2017-10-25 16:13:00

Kard.Stella:Zingatia uhalisia, maana utume wa padre usiwe wa kindumila kuwili!


Utume wa padre usiwe ni wa “kindumila kuwili” kiasi cha kutenganisha shughuli za kichungaji na uwajibikaji katika mali. Uchungaji na utunzaji mali ni kazi ambazo zinao utofauti fulani lakini zote zinahusika ndani ya utume mmoja ambao ni Ukarimu wa kichungaji. Kwa ufupi, kila anachofanya padre na maisha yake yote ni uchungaji, kwa sababu yote yanawahusu wanadamu. Kundi alilokabidhiwa kulilinda na kulilisha, pamoja na familia yake, ndugu, jamaa na marafiki wanahusika kwa kiasi kikubwa katika utume na maisha ya padre. Maneno mazito na ya kina kabisa kuhusu maisha na utume wa padre, yamesisitizwa na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, akitoa hotuba kwa mapadri wawakilishi wa Italia, tarehe 24 Oktoba 2017, huko mjini Assizi, katika kumbukumbu ya miaka mia moja tangu kuanzishwa Mshikamano wa Umoja wa Mapadri wa Italia, 

Katika hotuba yake, Kardinali Stella amewaalika mapadri, katika utume wao, wazingatie uhalisia wa mambo, maisha ya waamini, changamoto na mtazamo wa Kanisa katika kipindi hiki. Kati ya mambo makuu ya kutilia maanani, ni pamoja na Mabadiliko ya taratibu za kuendesha Mashauri ya ndoa kanisani, Huruma ya Mungu, kashfa zinazolisongasonga kanisa, na umisionari wa kujitoa mzima mzima bila kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, amesisitiza Kardinali Stella.

Mabadiliko ya baadhi ya taratibu za kuendesha Mashauri ya ndoa kanisani, ambayo Baba Mtakatifu Francisko aliyatoa mwaka 2015 kwa Barua Binafsi, Motu proprio, Mitis Iudex Dominus Iesus, yaani Bwana Yesu Hakimu mwenye Haki, yanalenga hasa katika kushughulikia mashauri ya ndoa kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi, ili kuepuka waamini wahitaji, wasibaki na sintofahamu kwa muda mrefu juu ya mashauri yao, huku wakihangaika na maumivu makali ya maisha yao ya ukristo, bila kujua muafaka au kupata faraja walau ya ukweli juu ya mashauri ya ndoa zao.

Ni wazi kwamba, kuzingatia mabadiliko ya taratibu hizo kiutendaji ni suala linalowalenga kwanza kabisa wahudumu mbali mbali katika Mahakama za Kanisa, lakini yanawalenga pia kwa uzito mkubwa tu, maparoko na mapadri katika ujumla wao. Taratibu hizo, hata kama ni taratibu za kisheria na zinazohitaji umakini wa kitaalamu katika kuhusika nazo, ni taratibu ambazo ni za kichungaji zaidi. Mabadiliko ya uendeshaji wa mashauri ya ndoa yamezingatia sana utume na mahitaji ya waamini walioonekana kana kwamba wanasahaulika pembezoni mwa utume na maisha ya Kanisa. Hii ilitokana na mtazamo kwamba mashauri ya ndoa yalikuwa yanachukua muda mrefu, pengine kwa gharama kubwa, na walioweza kutatuliwa mashauri yao walikuwa ni wachache, kana kwamba wanapendelewa au kubahatika tu. 

Mahakama nyingi za kanisa zilikuwa kama nchi ya kufikirika tu isiyofikika kiuhalisia, na hivyo zilionekana kana kwamba ni Mabangaloo yenye kuta ndefu zisizoweza kurukwa na kuwaacha waamini wengi wakiimba wimbo wa sungura “sizitaki mbichi hizi”, wakati wanatafunwa na madonda yenye maumivu makali ndani.Kardinali Stella anasisitiza kwamba, kati ya wahudumu wa mashauri ya ndoa, ni pamoja na maparoko, ambao utume wao wa kwanza katika hili, ni kuwapokea na kuwasikiliza wanandoa ambao kwa namna moja ama nyingine, wamefikia kwenye utengano wa mahusiano yao, maumivu makali ya wanafamilia husika, pengine hata talaka kutoka serikalini, na hata kujikuta tayari wakiwa na wenza wengine. 

