Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Mwaliko kwenye karamu ya uzima wa milele! Sharti ni vazi la harusi

Mwenyezi Mungu ameandaa karamu ya maisha ya uzima wa milele, jambo la msingi ni kuwa na vazi rasmi, yaani neema ya utakaso. - REUTERS

11/10/2017 15:54

Bila shaka mojawapo ya shughuli muhimu inayounganisha familia au jumuiya fulani au marafiki ni mlo na kinywaji cha pamoja. Watu wanapokutana kuzungumzia jambo fulani liwe kubwa au dogo au kutatua tatizo fulani liwe kubwa au dogo mwanzo wa kikao au mwishoni mwa kikao huwapo kinywaji au chakula ua vyote pamoja. Mlo wa pamoja ni muda ambao wote wapendanao wanaweza kukutana ili kula na kunywa pamoja na kushirikishana matumaini yao, mafanikio yao, hofu zao, uzoefu wao, mang’amuzi yao mbalimbali katika maisha au kusherehekea mafanikio fulani katika maisha yao. Hili tunaliona wazi katika jamii yetu hasa kunapokuwepo na tukio fulani jema jinsi watu wanvyojiandaa kwa sherehe ya kula na kunywa. Wanafamilia au ndugu au marafiki hutumia muda wa mlo wa pamoja kufahamiana, kukutana, kuongea kati yao na hata kusuluhishana mambo yanayowatatiza. Upendo unaowaunganisha unakomazwa na ikiwapo kutokuelewana basi muafaka hutafutwa. Mara nyingi pia tathimini ya ufanisi wa sherehe iko katika wingi wa vyakula na vinywaji viliyokuwepo.

Kwa uhakika wenye uadui au chuki hawawezi kula katika meza moja au kunywa katika kikombe kimoja. Leo katika maandiko matakatifu tunaona Bwana akitoa mwaliko wa sherehe. Ukifika nyumbani kwa mtu kwa kawaida hukupatia kinywaji na/au chakula. Ukarimu huu upo katika tamaduni zote za mwanadamu. Upo usemi kuwa ukitaka kumpata mtu kwa urahisi basi andaa chakula au kinywaji. Zipo sehemu hapa nchini chakula hutumika kama chambo ili kuwapata watu kwa mfano wakati wa kupiga kura au wa kufanya sensa ya watu. Hii yaonesha wazi kuwa chakula na kinywaji hutumika kuleta watu pamoja.

Katika hali ya kawaida ikitokea mgeni akikataa kula au kunywa basi mwenyeji anajisika vibaya sana. Pia akitokea mmoja kuwa mchoyo basi familia, ukoo na hata kabila zima humtenga mtu huyo au kumsema vibaya. Katika hati ya Mtaguso wa Pili wa Vaticani – Kanisa katika Ulimwengu wa Mamboleo – tunasoma – mlishe mwenye njaa kwani ukimnyima chakula, umemuua. Leo Bwana Yesu anatualika kwenye karamu. Anatualika ili tupate chakula cha uzima. Je, tunaitikia au tunatoa sababu mbalimbali pia leo kama tunayoona katika maandiko matakatifu jumapili ya leo? Katika somo la kwanza tunaona habari juu ya furaha ya hukumu ya Mungu inyoonekana katika mfano wa karamu kubwa. Ni mfano wa simulizi la karamu aliyotoa Yesu kuelezea furaha na heri ya mbingu.

Katika Injili mambo yafuatayo yanajionesha; mfalme ni Mungu na karamu ya harusi ni heri ya kimasiha, mwana wa mfalme ni masiha, watumwa ni manabii na mitume, waalikwa waliodharau au kufanya taabu ni Wayahudi, wakusanywao toka katika barabara za mji ni wakosefu na wapagani, kuteketea mji kwa moto ni uangamizi wa mji wa Yerusalemu. Katika kutambua au kukataa mwaliko huo kifuatacho ni hukumu hivyo basi mtu aitikiaye mwaliko wa karamu ya harusi hana budi kuvaa mavazi ya harusi. Matendo ya haki ni lazima yafuatane na imani. Tuone mifano michache ya ushiriki wa sherehe katika mlo katika Maandiko Matakatifu. Katika Agano la Kale: Mwa. 18:1-8 – Abrahamu anawakaribisha wageni asiowajua. Anawapikia chakula na kumbe walikuwa watumishi wa Mungu walioleta habari njema kwamba Sara atapata mtoto. Tob. 7:9 – Raheli anachinja mnyama na kumkaribisha ndugu yake Tobia. Tobia naye baada ya kula anampa mke.

Katika Agano Jipya: Yoh. 2:1 – Yesu anahudhuria harusi ya Kana. Katika muujiza anatoa alama ya uzima na upendo. Wanaokutana wanafurahi. Mk. 2:13-17 – tunaona habari ya wito wal Lawi na karamu ya wakosefu. Yesu anakaribia nyumbani kwake na anapata nafasi ya kukutana na wenye dhambi na watoza ushuru.  Lk. 15:11-32 – habari ya mwana mpotevu. Mwana mpotevu aliporudi nyumbani baba yake anamchinjia ndama aliyenona. Washiriki wanakula na kufurahi. Lk. 24 – pamoja na maelezo yote na muda waliotumia njiani lakini walipoketi mezani kula na kunywa wakamtambua katika kuumega mkate.

