Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Miaka 400 ya Mt. Vincent wa Paulo: shuhuda wa utandawazi wa upendo!

M. Vincent wa Paulo: chachu ya utandawazi wa upendo na mshikamano wa kimataifa. - EPA

13/10/2017 14:39

Mtakatifu Vincenti wa Paulo katika maisha na utume wake alitaka kutafakari wema na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwani kwake maskini walikuwa kama wawakilishi wa Yesu na sehemu muhimu sana ya Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa. Alitambua kwamba, maskini ni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa hata wao pia wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa kwa kulisaidia kumwongokea Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Vincent wa Paulo alipenda kushirikiana kwa karibu sana na waamini walei ndiyo maana Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Upendo linataka kujizatiti zaidi katika mchakato wa kuwajengea uwezo wanawake kwa kuwaondolea umaskini na mahangaiko ya: kiroho, kimwili, kimaadili na kiutu, wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu alipozaliwa. Yaani kuanzia mwaka 1617 hadi mwaka 2017.

Mambo yote haya anasema Baba Mtakatifu Francisko ni sehemu ya utashi wa Mungu kwa mwanadamu, yaani ni upendo unaopaswa kumwilishwa katika maisha ya binadamu, ili kumletea maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Kipaumbele cha kwanza wawe ni wanawake pamoja na watoto wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia. Maisha yanayofumbatwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake, yanawasaidia waamini kutambua uhalisia wa maisha, utu na heshima ya binadamu; matatizo na changamoto anazokabiliana nazo: kijamii, kisiasa na kiuchumi na kumthamini kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Familia ya Mtakatifu Vincenti wa Paulo Kimataifa kuanzia tarehe 12 – 15 Oktoba, 2017 inaadhimisha Kongamano la Kimataifa, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, huduma ya upendo inavaliwa njuga na kwa kusimikwa katika utandawazi wa upendo na mshikamano. Haya yamesemwa hivi karibuni na Padre Tomaz Mavric, Mkuu wa Familia ya Mtakatifu Vincenti wa Paulo Kimataifa. Kilele cha maadhimisho haya ni Jumamosi, tarehe 14 Oktoba 2017 kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kongamano hili ambalo limewashirikisha wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, linaongozwa na kauli mbiu “Nilikuwa mgeni mkanikaribisha”. Zote hizi ni mbinu mkakati wa kuhakikisha kwamba, huduma ya upendo inavaliwa njuga na kuwa ni sehemu ya utambulisho wa utandawazi wa kimataifa, sanjari na utandawazi wa utamaduni na ule wa kijamii. Vijana wataweza kupata ujumbe makini kwa ajili yao kwa njia ya tamasha la sinema lijulikanalo kama “Vincentian Film Festival” ambayo ni mkusanyiko wa video mbali mbali zilizotengenezwa navijana wa kizazi kipya kama sehemu ya ushuhuda wa utandawazi wa upendo. Washindi watapewa tuzo huko Castel Gandolfo baada ya uamuzi utakaotolewa na jopo la majaji wa sinema wakiongozwa na Bwana Clarence Gilyard.

Lengo ni kujenga mtandao wa Familia ya Mtakatifu Vincenti wa Paulo Kimataifa, kwa ajili ya kuwasaidia maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum sehemu mbali mbali za dunia. Takwimu za Jumuiya ya Kimataifa zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya bilioni 1.2 hawana makazi ya kudumu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya hii inachangia si tu kwa kugaribisha changamoto hii ya kimataifa, bali kutoa jibu makini kwa watu wasiokuwa na makazi maalum. Hii ndiyo ndoto wanayotaka kuifanyia kazi na hatimaye, kuipatia sura kamili. Jumuiya hii inataka kuwa ni sauti ya wanyonge na watu wasiokuwa na makazi, ili waweze kusikilizwa kwa makini na wanasiasa katika ngazi mbali mbali: kitaifa na kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

13/10/2017 14:39