Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji na ushuhuda wa imani

Papa Francisko anasema, madhabahu ni mahali pa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. - ANSA

14/10/2017 10:33

Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya  utimilifu na utakatifu wa maisha. Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya,  limepewa dhamana na madaraka ya kusimamia Madhabahu ya Kimataifa kadiri ya sheria za Kanisa; Kuhakikisha kwamba, maeneo haya muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, yanakuwa ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya: unaojikita katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Baraza lina wajibu wa kusaidia madhabahu ya Kanisa kuwa ni mahali pa mikutano ya kitaifa na kimataifa, ili kukuza na kudumisha ibada na hija kwenye maeneo matakatifu. Baraza lina dhamana ya kuwafunda wahudumu kwenye madhabahu haya, ili yaweze kutoa huduma msingi za kichungaji, kikanisa na maisha ya kiroho pamoja na kuendeleza sanaa na utamaduni wa maeneo haya, kama mifumo maalum ya uinjilishaji. Kimsingi hii ndiyo changamoto kubwa iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake binafsi ijulikanayo kama “Sanctuarium ecclesia” yaani “Madhabahu ndani ya Kanisa”.

Kwa kutambua changamoto hii katika maisha na utume wa Kanisa, hivi karibuni, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, aliongoza hija ya maisha ya kiroho kwa wahamiaji kutoka Ureno kwenda kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fàtima kama mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fàtima yaani: Francis, Yacinta na Lucia, kati yao, wawili yaani Francis na Yacinta, tarehe 13  Mei 2017, wametangazwa na Papa Francisko kuwa ni watakatifu katika kilele cha maadhimisho haya! Mchakato wa kutangaza mtumishi wa Mungu Lucia tayari umeanza. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, watoto hawa watatu wa Fàtima wataweza kuunganika tena katika utakatifu wa maisha katika utatu wao!

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, anafafanua kwamba, tukio hili la hija kwa wahamiaji kutoka Ureno, ilikuwa ni safari ya maisha ya kiroho, kurejea tena nyumbani, ili kuweza kujichotea neema na baraka yakuweza kusonga mbele na maisha ughaibuni. Si rahisi sana kuzoea maisha ya ugenini, yaani kuwa mbali na familia, mazingira na tamaduni ambazo mtu amezizoea katika maisha yake. Wahamiaji hawa kama walivyo wahamiaji wengine sehemu mbali mbali za dunia, walilazimika kuikimbia nchi ili kutafuta fursa za ajira na maisha bora zaidi. Hija hii imewawezesha kurejea tena katika historia na mapokeo ambayo yamewaunda na kuwafunda kama walivyo.

Ili kuweza kufikia lengo la maisha ya kiroho, kuna haja kwa mwamini kujisadaka, kuvumilia shida na mahangaiko ya maisha ili hatimaye, kuweza kukutana na jicho la Bikira Maria, Mama mpendelevu, ili kusali pamoja na kukimbilia katika ulinzi na tunza ya Mama wa Mungu na Kanisa. Jambo la msingi kwa waamini wanapofanya hija ya maisha ya kiroho ni kumwomba Bikira Maria awasaidie kujifunza kusali vyema, kama Kristo Yesu mwenyewe alivyowafundisha wafuasi wake, akawaonesha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayosimikwa katika sala kama sehemu ya maisha ya kila siku! Kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kutimiza mapenzi yake kadiri ya huruma na upendo kwa waja wake, tayari kuwafungulia vifungo vya dhambi, ili kupeta katika mchakato wa utimilifu na utakatifu wa maisha.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anakaza kusema, hija ya maisha ya kiroho, iwasaidie waamini kujifunza kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao, tayari kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wanaowazunguka. Huu ni mwaliko wa kufungua masikio ya mioyo ili kuisikiliza sauti ya Mungu inayozungumza na waja wake kutoka katika undani wa dhamiri nyofu. Ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha utamaduni wa ukimya, ili kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Madhabahuni hapa ni mahali pa toba na wongofu wa ndani; mahali pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani; ni mahali pa kukimbilia huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Hapa, waamini wamekumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya Wakristo, kumbe, daima wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Wao ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, kama sehemu ya Kanisa wanao wajibu na dhamana ya kuliombea Kanisa zima; kuwaombea watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali; watu wanaoogelea katika dimbwi la huzuni na machungu ya maisha; wagonjwa na wale wote walioko kufani; wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau watu wanaoteseka kutokana na athari za majanga asilia.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anafafanua kwamba, hizi zote ni dalili za umaskini unaomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Amewataka waamini kuwa thabiti katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake. Wajitahidi kukimbilia huruma na kuambata upendo wa Mungu katika maisha yao! Wajitahidi kukazia mambo katika maisha ya Kikristo yanayojikita katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha unaoshuhudiwa katika upendo kwa Mungu na jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

14/10/2017 10:33