2017-10-14 13:34:00

Kanisa lahitimisha Jubilei ya Miaka 100 ya B. Maria wa Fatima


Mama Kanisa tarehe 13 Oktoba 2017 amehitimisha rasmi maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima, yaani: Francis, Yacinta na Lucia. Askofu mkuu Antonio Augusto dos Santos Marto wa Jimbo kuu la Leiria-Fatima, Ureno anasema, katika kipindi cha mwaka mzima, waamini wametafakari kuhusu mwanga wa uzuri wa Mungu unaowaalika waamini kuambata imani katika matendo na kumwabudu Mungu katika maisha yao. Itakumbukwa kwamba, kilele cha maadhimisho haya kilizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko mwezi Mei, 2017 kwa kuwatangaza Francis na Yacinta Marto kuwa watakatifu. Hija ya Baba Mtakatifu wakati huo iliongozwa na kauli mbiu “hujaji wa matumaini na amani nchini Ureno”. Hii ilikuwa ni heshima kubwa kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaomiminika kila mwaka katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima.

Hii ni heshima kubwa kwa familia mpya ya Bikira Maria wa Fatima, ambayo kwa sasa imeenea sehemu mbali mbali za dunia, changamoto na mwaliko wa kumwilisha ujumbe wa Bikira Maria kwa watoto wa Fatima katika uhalisia wa maisha yao kwa nyakati hizi. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani; wao wenyewe wakiwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Bikira Maria ni nyota ya uinjilishaji mpya, mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kielelezo makini cha imani tendaji!

Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima ni kielelezo cha amani duniani, ushuhuda ambao ulitolewa na Mwenyeheri Paulo VI kunako tarehe 13 Mei 1967 alipowataka watu wa Mataifa kuwa wema na wenye hekima kwa kujikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliitaka familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia kujikita katika Injili ya haki, amani na maridhiano kwa kuondokana na utamaduni wa kifo na mapunduzi yasiyokuwa na mvuto wala mashiko; yanayosababisha majanga katika maisha ya watu wasiokuwa na hatia badala yake, wanapaswa kujizatiti katika sera na mikakati inayopania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kujikita katika upendo, mshikamano na udugu, ili kufikiri, kupanga na kudumisha amani duniani, badala ya kuwaza vita na maangamizi ya watu wengine.

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumilia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa! Bikira Maria anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu ili kuombea: haki, amani na maridhiano duniani! Hii ni changamoto endelevu hata kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo!

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unafumbatwa kwa kiasi kikubwa katika Injili, kiasi kwamba, Fatima inakuwa ni shule ya imani na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, na Bikira Maria ndiye Mwalimu wake mkuu! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani kwa Kristo Yesu na kamwe wasikatishwe tamaa na Vita, kinzani na majanga katika maisha ya watu; tawala za kifashisti na kikomunisti; tawala ambazo zimedhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kiasi hata cha kutaka kumng’oa Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Kilio cha waamini kilikuwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu asimame mwenyewe na kujitetea!

Waamini wanaalikwa kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili; ili kujiachilia wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kujazwa na upendo wake usiokuwa na kifani, upendo unaowaambata wote pasi na ubaguzi. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, imani inapaswa kukua na kukomaa na matunda yake ni toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.