2017-10-14 14:54:00

Papa Francisko aipongeza Lebanon kwa kuonesha ukarimu kwa wahamiaji


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 13 Oktoba 2017 amekutana na kuzungumza na Bwana Saad Rafic Hariri, Waziri mkuu wa Lebanon, ambaye baadaye amebahatika kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa amembatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Mazungumzo haya yamefanyika katika hali ya amani na utulivu, iliyowawezesha viongozi hawa wawili kupembua masuala kadhaa ya Lebanon na hali ya kisiasa huko Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu Francisko na Waziri mkuu wa Lebanon wameridhishwa na uhusiano uliopo kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuonesha matumaini yao kwamba, wataendelea kuudumisha na kuimarisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Lebanon. Wameonesha matumaini yao kuhusu mchakato wa uimarishaji wa masuala ya kisiasa nchini Lebanon kwa ajili ya kujenga na kudumisha amani na umoja wa kitaifa.

Baba Mtakatifu ameipongeza Lebanon ambayo imekuwa ni msaada mkubwa kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao nchini humo. Wamekazia umuhimu wa waamini a dini ya Kiislam na Kikristo kushirikiana katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa kwa kuzingatia historia, utume na maisha yake, litaendelea kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi huko Mashariki ya kati, kama sehemu ya utambulisho wake huko Mashariki ya kati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.