2017-10-12 14:20:00

Siku ya Afya ya Macho Duniani kwa mwaka 2017: Changamoto kwa Tanzania


Ndugu wananchi, Siku ya Afya ya Macho Duniani huadhimishwa duniani kote Alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba ya kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha jitihada za kutokomeza upofu unaozuilika duniani. Mwaka huu siku hii itaadhimishwa tarehe 12 Oktoba 2017. Maamuzi ya kuadhimisha Siku ya Afya ya Macho Duniani yalifikiwa na Lions Club International Foundation mnamo mwaka 1998, na baadae kuungwa mkono na wadau wengine wa Huduma za Macho ambao ni pamoja na Shirika la Afya Duniani, Muungano wa Mashirika ya Kimataifa yanayojihusisha na Huduma za Macho (International Agency for Prevention of Blindness), Serikali mbalimbali, wataalamu wa masuala ya afya, taasisi mbalimbali na watu binafsi kuwa, ni tukio mahususi la kuhamasisha utekelezaji wa Dira ya Kimataifa ya Kutokomeza Upofu Unaozuilika Duniani ifikapo mwaka 2020 kwa kuthamini Haki ya Kuona kwa wote (Vision 2020: The Right to Sight). Serikali ya Tanzania iliridhia na kuungana na Mataifa mengine duniani katika kutekeleza azimio hili mnamo tarehe 23 Mei 2003.

Ndugu wananchi, Inakadiriwa kuwa, takriban watu milioni 285 duniani wana matatizo ya kutokuona. Kuna ongezeko kubwa la matatizo ya kutokuona duniani ambayo asilimia 80 ya hayo yangeweza kuzuilika. Idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya kutokuona (asilimia 90) wanaishi katika nchi zinazoendelea. Asilimia 65 ya watu wasioona ni wale wenye umri wa zaidi ya miaka 50, hili ni kundi linalochangia asilimia 20% ya watu wote duniani. Ongezeko la watu wenye umri mkubwa katika nchi nyingi kunamaanisha ongezeko la watu watakaokuwa hatarini kupoteza uwezo wao wa kuona kutokana na matatizo ya macho yanayoathiri umri huu. Inakadiriwa kuwa Watoto milioni 19 duniani wana matatizo ya kutokuona vizuri.

Ndugu wananchi, Kulingana na makadirio na takwimu za Shirika la Afya Duniani (World Health Organization), asilimia 1 (takriban watu 573,000) ya Watanzania hawaoni kabisa. Aidha, kwa ujumla watu wote wenye matatizo ya kuona kwa viwango mbalimbali hapa nchini wanakadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu wasiiona ambao ni takriban watu 1,730,000. Ndugu wananchi, Matatizo makubwa yanayosababisha upofu unaoweza kuzuilika hapa nchini na dunia kwa ujumla ni:-

Pamoja na sababu kuu hizo, bado jamii ina matatizo mengine ya macho yanayohitaji kupata ushauri wa kitabibu katika vituo vyetu vya Tiba. Ndugu wananchi, Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho kwa mwaka 2017 yamebeba kauli mbiu isemayo: AFYA YA MACHO KWA WOTE. Sambamba na kauli mbiu hii, ujumbe mahususi kwa jamii na wadau wa huduma za macho na afya kwa ujumla ni: “THAMINI UONI WA JICHO!” Kauli mbiu hii inatulenga na kutuonyesha sisi wanajamii, ni kwa nini afya bora ya macho inahitajika kwa kila mmoja na hasa watu wasiokuwa na tabia ya kupima afya ya macho yao mara kwa mara kama ishauriwavyo na kuwahamasisha kufanya hivyo. Kila mwana jamii anapaswa kupimwa afya ya macho yake angalao mara moja kwa mwaka.

Aidha, ujumbe mahususi unatoa rai kwa kila mmoja kwa nafasi yake, kuanzia mwanajamii, watoa huduma ya macho, watoa huduma nyingine za afya na viongozi wa ngazi mbalimbali kuchukulia uwezo wa kuona ni kuwa ni swala muhimu sana na la kuthaminiwa. Uelewa wa pamoja wa umuhimu wa uwezo mzuri wa kuona utawezesha watendaji wa ngazi mbalimbali za Serikali kwa kushirikiana na wafadhili wetu, kuboresha miundombinu na rasilimali watu kwa ajili ya kutolea Huduma za Macho. Mafanikio makubwa pia yatapatikana kwa kufikia makundi kama vile wazee, watoto, watu wenye ugonjwa wa kisukari, watu wenye ulemavu wa kutokuona ambao hautibiki, makundi ya watu walio katika mazingira hatarishi (vulnerable groups) pamoja na watu wenye ulemavu wa aina nyingine tofauti.

