Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Papa Francisko: Waamini jengeni utamaduni wa kutafakari Fumbo la Kifo

Papa Francisko anawaalika waamini kutafakari Fumbo la Kifo ili kujenga na kuimarisha matumaini ya Kikristo juu ya Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele.

18/10/2017 15:16

Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na kwamba hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano, tarehe 18 Oktoba 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amefafanua kwamba, utamaduni wa watu wa kale, uliliangalia fumbo la kifo usoni pasi na kigugumizi! Mzaburi katika Agano la Kale anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima”. Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana.

Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na tabia ya kutaka kulipiza kisasi. Kifo kina wahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao!

Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na  kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu anataka kuganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu!

Katika Maandiko Matakatifu, kuna sehemu zinazoonesha wazazi wakiwaombea watoto wao wagonjwa wapate kupona! Hii ni hali inayogusa undani wa maisha ya mtu, ndiyo maana hata Yesu aliposikia kwamba, binti yake Yairo alikuwa amekwisha kufa, akamwambia mkuu wa Sinagogi: “Usiogope, amini tu.” Hii ilikuwa ni changamoto kwa Mzee Yairo kuhakikisha kwamba, anaendelea kuwasha moto wa matumaini na kwamba, Yesu alipofika nyumbani kwake, akamfufua binti yake na kumpatia tena akiwa mzima! Yesu anawaelekeza waja wake katika njia hii ya imani.

Martha alikuwa analia na kumwombolezea ndugu yake Lazaro na hapo Yesu mwenyewe anafafanua kuhusu Mafundisho tanzu juu ya Fumbo la Kifo kwamba, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi”. Yesu akamuuliza Martha, Je, unayasadiki haya? Baba Mtakatifu Francisko anasema hili ndilo swali la msingi ambalo anapenda kulirudia tena na tena, pale ambapo kifo kinararua maisha na mahusiano ya dhati! Maisha ya mwanadamu yanachezea katika uwanja huu, yani kati ya imani na wasi wasi juu ya kifo.

Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kumi” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka”. Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

18/10/2017 15:16