Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Habari \ Habari za Kimataifa

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili wa Watoto wadogo, 2017

Tarehe 11 Oktoba kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya kupambana na ukatili wa watoto wadogo. - AFP

10/10/2017 11:49

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, inaadhimisha Siku ya Kimataifa dhidi ya ukatili kwa watoto katika maisha yao ya kila siku. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wanawake milioni 120 wenye umri chini ya miaka 20 ambao wamejikuta wakilazimika kuolewa huku wakiwa na umri mdogo. Baadhi yao ni watu ambao wameteseka sana kutokana na nyanyaso na dhuluma walizokuwa wakifanyiwa majumbani mwao. Ni watoto ambao pia wameteseka ka kukosa fursa ya kuendelea na masomo na pengine kufanyishwa kazi za suluba!

Hizi ni takwimu ambazo zimetolewa na Terre de Hommes wa Shirika la Kulinda Watoto Wadogo. Anasema, dhuluma, nyanyaso na ghasia ni chakula cha kila siku kwa baadhi ya watoto, vitendo wanavyofanyiwa na wazazi, walezi, ndugu na hata wakati mwingine majirani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watoto wanapata fursa ya kuanza na kuendelea na masomo, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha na hatimaye, kuokoa maisha ya watoto wadogo ambao ni matumaini ya jamii kwa sasa na kwa siku za usoni.

Takwimu zinaonesha kwamba, ghasia ni kati ya mambo yanayochangia vifo vya watoto wadogo kati ya miaka 10 hadi 19 na wengi wao ni wale wanaotoka Barani Afrika. Kuna watoto zaidi ya milioni kumi na moja wanaofanyishwa kazi za majumbani; wanadhalilishwa utu na heshima yao kwa kufanyishwa biashara ya ngono na picha za aibu kwenye mitandao; hali inayoitaka Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati ili kulinda, kutetea na kudumisha utu, malezi na makuzi ya watoto wadogo katika hatua mbali mbali za maisha yao.

Watoto sehemu mbali mbali za dunia, wanapaswa kuwa na uhakika wa kupata: elimu bora, huduma ya afya, ulinzi na usalama dhidi ya nyanyaso, dhuluma na ubaguzi wa kina aina. Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2016 ulianzisha kampeni dhidi ya ukatili kwa watoto wadogo, changamoto ambayo inapaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali ili kulinda maisha, utu na heshima ya watoto wadogo ambao kwa sasa wanakabiliwa pia na hatari ya kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu, kazi za suluba, utumwa mamboleo na mifumo yake yote pamoja na ukatili. Siku ya Kimataifa dhidi ya ukatili kwa watoto, iwe ni nafasi ya kuwaonjesha watoto upendo na mshikamano wa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

10/10/2017 11:49