Ndugu wananchi, tunapoelekea kufikia mwisho wa utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Dira 2020 wa kutokomeza Upofu unaozuilika ifikapo mwaka 2020, kati ya watu 5 wenye ulemavu wa kutokuona, 4 ni wenye ulemavu unaotokana sababu ambazo zingeweza kuzuiliwa ama kutibika. Hali hii inahalalisha umuhimu wa kuweka nguvu zaidi katika kutatua changamoto hii. Mikakati ya kurejesha uwezo wa kuona ama kuzuia upofu ni kati ya mikakati ya afya inayoleta faida kubwa kwa kuwekeza kidogo tu.

Ndugu wananchi, kwa mwaka 2016, jumla ya watu takribani milioni 1 walihudhuria kwenye vituo vya tiba wakiwa na matatizo ya macho. Kati ya hao Milioni, asilimia 32 ni watoto wenye umri chini ya miaka 5. Idadi hii ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Watanzania. Aidha, kwa mwaka 2016, kulifanyika upasuaji wa mtoto wa jicho 23,000. Idadi hii pia ni ndogo sana hasa kwa kuzingatia kuwa asilimia 50 ya watu wenye ulemavu wa kutokuona, ambao ni 287,000 wana tatizo la mtoto wa jicho.

Ndugu wananchi, pamoja na jitihada za Serikali za Kuboresha afya ya kila Mtanzania, Tathmini ya Mfumo wa Kutolea Huduma za Macho hapa iliyofanyika mwaka jana hapa nchini ilibaini bado kuna mapungufu katika matofali yote 6 ya huduma za Afya kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani. Mapungufu hayo yalionekana kwenye maeneo yafuatayo:

Utawala na uratibu – Mfano: ushirikishwaji wa wadau wa macho katika kuweka vipaumbele vya huduma za Afya kwa ngazi zote. Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kwa ajili ya huduma za macho – Mfano: Bajeti ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji kwa ngazi zote. tolewaji wa Huduma ikijumuisha majengo na vifaa kulingana na rasilimali watu Uliyopo – Mfano: Huduma za macho kutokuwa na jengo au chumba kwa ajili ya kliniki, uchunguzi na huduma za upasuaji mdogo na mkubwa. Upatikanani wa dawa na mahitaji mengine – Mfano: Lensi kwa ajili ya upasuaji wa mtoto wa jicho na nyuzi za upasuaji. Upatikanaji wa rasilimali watu – Mfano: Uhaba wa Madaktari Bingwa, Wauguzi wa Macho na Wataalamu wa Optometria kwenye Hospitali za Umma kwa wastani wa asilimia 70. Ni mikoa 6 tu kati ya 26 yenye Madaktari Bingwa wa Macho. Upatikanaji wa Taarifa za huduma za macho. Mfano: kwa mwaka jana ni wastani wa asilimia 43 tu ya taarifa za huduma za macho ziliwasilishwa. Ndugu wananchi, ushirikishwaji wa wadau utawezesha upatikanaji wa huduma za macho kwa watu wote na kuepusha jamii kuwa walemavu kwa kuzingatia:-

Ndugu wananchi, hapa nchini huduma za macho zinatolewa na Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali kwa kupitia Vituo vya Tiba vya Umma, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na vituo Binafsi. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kuwashukuru wadau mbalimbali kwa ushirikiano katika mapambano ya kutokomeza upofu. Serikali peke yake haitaweza kukidhi mahitaji yote na hivyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea inatoa wito kwa wadau mbalimbali wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na Tawala za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, Taasisi za Mafunzo na Tafiti, Wana taaluma wa Fani ya Macho, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Makampuni, Asasi mbalimbali pamoja na watu binafsi kuendeleza ushirikiano hususan katika kuwekeza rasilimali kwenye huduma za macho.

Aidha, Wizara pia inatoa wito kwa Wadau wote kuendelea kuzingatia taratibu za Serikali ili kuhakikisha huduma za macho zinazotolewa kwa wananchi ni za viwango vinavyokubalika, gharama nafuu na pia kuwezesha upatikanaji wa taarifa zitakazotuwezesha kutathmini huduma za macho nchini kwa ujumla. Afya bora ya macho itaepusha Taifa kuingia kwenye gharama zitokanazo na huduma za kijamii kwa ulemavu wa kuona na pia itachangia kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati wa Viwanda. Aidha, Afya bora ya macho itawezesha nchi kufikia malengo ya MKUKUTA na Maendeleo ya Taifa kwa ujumla na kuchangia katika ufikiwaji wa malengo ya Maendeleo ya Kimataifa.

Ndugu wananchi, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Watanzania kwa ujumla kutumia wataalamu waliopo kwenye hospitali zetu kupima afya ya macho angalau mara moja kwa mwaka kwani kuna matatizo ambayo yanaleta upofu bila kuwa na dalili wakati wa hatua za awali za magonjwa hayo. “Tushirikiane kutokomeza ulemavu wa kutokuona” Asanteni sana kwa kunisikiliza.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.