini fulani wa kufikiri, lakini kwa akili yenye imani, ni mwamsho wa kufikiri zaidi, kukuza uelewa juu ya Mungu na ulimwengu, na kukomaza imani ili kuuona upendo, ukarimu, huruma na msamaha wa Mungu kwa wanadamu. 
Hivyo katika kuyatafsiri na kuyaelewa mafundisho ya namna hii, kunahitajika imani na sio kung’ang’ana na ubishi mpaka unatokwa jasho kwenye nyusi na kutemea watu mate kama swira.   

Mwanafalsafa wa kifaransa René Descartes aliwahi kusema kwamba, ufahamu au elimu ya kweli inakuwa yenye fikra wazi na zinazojipambanua. Monsinyo Viganò anasema, tofauti kidogo kwenye ufahamu wa ukweli juu ya maisha na utume wa kikristo ni kwamba, sio fikra tu za kila mmoja anavyojisikia, bali kuna Mafundisho Tanzu yaliyo wazi na yanayojipambanua. Mfumo huu ndio unaoliwezesha Kanisa, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kujenga umoja wa jumuiya ya waamini, ndani ya upendo na ukarimu, kwa pamoja wakijikita katika wongofu wa ndani, mabadiliko ya dhati, toba na msamaha.

Ufahamu na ukweli wa maisha ya kikristo unafumbatwa katika maisha ya jumuiya, maisha ya mahusiano mazuri yanayozaliwa, yanayojitambua na yanayokua na kukomaa ndani ya Kanisa yakipenya na kuutakatifuza ulimwengu kwa harufu nzuri ya manukato ya utakatifu. Ni kwa namna hii, upyaisho wa taalimungu, mafundisho, utume na maisha yote ya wanakanisa yanaweza kuutambua na kuuopokea Uso wa Huruma ya Mungu unaojifunua kwa mwanadamu kama ndugu, kama jirani mwema, na kama rafiki. 

Kwa sababu hii, siku zote Kanisa lipo katika Hija ya maisha kuuchuchumilia utakatifu, hata kama kuna nyakati kunakuwepo na makosa ya hapa na pale, yanayosababishwa na udhaifu wa mwanadamu. Utakatifu wa maisha ya kikristo hauko kwenye kiburi cha kujiona waaamini wasio na doa wala mapungufu yeyote, bali ni utakatifu unaoona fahari katika kubadilika, kujutia dhambi, kudhamiria wongofu wa ndani na kufanya toba ya kweli.

Monsinyo Viganò anasema kwamba, inawezekana kitabu hiki kikawa utafiti wa mwisho wa Askofu Marchetto kuzingatia umri wake, kwani utafiti unahitaji nguvu za kutosha ili kutoa majibu yenye kufaa na kuboresha. Askofu mkuu Marchetto alizaliwa huko Vicenza Italia mnamo tarehe 28 Agosti 1940, akapata Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Juni 1964. alipata Daraja takatifu ya Uaskofu mnamo tarehe 1 Novemba 1985, na kufanya utume kwenye Balozi za Vatican zilizo katika nchi za Madagascar, Tanzania, Mauritius na Belarus. Mnamo tarehe 6 Novemba 2001 aliteuliwa kuwa Katibu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya wakimbizi, na mnamo tarehe 28 Agosto 2010 alistaafu akiwa na miaka 40. 

Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

27/10/2017 10:53