2017-10-20 16:45:00

Papa ametuma salama za rambi rambi kufuatia kifo cha Daphne C.Galizia


Baba Mtakatifu Francisko ametuma telegram kwa kufuatia kifo cha kutisha  cha mwandishi wa Habari wa Malta Daphne Caruana Galizia  ujumbe  uliotiwa Saini na Kardinali Pietro Parolin Katibu wa Vatican. Telegram hiyo imeelekezwa kwa Askofu Mkuu Charles J. Scicluna wa Jimbo Kuu la Malta. Baba Mtakatifu anaonesha ukaribu wake kiroho kwa familia yake na watu wote wa Malta katika msiba huo mkubwa.

Ikumbukwe huyu ni Mwandishi maarufu wa habari za uchunguzi katika visiwa vya Malta aliyeuwawa tarehe 16 Oktoba 2017 wakati gari alilokuwa akiliendesha kulipuliwa na bomu visiwani humo. Daphne Caruana Galizia ambaye alikuwa mwandishi maarufu nchini humo, alikuwa akiitumia blogu yake kuandika taarifa zinazohusu kesi za madai ya rushwa zikiwemo za wanasiasa visiwani humo.

 Aidha, wakati wa uhai wake, Dphine alikuwa akimshutumu waziri mkuu wa visiwa hivyo, Joseph Muscat, na mkewe kutumia akaunti za benki za siri ili kuficha malipo kutoka kwa familia ya utawala wa Azerbaijan suala ambalo waziri mkuu na familia yake wamelikana. Hata hivyo, kwa upande wake waziri mkuu wa visiwa hivyo, Muscat amelaani mauaji hayo ambayo ameyaita ni ya kinyama, hivyo na kuahidi kuhakikisha wanakamatwa wote waliotekeleza mauaji hayo.

Sr Angela Rwezaula 
idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.