Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Ujumbe kwa Siku ya XXX ya Afya ya Macho Duniani Kwa Mwaka 2017

Siku ya Afya ya Macho Duniani kwa Mwaka 2017 inaongozwa na kauli mbiu " Afya ya macho kwa wote". - RV

12/10/2017 13:36

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 12 Oktoba 2017 inaadhimisha Siku ya XXX Afya ya Macho Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Afya ya macho kwa wote”, mwaliko na changamoto kwa watu wote kujibidisha kupima afya ya macho yao ili kuzuia upofu unaoweza kujitokeza. Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu katika maadhimisho haya ambayo yameandaliwa na Shirika la Afya Duniani, Muungano wa Mashirika ya Kimataifa Yanayojishughulisha na Huduma ya Macho kwa kushirikiana na Serikali mbali mbali duniani, anapenda kukazia umuhimu wa afya ya macho kama kielelezo cha maisha bora na kinyume chake, ni hali ambayo inaweza kuwatumbukiza watu katika mazingira ya umaskini, kiasi hata cha kuhatarisha Injili ya uhai.

Kardinali Turkson anasema, sehemu kubwa ya mambo yanayosababisha upofu yanaweza kuzuiwa au kupatiwa tiba muafaka. Inasikitisha kuona kwamba, sehemu kubwa ya magonjwa ya macho katika Nchi maskini zaidi duniani yanaendelea kusababisha upofu pamoja na vifo. Maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu yamewezesha wataalam wa afya ya macho kuzuia magonjwa ambayo yalikuwa yanasababisha upofu, ikiwa kama yatatibiwa mapema. Hata hivyo, umri wa watu kuishi duniani umeongezeka maradufu na matokeo yake, magonjwa yanayotokana na umri huu yanaendelea pia kuongezeka. Haya ni magonjwa ya: retina, upofu wa utotoni, makovu kwenye kioo cha jicho, upungufu wa upeo wa macho kuona pamoja na vikope.

Ili kuweza kujizatiti zaidi katika maboresho ya “Afya ya macho” anasema Kardinali Turkson, kuna haja ya Serikali na wadau mbali mbali kuhakikisha wanawaandaa wataalam wa afya ya macho katika ngazi mbali mbali. Wananchi wapate fursa ya kupata kinga na tiba kwa magonjwa ya macho! Wananchi wajizatiti katika mapambano dhidi ya athari ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta athari kwa ekolojia ya binadamu, lakini waathirika wakubwa ni wananchi wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani.

Mama Kanisa katika maisha na utume wake, amekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee vipofu. Kanisa wakati mwingine linatekeleza dhamana hii kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ili: kuzuia, kutibu na kutekebisha kasoro za afya ya macho. Kutokana na mwaliko uliotolewa na “Global Action Plan”, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu limeandaa kongamano la kimataifa litakalofanyika mwezi Novemba, hapa mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mapambano dhidi ya fursa sawa za afya kimataifa”. Huduma ya tiba ya afya ya macho inaingia moja kwa moja katika mtazamo huu.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinalindwa na kudumishwa, kwani hata maskini katika umaskini wao, wanaweza kupata huduma bora ya afya kama sehemu ya haki zao msingi. Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu anahitimisha kwa kusema, licha ya mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika tiba ya mwanadamu, lakini pia kunaendelea kuibuka magonjwa mapya yanayofumbatwa katika umaskini; uhamiaji na umri mkubwa. Watu wote wanahimizwa kujizatiti zaidi kwa kuwajibika katika mapambano dhidi upofu, kwa kujiaminisha mbele ya huruma ya Mungu na huduma makini ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

12/10/2017 13:36