2017-10-19 16:30:00

Waathirika wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni watu!


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti zaidi katika mchakato wa majiundo makini ya binadamu, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu; kwa kuwatambua na kuwasaidia waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili waweze kuandika tena kurasa za maisha yao kwa matumaini mapya pasi na kutafuta njia za mkato katika maisha. Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Monsinyo Janusz S. Urbanczyk, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss wakati alipokuwa anachangia mada kuhusu udhibiti wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya wakati wa Kikao cha Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa Haramu za Kulevya.

Monsinyo Janusz S. Urbanczyk katika kikao hiki cha sitini amesikitika kusema kwamba, matumizi haramu ya dawa za za kulevya ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu na kwamba, familia zinapaswa kuwezeshwa zaidi ili kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya tangu awali. Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 19- 21 Aprili 2016 Umoja wa Mataifa uliendesha Mkutano kuhusu janga la dawa za kulevya duniani na hatua mbali mbali ambazo zimekwisha kutekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa sanjari na changamoto kubwa zilizoko mbele yao.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajizatiti zaidi katika maboresho ya afya ya binadamu, kwani afya bora ni haki msingi ya binadamu inayomwezesha mtu kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara; haki hii inapaswa kuendelezwa katika familia na jamii katika ujumla wake. Matumzi haramu ya dawa za kulevya ni janga kubwa linalomwandama mwanadamu, kiasi hata cha kuathiri mfumo wa uchumi, ustawi na maendeleo ya binadamu. Kutokana na madhara yake makubwa, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta mbinu muafaka ya kupambana na vikali na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Ujumbe wa Vatican kwa namna ya pekee, unaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mambo yafuatayo kama sehemu ya mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na utafiti pamoja na unchambuzi yakinifu unaopelekea watu kujitumbukiza katika biashara, usambazaji na matumizi ya dawa haramu za kulevya. Kimsingi mara nyingi mambo haya yanasababishwa na msongo wa mawazo kutoka katika familia, jamii pamoja na ushabiki unaofanywa na watumiaji wa dawa haramu za kulevya kwani mara nyingi ni watu wanaojionesha kuwa na umaarufu sana kutokana na fedha na mali wanazomiliki hata kama si kihalali.

Baadhi ya watu wanadhani kwamba, huu ndio mtindo wa maisha, yaani ukitaka kuwa maarufu katika jamii lazima “ubwie unga” lakini matokeo yake ni vijana wengi kujikuta wakiwa mateja wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya! Makombora ya mapambano ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya hayana budi kuelekezwa zaidi kwenye elimu na majiundo makini yanayopania kumpatia mwanadamu maendeleo endelevu: kiroho na kimwili; kwa kutumia vyema utashi na akili ili kupambana vyema na mazingira, ili kuweza kuifanya dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kama hakuna elimu makini, watu wengi wanaweza kutumbukizwa kwa urahisi sana katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa lengo la kujipatia mali na utajiri wa haraka haraka pamoja na umaarufu katika jamii hata kama utu na heshima yao vinawekwa rehani kama binadamu!

Monsinyoìo Urbanczyk anakumbusha kwamba, makosa ya jinai yanayofanywa na wafanyabiashara, wasambazaji na watumiaji haramu wa dawa za kulevya yanapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia haki, utu na heshima ya binadamu. Vatican inapinga adhabu ya kifo kama njia ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya kwani adhabu hii inakwenda kinyume kabisa cha haki msingi, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haki inapaswa kumwilishwa katika matumaini yatakayomwezesha mtuhumiwa kupata nafasi ya kuweza kuandika tena historia ya maisha yake.

Monsinyo Urbanczyk anakaza kwa kusema, kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati utakaowawezesha waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya kupatiwa matibabu ili hatimaye, kuweza kuingizwa tena katika maisha ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, kila mtu aliyeathirika na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya nyuma yake anafunikwa na historia ambayo inapaswa kusikilizwa kwa makini, kufahamika, kupendwa na kupewa nafasi ya kuweza kupata tiba ili kutakaswa.

Waathirika wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni watu wenye utu na heshima yao na kamwe hawawezi kugeuzwa kuwa kama vichokoo au watu wasiokuwa na thamani tena katika jamii! Vatican inakaza kwamba, familia ni mahali muafaka pa kupambana na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Hapa ni mahali ambapo familia zikijengewa uwezo zinaweza kuwa ni msaada mkubwa wa kuzuia pamoja na kuponya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.