2017-10-18 15:59:00

Dini zihamasishe amani kwa kujenga haki, udugu na kutunza mazingira


Watu sehemu mbali mbali za dunia wamechoshwa sana na vita, kinzani na migogoro inayoendelea kupandikiza mbegu ya kifo, chuki na uhasama kati ya watu. Ikumbukwe kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo pia inamwajibisha mwanadamu. Watu wote wenye mapenzi mema na hasa wale walioko kwenye nafasi za uongozi wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa Injili ya amani, kwa akili, nyoyo na mikono yao! Hii inatokana na ukweli kwamba, amani ni Sanaa inayopaswa kutengenezwa na kudumishwa na wote!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 18 Oktoba 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki mkutano wa “Dini kwa ajili ya amani” ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Dini zina utajiri na amana kubwa ya maisha, tasaufi na kanuni maadili, tunu msingi zinazoweza kusaidia katika mchakato wa ujenzi na udumishaji wa Injili ya amani duniani. Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ghasia na mauaji kwa kisingizio cha jina la Mwenyezi Mungu wanafanya kufuru kwa Mungu ambaye ni amani na chemchemi ya amani kwa watu wake.

Dini katika asili yake, zinatakiwa kuwa ni vyombo vinavyohamasisha amani kwa njia ya haki, udugu, utunzaji wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kukataa katu katu kutumia silaha kama suluhu ya migogoro kati ya watu! Kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kukuza na kudumisha kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu baada ya kukamilisha yote, akaona kwamba, kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Viongozi wa dini wanayo dhamana na agano la kimaadili linalowataka kuheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu sanjari na kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua nafasi hii, kumshukuru Mungu ambaye, anaiwezesha dunia kuwa na mashuhuda wa ushirikiano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani dhidi ya vita, ghasia, ili kuendeleza mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na kuitunza dunia. Hii ndiyo njia ambayo viongozi wa dini wanapaswa kuifuta  kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu pamoja sala za watu wema sehemu mbali mbali za dunia. Kwa hakika, juhudi kama hizi zitaweza kuzaa matunda ya amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.