2017-10-20 08:15:00

Jamani! Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu apewe haki yake!


Leo tunaadhimisha Jumapili ya 29 ya Mwaka A wa Kanisa. Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Kimisionari Duniani kwa Mwaka 2017 inayoongozwa na kauli mbiu “Utume ni kiini cha imani ya Kikristo”. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa utume katika maisha ya Kanisa kama nguvu iletwayo na Injili ya Kristo Yesu, aliye njia, ukweli na uzima. Utume wa Kanisa uwawezeshe waamini kuambatana na Yesu katika njia ya toba na wongofu wa ndani. Kila mmoja wetu anahamasishwa na Mama Kanisa kuwa mmisionari katika mazingira yake kwa njia ya sala pamoja na kusaidia kuenzi kazi za kimisionari sehemu mbali mbali za dunia.

Tafakari ya Neno la Mungu katika Jumapili hii, tunaichota kutoka katika jibu la Yesu kwa Maherode na Wanafunzi wa Mafarisayo akisema “Mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu”. Kwetu sisi leo jibu hili la Yesu linayazungumzia maisha yetu moja kwa moja. Maisha yaliyo na wajibu kwa Mungu na pia wajibu kwa jamii inayozunguka - uongozi wake, utawala wake na yote yanayohusisha ustawi wake. Hapa tunajiuliza: Ni yapi yaliyo ya Kaisari na ni yapi yaliyo ya Mungu? Je, nifanye nini katika mazingira ambayo watawala wa nchi au jamii niliyomo wananiagiza kuwatii au kutenda yanayopingana na imani yangu kwa Mungu? Na Je, ninawezaje kutekeleza “ya Kaisari” bila kuathiri “ya Mungu”? Kwa hakika tunahitaji msaada wa Mungu na neema yake ya pekee katika kuyang’amua hayo. Lakini Mungu ambaye daima hatuachi peke yetu, ameweka ndani yetu sauti yake kwa njia ya dhamiri tulizonazo. Dhamiri ambayo huwa kama taa inayomulika hatua zetu katika njia iliyo na giza. Basi tafakari hii ya leo itusaidie kuziangalia dhamiri zetu: kuzichunguza, kupima uhai wake na kutibu magonjwa yake endapo yapo ili daima zituongoze kuyafikia mema anayoyakusudia Mwenyezi Mungu katika maisha yetu.

Swali: Wanafunzi wa Mafarisayo na Maherode: Katika somo la injili makundi mawili ya watu wanamfata Yesu na kumuuliza swali la kumtega kama ni halali kumlipa Kaisari kodi au la. Makundi haya ni Wafarisayo na Maherode. Wafarisayo walikuwa ni kundi la wayahudi waliojitenga na wenzao na walikuwa na mtindo wa pekee wa maisha. Hawa walishika dini kwelikweli na walipenda kila mtu aone kuwa kweli wanashika dini. Waherode walikuwa kama chama cha siasa ambacho kiliundwa na watu waaminifu kwa utawala wa Kirumi.

Kwa kawaida makundi haya mawili yalikuwa ni mahasimu wakubwa. Hii ni kwa sababu ya kuwa na misimamo tofauti juu ya utawala wa kirumi. Tunaona pamoja na uhasimu wao, leo wanaungana ili kumuuliza Yesu swali la kumtega kwa lengo la kumwangamiza. Na hii ndiyo huwa kawaida: Maadui wanaweza kuungana kwa muda ili kutekeleza nia fulani yenye manufaa kwao na kisha kuikamilisha wanarudi katika hali zao. Nia yao mbaya inaonekana pia kwa sifa walizoanza kumpa Yesu wakimwita mtu wa ukweli na anayeongea ukweli bila kuogopa mtu. Hii ndiyo huitwa “kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa”.

Mtego wa Swali kwa Yesu: Swali walilouliza lilikuwa na mtengo mkubwa kwa Yesu kutokana na mazingira ya kisiasa waliyokuwa nayo wayahudi kwa wakati huo. Kama koloni la dola ya kirumi, wayahudi walipaswa kutoa kodi nyingi kwa watawala. Wengi hawakupenda kabisa kodi hizi. Waliwachukia watawala na walimchukia sana yeyote ambaye alihimiza au kushauri kodi hizo zilipwe. Kumbe endapo Yesu angejibu ni halali kulipa kodi kwa Kaisari basi angeingia katika chuki kubwa sana na Wayahudi. Hali kadhalika, Wayahudi kama taifa teule la Mungu walijiona wako chini ya Mungu kama mtawala wao pekee. Kwake waliwajibika pia kutoa zaka na majitoleo mengine. Kitendo cha kulazimika kutoa kodi kwa Kaisari kilionekana pia kama uasi kwa Mungu wao. Jambo hili lilipingwa vikali sana na Mafarisayo.