Lk. 22 – ukamilifu katika sakramenti ya Ekaristi, sakramenti ya uzima wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Mungu anatupatia chakula na kinywaji cha uzima. Mifano hii michache toka maandiko matakatifu utufikirishe leo juu ya ushiriki wetu katika karamu zetu tufanyazo – tumeona kuwa makutano na milo hiyo imeleta uzima na imezaa upendo unaodumu.  Bila shaka sote twatambua kuwa katika mlo undugu na urafiki unajengwa. Upo msemo wa Kiyahudi kuwa njaa ikiingilia mlangoni upendo hupaa kupitia dirishani. Katika Biblia hadhi hii ya mlo inaunganisha Mungu na mwanadamu. Wakamtambua katika kuumega mkate. Tunakumbushwa kuwa hata sisi katika milo na sherehe zetu za kila siku yupo Mungu na mwanadamu kati yetu.

Tunasoma katika 1Kor. 11:23-29 – habari ya Paulo juu ya ushuhuda wa karamu ya Bwana; maana kila muulapo mkate huu na kukinywa kikombe hiki mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Kwa kifupi ni kuwa kila aulaye mwili na kunya damu yangu anao uzima wa milele. Kwa kufanya mkate na divai kwa mwili na damu yake, ekaristi inakuwa kifungo cha upendo na ishara ya umoja na inatupatia uzima kati ya Mungu na mwanadamu. Katika ekaristi tunashiriki upendo na uzima. Katika masomo yetu ya leo tunachoona ni kuwa Bwana ametualika kwenye karamu yake. Tuwe tayari kwenda ili tushiriki uzima na upendo wake Mungu. Katika 1Kor. 10:16-17 tunasoma; kikombe kile cha Baraka tukibarikicho Je, si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao si ushirika wa mwili wa Kristo? Katika mfano wa Injili ya leo tunaona makundi matatu ya watu kati ya waliolikwa karamuni;

Wapo waliokubali mwaliko – muda ukifika wanajitoa, wana shughuli zao, hawajali hata ule upendo na ule muda aliotumia mtoa mwaliko. Ipo hatari pia katika maisha yetu kujali zaidi mambo yetu na shughuli zetu na kusahau pia uwepo na upendo wa mwenzetu, mialiko mizuri ya kukaa pamoja na hata kufikia kuudharau mwaliko wa Mungu Wapo wanaofika karamuni bila mwaliko rasmi – hawa hawahangaiki kujiandaa ipasavyo, hawajali na hawana muda wa kufanya hivyo. Wako karamuni kimwili tu lakini kiroho na kiakili hawapo kabisa. Yesu anachukia hali hii ya uvuguvugu. Wapo wanaofika karamuni, wanaochukua muda kujiandaa ili walingane na hadhi ya sherehe. Hawa wanajali na wanaweza kutofautisha mambo, wanaingia katika sherehe ya mfalme wakiwa na mavazi rasmi. Hawa tuwafuate.

Katika Injili ya Lk. 14: 18-20 tunaona sababu nyingi tu za kutokwenda karamuni – shamba, biashara, ununuzi wa ng’ombe, kuoa mke na kadhalika. Zote hizi ni sababu za msingi na ziko katika mahitaji ya mwanadamu. Hawa wanaonesha shughuli na mahangaiko yao ya kibinadamu. Ni vizuri lakini pia ipo shughuli muhimu ya Mungu. Tunaipa nafasi gani? Hatuna budi kutofautisha mambo yetu na mambo yanayomhusu Mungu. Maandiko haya matakatifu yatupe changamoto hasa nyakati zetu hizi ambapo kila mmoja wetu anaonekana kuwa na shughuli nyingi na mambo mengi kupita hata uwezo wake. Tunasahau si tu mambo ya Mungu bali pia hata na ya wenzetu.

Hapa tunaona kuwa; Wanaojiweka nje ya karamu ya bwana wanajinyima furaha na uzima unaopatikana kwa kuwa pamoja. Wao wanaokubali mwaliko wanakumbushwa wasichezee neema ya Mungu iliyomiminwa kwao ila wajiweke safi daima na wenye kumpendeza Bwana mwenye karamu yaani Mungu Katika Yoh. 6:55-56 tunasoma – kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu nami hukaa ndani yake. Basi ndugu zangu, leo Yesu anatukaribisha kwenye karamu ya mbinguni. Karamu isiyo na gharama wala malipo lakini inayohitaji utayari wetu na maandalizi yetu kuingia katika ufalme wa Mungu. Anatulika kuwa tayari kuwaandalia wenzetu karamu, yaani pamoja naye Bwana, tuwapatie upendo, uzima, matumaini na furaha ya uzima utokao mbinguni.

Tumsifu Yesu Kristo. 

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S

11/10/2017 15:54