Mafundisho tanzu juu ya ndoa moja isiyovunjika kamwe, yanabaki kusimamiwa na Kanisa hata sasa, kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko. Hivyo Kanisa halitengui ndoa, isipokuwa, kama kulikuwapo na sababu za awali ambazo zimegundulika kuwa ndoa hiyo ilikuwa batili tangu awali, basi shauri hilo linaweza kutazamwa na kuwasaidia wahusika kufunguliwa vifungo kadiri ya taratibu za sheria na kuwawezesha kuishi vema maisha ya kikristo.

Utume wa kwanza wa paroko sio wa kutafuta sababu za kutangaza ndoa kuwa ni batili, bali ni kuwasikiliza na kuwasaidia kama kuna uwezekano wakarekebisha tofauti zao na kuendelea kusaidiana kuuchuchumilia utakatifu, basi na wafanye hivyo kwa maongozi ya mapadre, wachungaji wao. Na kwa wale ambao ndoa zao, hazina misingi ya ndoa batili kadiri ya taratibu za sheria za Kanisa, wasaidiwe na maparoko wao kuendelea kuwa waaminifu katika hija ya maisha ya ukristo, hata kama wanaishi kinyume cha taratibu fulani kikanisa, mapadre wawasaidie kujikwamua katika hali zao, wakiwasindikiza na kuwachukulia kwa upole, wao mapdre, wakiwa haswa wawakilishi wa sura ya Huruma ya Mungu, inayowatafuta watoto wake ili wote wapate kuokoka.

Suala lingine muhimu analosisitiza Kardinali Stella ni utunzaji na matumizi ya mali. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akiimba sana wimbo huu kwa mapadri, wawe makini na mali kwani pamoja na uhitaji wa fedha na vitu vingine katika huduma za Kanisa, mali inaweza kuwafanya wakawa kweli mashuhuda wa Injili au ikawaingiza katika kashfa kubwa za kukosa uaminifu na anasa. Ili kuwa na mahusiano mazuri na mazingira ya kiuchumi na mali, padre anapaswa kupalilia sana maisha yake ya kiroho, na kuwa makini sana asianguke katika mtego wa dhambi ya kuabudu fedha na mali. 

Padre ajihusishe na mali kama baba mwema na mwaminifu ndani ya familia. Baba mwema na mwaminfu huwa na busara na kiasi, akiwaandalia wanae maisha bora kwa siku zao za usoni. Hivyo padre kama baba mwema na mwaminifu, asiwe na ndoto za mchana zenye nadharia nyingi, wala asiwe na ujanja ujanja unaohatarisha mali za kundi au taasisi aliyokabidhiwa, bali awe na mipango madhubuti na inayotekelezeka katika uhalisia wa maisha. Mipango na utendaji wenye kuheshimu watu na wenye kuzaa matunda yanayodumu na kuwa faida kwa kundi la wana wa Mungu.

Mapadri wanapaswa kuzingatia, mbali ya miradi, sadaka na zaka, wazingatie pia uhalali na uaminifu wa maadhimisho ya Misa Takatifu kadiri ya Nia za Misa wanazopatiwa na kadiri ya taratibu za sheria, ikizingatiwa pia taratibu za jimbo husika au Baraza la Maaskofu. Mapadri wakumbuke pia huduma yao ya Ukarimu kwa wahitaji. Utunzaji na matumizi mazuri ya fedha na mali ya Kanisa uwe ushuhuda mzuri hata kwa waamini Walei namna ya kuhusika na mali, kwa sababu fedha, anasa na majivuno, ni ngazi tatu zinazowaangusha wanadamu wote kwenye dhambi. Padre akumbuke siku zote kwamba, waamini hawatamsamehe kwa urahisi, iwapo atajishikamanisha sana na fedha na mali, ametahadharisha Kardinali Stella. Kila jambo na kila huduma, itendeke katika roho ya kimisionari na uchungaji unaojikita katika wokovu wa roho za watu, ikiwa ni pamoja na wokovu wa roho ya padre mwenyewe.


Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.