2017-10-21 09:51:00

Ufunguzi wa mwaka mpya wa masomo 2017/18 wa Chuo Kikuu Urbaniana


Tarehe 17 Oktoba 2017 ilikuwa siku ya kipekee katika jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana ambapo mwaka mpya wa masomo 2017-2018 ulifunguliwa rasmi. Ni mwaka wa 390 wa masomo tangu kuanzishwa kwa chuo hicho. Katika ufunguzi huo ulitanguliwa na  Misa Takatifu ambayo imeongozwa na  Kardinali Fernando Filoni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Uinjilishaji, wakiwepo maprofesa  na wanafunzi wote wa Jumuiya nzima ya Chuo.

Katika  mahubiri ya Kardinali Filoni  amewataka wanafunzi kukazana na kutia bidii katika masomo na tafiti mbalilimbali kwa makini ili kujiandaa kikamilifu kumtumikia Mungu na watu wake, pia  walimu wamepongezwa kwa kazi nzuri ya kuendeleza madhumuni ya chuo hicho kikongwe cha kuinjilisha mataifa kwa maana ya  masomo na tafiti nyingi zinazofanywa na chuo hiki ni kwaajili ya kumtangaza Kristu kwa mataifa yote.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kardinali Filoni halikadhalika amempongeza Gombera wa chuo  aliyemaliza muda wake Padre Alberto Trevisol Mmisionari wa Shirika la Wakonsolata (IMC) kwa kazi nzuri na majitoleo yake  kukitumikia chuo kwa weledi na kujituma katika kipindi cha miaka sita. Sambamba na pengezi, Kardinali amemkaribisha na kumtia moyo gombera mpya wa Chuo cha Kipapa cha Urubaniana, Padre Leonardo Siloe wa Shirika la ndugu wadogo Wakapuchini (O.F.M) ambapo amemtakia utume mwema katika jumuiya ya Chuo Kikuu Urbaniana.

Akitoa msisitizo kwa wanachuo, Kardinali Filoni amewataka wanachuo wote kuzingatia ubora na hadhi ya chuo kama ilivyo desturi. Ametoa wito kwa wanafunzi kuutumia vyema muda wao na maprofesa ili waweze kunufaika na taaluma inayopatikana katika chuo hicho. Aidha kwa wanajumuiya nzia ya chuo amewaalika kutumia vema fursa ya uwepo wa wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali duniani ili kujinufaisha na utajiri wa tamaduni za mataifa mengine.

http://www.urbaniana.edu/Urbaniana/Default.aspx 

Chuo Kikuu cha Urbaniana ni taasisi ya kitaaluma ambayo ni sehemu ya shirika la kipapa kwa Uinjilishaji. Katika Chuo hiki, kazi za utafiti na ufundishaji hufanyika ndani ya mfumo wa huduma ya elimu takatifu inayoongozwa na Kanisa Katoliki.

Na Frt. Tito Kimario (IMC)








All the contents on this site are copyrighted ©.