Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Tunzeni sana vazi la neema ya utakaso katika maisha yenu!

Waamini wanahamasishwa kutunza ndani mwao ile neema ya utakaso waliyobahatika kupewa walipozaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu. - REUTERS

11/10/2017 15:08

Hulka ya mwanadamu inamvuta katika kutafuta raha na kuepa shida. Hakuna anayependa kusikia habari za kusikitisha kama ugonjwa, kifo au kupoteza jambo la thamani. Mambo haya humletea mwanadamu huzuni na hujisikia kupungukiwa. Lakini mmoja asikiapo habari ya furaha na tafrija hujawa na furaha na kwa hakika atajiandaa vyema kwa ushiriki wa karamu hiyo. Dominika ya leo inatuwekea mbele yetu karamu iliyoandaliwa na Mungu kwa ajili yetu. Sote tunaalikwa kushiriki karamu hiyo ambayo ni kitulizo cha roho zetu. Kila mmoja ajiweke tayari, ajiachanishe na ratiba nyingine za kidunia ili asije akaikosa karamu hii.

Karamu ambayo tunaalikwa kuishiriki ni karamu iliyoandaliwa na Mungu kwa ajili yetu sote. Karamu hii ni ukarabati wa ubinadamu wetu ambao ulichakazwa na dhambi. Katika somo la kwanza anatufunulia namna karamu hiyo ilivyoandaliwa na mahali ambapo imeandaliwa. “Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono iliyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu urojorojo wake, iliyochujwa sana”. Sehemu hii ya mwanzo inatuonesha karamu hiyo kwanza inaandaliwa juu ya mlima wa Bwana. Huu ni mlima Sayuni ambao juu yake umejengwa mji wa Yerusalemu, mahali ambapo hueshimika kama mlima wa Bwana. Karamu hii inaandaliwa kwa ajili ya watu wote. Ni uhakika kwa wokovu wa watu wote. Na mwisho ni karamu ambayo inaandaliwa katika hali njema kabisa.

Yote haya yanaupambanua ubora na ukuu wa karamu hii. Kwa hakika ni karamu iliyo bora kwani inakusudia kumpatia mwanadamu furaha kubwa kabisa. Na ni karamu kuu kwani inaandaliwa na Mungu mwenyewe aliye mkuu. Mmoja anapokwenda katika sherehe furaha yake huwa kubwa si kwa wingi wa watu au mapambo bali katika nafasi ya kwanza ni ubora wa chakula na vinywaji. Mwenyezi Mungu anatuandalia karamu hii bora ambayo itatupatia chakula na kinywaji kilicho bora na cha kweli. Hapa tunaoneshwa jinsi ambavyo mwanadamu anapendwa na kuinuliwa na Mungu. Dhambi ambayo inamuingiza katika huzuni inaweka mbele yake visasi, majivuno, chuki, hasira na machukizo yote. Haya ndiyo yanakuwa chakula chake. Lakini yeye anayeitikia mwaliko wa karamu ya Mungu atajazwa furaha na amani kwani karamu yake inatupatia unyenyekevu, upole, saburi, kuvumiliana na katika jumla ya yote tunaupata upendo wake usio na kikomo.

Mwanadamu huingia katika hali hiyo anapokuwa mbali na Mungu. Hivyo pasipo na Mungu kati yetu huingia maovu ambayo hutuweka mbali na karamu yake. Lakini yeye anayeitikia mwaliko huo na kupanda juu ya mlima wa Bwana atajazwa mema ya mbingu na kushibishwa kwa faraja zake. Karamu hiyo inayoelezewa na Nabii Isaya inaagua karamu ya Ekaristi Takatifu sana ambayo ni Sadaka ya Kristo Msalabani. Mwenyezi Mungu ametuandalia karamu hiyo kwa sadaka ya Mwanae mpendwa, sadaka ambayo imeturudishia hadhi yetu tuliyoipoteza kwa sababu ya dhambi. Karamu hii ya kipasaka ndiyo urojourojo na utamu ambao mwenyezi Mungu amenuia kutuandalia sisi wanadamu. Sadaka hii ni muhtasari wa fumbo zima la wokovu wetu linalohitimishwa katika nafsi ya Kristo, yaani kumwondoa mwanadamu katika utumwa wa dhambi na kumrudishia tena hadhi yake ya kuwa mwana huru wa Mungu, kumfanya tena kustahili kushiriki karamu ya mbinguni. Sadaka hii ya Kristo ilitolewa katika mlima huo huo mtakatifu wa Mungu wa Yerusalemu ili kutimia hilo aliloliagua Nabii Isaya kama tuonavyo katika somo la kwanza.

