2017-10-16 08:52:00

Askofu Shao: Watanzania ungeni mkono juhudi za Rais Magufuli!


Askofu Agustino Ndeliakyama Shao, C.S,Sp., wa Jimbo Katoliki la Zanzibar amewataka Watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua anazochukua kurekebisha mambo muhimu na msingi kwa maendeleo, ustawi na mafao ya watanzania wengi, licha ya kuwepo kwa changamoto katika kipindi cha mpito. Askofu Shao amesema hayo tarehe 15 Oktoba, 2017 wakati akihubiri katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye  Kanisa la Mtakatifu Yosefu, Parokia ya Minaramiwili, Jimbo Katoliki Zanzibar. 

Rais Magufuli ameungana pia na waamini wengine kusali Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya XXVIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, ambamo mwaliko umekuwa ni kushiriki kikamilifu karamu ya Bwana Harusi, kwa kuwa na vazi la harusi, yaani neema ya utakaso waliyopewa wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo. Amekazia kwamba, maisha ya Kikristo yanasimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala si  kwa mazoea tu!

Akitoa mfano wa nchi ya Zimbabwe ambayo Rais wake Robert Mugabe aliamua kuchukua hatua za kupigania maslahi ya Wazimbabwe na sasa wananchi wa nchi hiyo wameanza kuzalisha bidhaa na kuziuza nje ya nchi, Askofu Shao amesema hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli kupambana na rushwa, kupigania rasilimali za Watanzania, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji, kukabiliana na wizi na ubadhilifu wa mali za umma na kubana matumizi, zinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote. “Hatutaweza kusema tunaimaliza rushwa wakati tunaendelea kuishi kwa kupata fedha ambazo hutujazifanyia kazi, ni lazima tuishi machungu ya kuimaliza rushwa, ni lazima tuishi machungu ya kuweka uadilifu katika utendaji wetu, tusipoishi machungu hayo tutaishi dunia mbili, dunia ya rushwa na dunia ya kujenga uchumi na uadilifu wa Watanzania, tukubali kujikatalia ili tuweze kupata mazuri tuliyotaka” amesema Askofu Shao.

Katika salamu zake baada ya kuhitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu, Rais Magufuli amemshukuru Askofu Shao kwa mahubiri yake na ameungana naye kuwahakikishia Watanzania kuwa, Serikali ya awamu ya tano inachukua hatua za kupambana na rushwa na kulinda rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha wananchi wenyewe. Rais Magufuli amesema hata Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye tarehe 14 Oktoba 2017 ametimiza miaka 18 tangu alipofariki dunia, alipiga vita rushwa na alipigania rasilimali za nchi, hivyo ametawaka Watanzania wote kuungana katika juhudi hizo. Rais Magufuli ambaye alikuwa ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru Watanzania wote kwa maombi na sala yao na amechangia Shilingi Milioni 1 kwa ajili kwaya ya Kanisa hilo na Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali haitafuta mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kuwa ni alama ya Uhuru na Utaifa wa nchi na kwamba, unatoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo, kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano. Hiki ni kielelezo makini cha maadili, uzalendo, ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 14 Oktoba, 2017 katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa Amaan uliopo Mjini Magharibi, Zanzibar.

Pamoja na kauli hiyo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendeleza mbio za mwenge wa uhuru na kuutetea Muungano kwa nguvu zote. “Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi yetu. Nimefarijika zaidi kusikia kuwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu jumla ya viwanda 148 vimezinduliwa, viwanda hivyo vimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 468.46 na vinatarajiwa kuzalishaji ajira 13, 370. Hii ndio sababu tumekuwa tukihimiza ujenzi wa viwanda na hizi ni baadhi ya faida za Mwenge” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuwa wazalendo, kuthamini utu na usawa wa binadamu na muhimu zaidi kujitathimini ni kwa kiasi gani wanajiepusha na vitendo vinavyoathiri ustawi wa nchi na watu wake kama vile wizi, rushwa, ubinafsi na kukosa uzalendo.

Ametolea mfano wa Mwl. Nyerere ambaye mwanzoni mwa uongozi wake alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania aliamua kupunguza mshahara wake na kukataa kuongeza mishahara ya wafanyakazi wengine Serikalini kwa maelezo kuwa hawezi kuongeza mishahara ya wachache wakati wananchi wengi ni maskini na hawapati huduma muhimu za afya, elimu na maji. “Ninaposema hivyo simaanishi kuwa mishahara isiongezwe. La hasha. Ninachosema ni kwamba, kabla ya kudai nyongeza ya mishahara ni lazima kwanza: kufahamu uwezo wa Serikali, lakini pia tutambue kuwa kuna Watanzania wenzetu wengi tu wanaohitaji kuboreshewa huduma za kijamii na kiuchumi. Hata hivyo baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na vyeti feki, Serikali imewapandisha vyeo na kuwarekebishia mishahara watumishi 59,967 ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 159.33 zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu na mishahara mipya itaanza kulipwa kuanzia mwaka huu. Na kwa upande wa Zanzibar kima cha chini cha mshahara kimeongezwa kutoka Shilingi 150,000/- hadi kufikia Shilingi 300,000/-”  Amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu vijana Rais Magufuli amewataka kuendelea kujielimisha katika Nyanja mbalimbali, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi. Aidha, Rais Magufuli amewapongeza na kuwakabidhi vyeti wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa walioongozwa na Amour Hamad Amour kwa kukimbiza mwenge huo kwa siku 195 katika mikoa yote 31 na Halmashauri 195, ambapo jumla ya miradi 1,512 yenye thamani ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.1 imepitiwa. Na pia ameahidi kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kusababisha dosari katika miradi 19 ambayo viongozi wa mwenge wamebaini. Sherehe hizo zimehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makama wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Idd, Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Zanzibar.

15 Oktoba, 2017.








All the contents on this site are copyrighted ©.