2017-10-20 10:02:00

Askofu Castory Msemwa wa Jimbo Katoliki Tunduru- Masasi afariki dunia


Jimbo Katoliki Tunduru Masasi nchini Tanzania linasikitika kumpoteza mpendwa wao Baba Askofu  Castory Msemwa aliyefariki tarehe 19 Oktoba 2017, saa 7 mchana nchini Oman. Kwa mujibu wa Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki Tunduru Masasi, Padri Jordan Liviga, anasema, Askofu Msemwa amefariki dunia akiwa mjini Muscat (Oman), wakati wa safari ya kwenda nchini India kupata matibabu ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Marehemu Msemwa amekuwa na tatizo la kiafya kwa kipindi cha miaka miwili, na amekuwa akipata tiba mbalimbali na kuendelea na utume kama kawaida. Aliondoka nchini siku ya Jumatano 18 Oktoba kuelekea nchini India kwa matibabu kabla hajafariki dunia. Padri Liviga amebainisha kuwa utaratibu wa kuuleta nchini mwili wa marehemu Askofu Castory Msemwa siku ya Jumapili Dar es Salaam unafanyika. Na hivyo taarifa zaidi za utaratibu wa mazishi zitatolewa baadaye.

Askofu Castory Paul Msemwa amezaliwa mwaka 1955 katika kijiji cha Kitulira, Parokia ya Matola Jimbo Katoliki Njombe. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Motola, baadaye Sekondari katika Seminari Kuu ya Peramiho ambapo pia alisomea Falsafa na Teolojia kati ya mwaka 1981 na 1987. Alipata daraja ya Upadri tarehe 7 Juni 1987. Amekuwa Paroko Msaidizi na  kiongozi wa vijana jimboni Njombe. Alikuwa pia mwalimu na amesomea katika Chuo cha Kipapa cha kitasaufi cha  Teresiaunum Roma na kuhitimu mwaka 1996. Alipata Daraja la Uaskofu tarehe 30 Januari 2005  na  kusimikwa rasmi katika Jimbo Katoliki Tunduru Masasi tarehe 25 Agosti 2005.

Mwenyezi Mungu ampumzishe pema mbinguni, Amina.

Na Bernard James, DSM.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.