2017-10-20 09:37:00

Tafadhali msichanganye mambo! Kodi ilipwe na Mungu atukuzwe!


Ndugu mpendwa, katika Injili ya leo – tunamwona Yesu akituachia msemo ambao umeacha  alama katika historia na katika maisha ya  mwanadamu - mpe Kaisari yaliyo yake Kaisari na Mungu yaliyo yake Mungu. Siyo tena au Kaisari au Mungu ila Kaisari na Mungu, kila mmoja kadiri ya hadhi yake. Ni mwanzo wa utengano kati ya dini na siasa.  Wayahudi walielewa ujenzi wa ufalme wa Mungu utakaojengwa kwa ujio wa Masiha – Mungu akiwa ndiye mtawala. Haya maneno ya Kristo yaonesha uwezekano wa uwepo wa ufalme katika ulimwengu lakini si wa ulimwengu huu, ila unaokuwepo kwa kiwango tofauti na kwa hivyo waweza kuendana na utawala wo wote, ikiwa ni wa kiroho au wa kidunia. Hapa twaona falme mbili lakini tofauti za Mungu katika dunia: utawala wa kiroho ambao ni utawala wa Mungu unaoongozwa moja kwa moja na Kristo, na utawala wa kidunia na kisiasa unaoongozwa si moja kwa moja na Mungu, lakini uliowekwa mikononi mwa mwanadamu huru.

Ieleweke wazi kuwa Kaisari na Mungu hawawekwi katika ngazi moja, kwa sababu Kaisari anamtegemea Mungu na anajibu kwake.  Hivyo mpe Kaisari yaliyo yake Kaisari ina maana kuwa – mpe Kaisari ambacho Mungu mwenyewe kamjalia Kaisari. Mungu ni mkuu wa vyote, hata Kaisari mwenyewe. Hatujagawanywa na falme mbili, hatutumikii/hatujagawanywa katika falme mbili, hatulazimishwi kutumikia mabwana wawili. Na lengo la Yesu halikuwa hilo katika jibu lake. Shida ni kwamba swali aliloulizwa lilikuwa la mtego. Yesu aliweka jibu lake katika fumbo ili waliomtega wasipate jibu moja kwa moja. Na kwa namna hii aliwachanganya waliomwuliza swali na hata sisi leo tusomao Neno hili. Ukidhani kuwa Yesu aliunga mkono falme mbili, ieleweke pia kuwa hata wale Mafarisayo waliomsikia akitoa jibu hawakumwelewa hivyo. Katika hukumu dhidi ya Yesu, moja ya shtaka lililowekwa mezani ni kwamba Yesu alikataza watu wasilipe kodi – Lk. 23:2.

Mkristo yuko huru kutii mamlaka ya kidunia, lakini pia yuko huru kuukataa utawala kama unaenda kinyume na Mungu na amri zake.  Hakuna anayelazimishwa kutii amri zisizo halali kwa mfano utawala wa kidikteta. Mara kadhaa unapotekea mgongano hasa wa kimaslahi kisiasa kati ya serikali na dini – wengi hasa wanasiasa wamesikika wakitumia maneno haya ya Injili ya leo. Lengo likiwa kunyamazisha viongozi wa dini ili wasikemee maovu ya wanasiasa au utawala mbovu. Huku ni kutokuelewa kabisa maana ya fundisho hili la Yesu. Ieleweke vizuri kuwa kabla ya kumtiii mtu, hatuna budi kumtii Mungu kwanza na dhamiri zetu. Huwezi kutoa roho yako, ambayo ni mali ya Mungu, kwa Kaisari. Na sote tukielewa hivi basi hakika somo la Injili la leo litatupa sote changamoto ya kutimiza nyajibu zetu vizuri zaidi kidini na kisiasa.

Mtume Paulo ni wa kwanza kutoa mwongozo wa kiutendaji kwa fundisho hili la Kristo – Rom. 13: 1…kila mtu awatii wakuu wa seikali. Kwa maana hakuna mamlaka yasiyotoka kwa Mungu, na kila yaliyoko yamewekwa na Mungu.  Kulipa kodi ni wajibu na si tu jukumu la wakristo bali kwa ye yote aliye raia mwema, ni wajibu wa kihaki na hivyo wajibu wa kidhamiri pia. Wajibu wa mamlaka ni kuongoza watu wake vizuri ili waweze kutimiza vizuri wajibu wao.  Kukwepa kodi ni dhambi kama vile ilivyo dhambi ya wizi – tunaona pia katika KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI.  Ni wizi na ni sawa na kujiibia mwenyewe.  Lakini hii itaenda tu vizuri kama mamlaka nayo inasimamia vizuri mapato ya kodi kwa manufaa ya watu wake.

Ushiriki wa wakristo katika ujenzi wa mamlaka iliyo ya haki na amani wahimiza pia ulipaji wa kodi. Hii ndiyo namna ya ushiriki wa wakristo katika ujenzi wa mamlaka hapa duniani.  Ulipaji wa kodi husaidia kudumisha thamani mbalimbali kama familia, kulinda maisha, mshikamano na maskini na kujenga amani. Huu ndiyo ushiriki wa wakristo katika maisha ya siasa ili kuondoa kutokulewana kunakoweza kuwepo na kujenga utu, kujenga mahusiano mema na maendeleo ya mamlaka husika. Uelewa huu utusaidie kujua hitaji letu la kulipa kodi na maana pana ya jibu la Yesu katika Injili ya leo. Kazi kwetu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. 








All the contents on this site are copyrighted ©.