Changamoto inakuja katika mwitikio wa mwaliko wa karamu hii. Mwanadamu anayeitwa kutoka utumwani anapokea wakati mwingine katika namna hasi au wakati mwingine katika namna chanya. Karamu hii ipo tayari na Bwana Mungu wetu anatutaka kila mmoja wetu kuijongea ili kuzifaidi furaha zake. Wale wanaoitikia ndiyo ambao wanaukaribisha uwepo wa Mungu kati yao na hivyo watafurahia utajiri wake. Haya yataonekana katika maisha yaliyojaa upendo. Mmoja anayeitikia karamu hii atajaa huruma kwa wenzake, ataeneza masamaha, atawalisha na kuwanywesha wahitaji kwa ukarimu wake, atawatunza wenye shida au kwa ujumla atayaonesha matunda ya huruma ya Mungu yaliyojaa ndani mwake. Matokeo yake ni amani na uelewano ndani ya familia na jamii kwa ujumla.

Kinyume chake ni wale ambao wanapokea mwaliko huo katika namna hasi. Hapa tunaweza kuwaona katika makundi matatu. Kwanza wapo wale ambao hawataki kabisa kuisikia habari njema ya Kristo na hutafuta kila namna ya kuangamiza uwepo wake katika jamii ya watu. Kundi la pili ni la wale ambao daima wapo “bize” huku wamesongwa na shughuli za kidunia. Na kundi la tatu ni la wale ambao wanaitikia wito lakini wanakosa vazi la harusi. Makundi mawili ya mwanzo huleta kuzorota kwa kuenea kwa ufalme wa Mungu katika jamii ya mwanadamu. Haya yanaweza kuelezewa na jamii mambo leo ambayo inatafuta kuitenga jamii na maongozi ya Mungu. Ni pale mwanadamu anapotaka uhuru kamilifu, uhuru bandia ambao unampeleka katika kujifikiri yeye ni bwana na mmiliki wa ulimwengu huu. Katika hali hii Neno la Mungu ni kauzibe na halipewi nafasi.

Tunaona mwanadamu wa leo katika ukinzani huo yupo katika hali ya maangaiko. Faida ni chache au hakuna kabisa ukilinganisha na hasara. Familia nyingi zinaparanganyika na kwa anguko hili ubinadamu unapigwa kwa pigo kuu. Hii ni kwa sababu tunu za kiutu ambazo zinachochea na kuimarisha maisha ya kindugu zinapotea. Ndiyo maana si ajabu kuona uadui, visasi, rushwa na unyonyaji. Tunashuhudia ubinafsi na kutokuwajibika kwa watu katika nafasi mbalimbali. Tunaona vijana wetu wanajiloweka zaidi katika starehe na anasa na mengineyo mengi yanayochukiza. Kwa hakika tunaungamiza ubinadamu wetu kwa sababu tunakataa au tunafumbia macho mwaliko wa kushiriki wokovu tulioandaliwa. Tusiache mbachao kwa msala upitao.

Kundi la tatu ni la wale wanaoingia bila maandalizi madhubuti. Tunapoingia katika karamu tunapaswa kujiweka katika sare ya vazi la sherehe. Hii inamaanisha kuwa katika hali ya neema kama wanavyopaswa wana wa Mungu. Si suala la kuingia tu bali kujifananisha na wale waliopo karamuni. Ili ni dokezo la uwepo hai wa imani yetu. Katika mfano wa wanawali kumi: watano wenye hekima na watano wapumbavu (rejea Mt 25: 1- 13) tunaona wale wapumbavu wanashindwa kuingia karamuni kwa sababu walikosa mafuta. Ndiyo! walialikwa lakini wameshindwa kuweka hai uwepo wao. Kwa ubatizo sote tunaingia katika karamu iliyoandaliwa na Mungu. Lakini uwepo wetu hai utaifanya imani yetu kuendelea kung’aa. Hii ni kwa njia ya mazoezi mbalimbali ya kiimani ambayo kwayo tunajitajirisha imani yetu. Hapa ni kwa njia ya sala, masakramenti na neno la Mungu. Si suala la kujibwetesha tu na kutojishughulisha katika imani. Tukumbuke kwamba kukaa ndani ya maji si kibali kwamba umetakata.

Mtume Paulo anaona utajiri wa Mungu uliojazwa ndani mwake ni kielelezo cha kuyaweza yote katika hali zote. “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Uwepo wa Mungu ndani mwake ndiyo unamwezesha kuyatenda yote kwa kadiri ya mpango na mapenzi ya Mungu. Sala yake kwetu ni kujitengemeza kwa Mungu. Huku ndiko kuijongea karamu ambayo anatuandalia, karamu ambayo inafumbatwa na fumbo la Kristo. Mwisho anatuambia: “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.

11/10/2017 15:08