2017-10-09 09:48:00

Hali ya maisha na utume wa Kanisa nchini Australia


Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limehitimisha mkutano wake na viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Vatican,  chini ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 7 Oktoba 2017. Kwa muda wa juma zima, Baraza la Maaskofu Katoliki Australia chini ya uongozi wa Askofu mkuu Denis James Hart, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Australia. Imekuwa ni fursa ya kuzungumzia kwa kina na mapana hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Australia kwa wakati huu.

Kati ya mambo msingi yaliyojadiliwa ni: Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini humo na madhara yake katika maisha na utume wa Kanisa; Uhusiano uliopo kati ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Jitihada zinazofanywa na viongozi wa Kanisa katika kurejesha tena imani na matumaini kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Australia pamoja na kuwajengea uwezo mkubwa wa ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa;pamoja na ushiriki wa walei katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limekutana na kuzungumza kwa kina zaidi na Kardinali Pietro Parolin, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu pamoja na Askofu mkuu Giacomo Morandi, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Kanisa nchini Australia linapitia kipindi kigumu cha maisha, utume na historia yake kutokana na uhusiano tenge kati ya Kanisa na Serikali, baada ya Serikali kumfungulia mashtaka Kardinali George Pell kwa kumtuhumu kuhusika na kashfa ya nyanyaso za kijinsia wakati alipokuwa Askofu mkuu Jimboni mwake, miaka kadhaa iliyopita. Kardinali Pell, alilazimika kuomba likizo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ili kurejea tena nchini Australia, kujibu shutuma hizi ambazo wakati wote amena kutojihusisha nazo ili ukweli uweze kufahamika na sheria kuchukua mkondo wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.