2017-10-11 14:05:00

Familia ya Mungu nchini Kenya iweni mashuhuda wa matumaini na huruma


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ilikuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kumtafakari kwa kina na mapana Kristo Yesu kama uso wa huruma ya Mungu, muhtasari wa fumbo la imani ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira ni mwingi wa rehema na kweli. Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani; ni sheria msingi katika hija ya maisha ya kiroho na daraja kati ya Mungu na binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya amekazia kwa namna ya pekee kabisa: umuhimu wa hija za maisha ya kiroho, daima wakiongozwa na kauli mbiu “Iweni na huruma kama Baba wa mbinguni”.

Baba Mtakatifu Francisko, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili sanjari na kujitafutia muda wa kukaa na kumsikiliza Kristo Yesu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Huu ndio “mpango mkakati wa masaa 24 kwa ajili ya Bwana”. Baba Mtakatifu alikazia toba na wongofu wa ndani ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kiasi hata cha kuwatuma wamisionari wa huruma, kielelezo cha Kuhani mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika mambo ya Mungu na kwamba, huruma kamwe haipingani na haki!

Hivi karibuni, Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudani ya Kusini, wakati wa kongamano la kitaalimungu lililofanyika huko Nairobi, Kenya, amewataka wakleri kuhakikisha kwamba, wanajitaabisha kuitafakari dhana ya huruma ya Mungu na kuifanyia kazi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kulinda na kudumisha: utu na heshima ya binadamu hasa katika ulimwengu mamboleo ambamo vita, ghasia na nyanyaso mbali mbali zinaendelea kunyanyasa binadamu aliye umbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mapadre wajenge ndani mwao moyo wa huruma na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, huruma na mapendo ya Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, amejifunua kuwa ni Mungu mwenye huruma na mapendo, yanayomwambata na kumzunguka mwamini kama afanyavyo mama kwa mtoto wake. Huruma ya Mungu inajikita katika msamaha, hali inayowapatia nafasi watoto wake kukua na kukomaa katika upendo wa Mungu, unaopaswa pia kumwilishwa kwa jirani kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huruma ya Mungu ni changamoto ya toba na wongofu wa ndani, ili kuambata upendo huu unaotolewa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho; mahakama ya huruma ya Mungu. Ikumbukwe kwamba, waamini wanaimarishwa katika safari ya maisha yao kwa njia ya msamaha wa dhambi.

Wakati huo huo, Padre Lucas Ongesa, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, akichangia mada kwenye warsha kuhusu Waraka Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” amekazia mambo kwamba, huruma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanapaswa kuchuchumilia mambo msingi katika maisha, tayari kuyatolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Toba na wongofu wa ndani; upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ambao kimsingi ni amana na utajiri wa Kanisa ni mambo msingi yanayoweza kulipyaisha Kanisa kwa kuambata utakatifu wa maisha.

Hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu kinachopania kuwaonjesha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka na kwamba, kila mtu anaalikwa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yake. Ni kipindi cha huruma ya Mungu, ili maskini na wanyonge waweze kuangaliwa kwa heshima pamoja na kujali utu na mahitaji yao msingi kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha badala ya kugubikwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Ni muda wa huruma ya Mungu, ili wadhambi waweze kutubu na kumwongokea Mungu. Ni kipindi cha kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, udugu na upendo unaowashirikisha watu wote bila ubaguzi!

Ili kuweza kukabiliana na changamoto za umaskini wa hali na kipato, kila mwaka kuanzia sasa Jumapili ya XXXIII ya Mwaka wa Kanisa, itakuwa ni Siku ya Maskini Duniani, kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu inayofunga Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alijitambulisha na maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, Siku ya hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kwa jinsi walivyowajali na kuwahudumia maskini. Lakini, ikumbuke kwamba, maskini ni kiini, amana na utajiri wa Habari Njema ya Wokovu. Bila ya kupambana na umaskini haiwezekani kuwa na haki wala amani! Siku ya Maskini Duniani itakuwa ni njia nyingine ya Uinjilishaji mpya inayopania kupyaisha Uso wa Kanisa katika mchakato wa kuendeleza wongofu wa kichungaji, ili kuwa kweli shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu!

Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji ”Misericordia et misera” yaani ”Huruma na amani” uliotiwa mkwaju na Baba Mtakatifu mwenyewe Jumapili tarehe 20 Novemba 2016 wakati wa kufunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Mwaka wa huruma ya Mungu umekuwa ni kipindi muafaka cha kuadhimisha na kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu. Huruma ni kiini na muhtasari wa maisha na utume wa Kanisa unaofunua ukweli wa ndani kabisa wa upendo wa huruma ya Mungu.

Padre Lucas Ongesa, anasema, huruma ni kiini na maisha ya Mungu na utambulisho wake kwa mwanadamu. Huruma ni muhtasari wa historia nzima ya uumbaji inayopata utimilifu wake katika kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.  Kristo Yesu, ni mlango wa huruma ya Baba wa milele, changamoto kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wa Mungu kwa binadamu, kwani anatamani kuwaona waja wake wakiwa na afya tele, watu wenye furaha na amani ya kweli. Haya ni mambo msingi yanayoendelea kutiliwa mkazo na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema huruma ya Mungu imekuwa ni kauli mbiu katika maisha na utume wake katika shughuli za kichungaji “Miserando atque eligendo”. Yesu alimwangalia Mathayo mtoza ushuru kwa jicho la huruma, upendo na msamaha, kiasi hata cha kugusa undani wa maisha yake, akatubu na kumwongokea Mungu, leo hii ni chombo na shuhuda wa huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mungu kwa njia ya Kristo na Kanisa lake. Kanisa linapaswa pia kuwa ni chombo na Sakramenti ya huruma ya Mungu kwa binadamu, mahali ambapo watu wanaweza kujichotea upendo, huruma na huduma makini katika mahangaiko yao: kiroho na kimwili! Wajumbe wa warsha hii kwa muda wa siku tano, wamepembua pia kuhusu huruma mintarafu Maandiko Matakatifu; ufafanuzi wa huruma katika masuala ya kitaalimungu na kimaadili; huruma katika Sakramenti ya Upatanisho; huruma ndani ya familia na huruma katika muktadha wa mazingira ya Kiafrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.