Kumbe pia endapo Yesu angejibu ni halali kulipa kodi kwa Kaisari angeingia pia katika mgogoro mkubwa na kundi hili la Mafarisayo. Hali kadhalika, hata kama Yesu agejibu si halali kulipa kodi kwa Kaisari bado angeingia katika mgogoro na kundi la Maherode. Hawa kwa uaminifu wao kwa utawala wa kirumi walisisitiza kodi zilipwe na utawala wa kirumi upewe utii. Uhasama huu Yesu asingeingia na Maherode pekee bali pia na watawala wenyewe wa Kirumi. Jibu la Yesu: Ni nini alichofanya Yesu? Aliwaomba sarafu na kuwauliza picha na anuani iliyo katika sarafu ni ya nani? Wakajibu ya Kaisari. Hapo akawaambia “mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu”.

Kwa Jamii yetu: Somo hili la Injili linatualika tuuangalie wajibu tulionao kwa jamii tuliyomo sambaba na wajibu wetu kwa Mungu kulingana na imani yetu kwake. Ni dhahiri kuwa tunapoitazama jamii hatuwezi kuweka kando uongozi, utawala na mfumo wake; na hivi ni vitu ambavyo vimekuwa na changamoto nyingi sana katika maisha ya waamini na wanachi kwa ujumla. Kama ilivyokuwa kwa wayahudi, hata sisi leo tunayo manung’uniko juu ya watawala wetu katika masuala mbalimbali kama vile kodi,  ugumu wa maisha na mengineyo. Lakini pia yapo yasiyotoa picha nzuri kwa baadhi ya watawala wetu. Haya ni kama vile masuala ya utawala bora, chokochoko za uchaguzi na hata baadhi kung’ang’ania madaraka. Katika mazingira haya ni ipi nafasi ya muumini na ni nini anachotakiwa kufanya? 

Sanjari na yale tusiyoyapenda katika mifumo ya uongozi na utawala kwenye jamii zetu, yapo pia ambayo huenda tunayapenda na kuyafumbia macho katika mifumo hiyo lakini yanakwenda kinyume na matakwa ya Mungu na yanakwenda kinyume na matakwa ya imani yetu. Sura ya uongozi wa kujilimbikizia mali na kutafuta faida binafsi, utendaji usio na hofu ya Mungu na usioeneza ufalme wake na mengine kadha wa kadha ni baadhi ya mambo yanayo kwenda kinyume na matakwa ya Mungu na ya imani yetu kwake. Katika mazingira haya ni ipi nafasi ya muumini na ni nini anachotakiwa kufanya? 

Kwa wananchi?  - Kwa watawala?: Jibu la Yesu “Mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu” halilengi kukwepa kutoa jibu ili kuhofia kuchukiwa na waliomuuliza. badala yake linatoa kanuni au msimamo wa daima unaoongoza mahusiano kati ya mwanadamu, jamii (uongozi na utawala) pamoja na Mungu. Mwanadamu anawajibika kwa jamii na kwa watawala wake. Na wote hawa wawili, mwanadamu na watawala wanawajibika kwa Mungu. Ndiyo kusema baada ya mwanadamu kumlipa Kaisari yaliyo yake, wote wawili mwanadamu na Kaisari mwenyewe wanamlipa Mungu yaliyo ya Mungu. Kama tunavyoona katika somo la kwanza, watawala wa jamii ni vyombo vinavyomtumikia Mungu katika kuyakamilisha mapenzi yake kwa watu wake na hatimaye kumpa yeye Mungu utukufu. Hii ni nafasi ambayo watawala wa jamii zetu wanapaswa kuitambua na kuiakisi katika nafasi mbalimbali walizo nazo.

Jibu la Yesu halilengi kuegemea upande mmoja tu, ama kuwaridhisha wananchi ama kuwaridhisha watawala bali linawaweka wote katika mahali pamoja. Wote wampe Mungu haki iliyo yake na kwa kufanya hivyo wanayatimiza mapenzi yake na kumpa yeye utukufu.

Dhamiri zetu: Katika mang’amuzi yake ya kimungu, Mungu ametupatia dhamiri katika nafsi zetu. Hii ni sauti inayotuagiza tutende mema, tuache mabaya; inatisuta tukitenda mabaya na inatupongeza tukitenda mema; inatuongoza kuamua kwa hekima na kutenda kwa busara. Mwanadamu aliyeiunda dhamiri yake vema na anayeifuata hawezi kuhangaika katika kufikia maamuzi sahihi hata katika mazingira yanayokanganya. Ni muhimu kila wakati kuisikiliza dhamiri na kuifuata ili tusipotee. Uundaji wa dhamiri si tukio la mara moja, ni malezi mazima ya hatua kwa hatua ya mwanadamu tangu utoto. Malezi ambayo Kanisa, mafundisho yake na maadhimisho ya sakramenti zake yana nafasi ya pekee sana katika kuiunda, kuikomaza na kuiponya dhamiri inapopata majeraha.  Ni kwa dhamiri iliyo hai na safi tunaweza kusimama imara katika imani yetu dhidi ya mambo mbalimbali yanayotuvuta katika jamii zetu na kuwa changamoto kwa imani tuliyonayo kwa Mungu wetu. Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima, atuombee na kutusaidia daima.

Na Padre William Bahitwa.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.