Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Habari \ Habari kutoka Barani Afrika

Kenya hali kwa sasa ni tete!

Bwana Raila Odinga amejitoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania Urais hapo tarehe 26 Oktoba 2017. - AFP

11/10/2017 14:48

Katika mazingira ya kutatanisha kuhusu hatma ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, hapo tarehe 26 Oktoba 2017, Bwana Raila Odinga ameamua kubwaga manyanga na kutangaza rasmi kwamba, hatashiriki katika kuwania uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao! Bwana Odinga, Jumanne, tarehe 10 Oktoba 2017 amesikika akisema, kwamba, uchaguzi mkuu ujao hauwezi kuwa huru na wa haki kwani viongozi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)  hawajabadilishwa kwani wao ndio waliokuwa sababu ya kuharibika kwa uchaguzi mkuu uliopita hapo tarehe 8 Agosti 2017.

Wakati huo huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema, mchakato wa uchaguzi mkuu utaendelea kama ulivyopangwa hapo tarehe 26 Oktoba 2017 na kwamba, Chama tawala kinatarajia kuibuka na ushindi wa “Tsunami” wakati huu, ikilinganishwa na wakati uliopita. Rais Kenyatta anamshutumu Bwana Odinga kwa kuendekeza siasa zinazotaka kuligawa taifa kwa misingi ya ukabila na umajimbo. Hali nchini Kenya kwa sasa inaendelea kuwa tete, huku macho na masikio ya wapenda amani yakiendelea kuelekezwa nchini Kenya, ili kufahamu hatima ya uchaguzi mkuu hapo tarehe 26 Oktoba 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

11/10/2017 14:48