2017-10-06 17:00:00

Vatican yazindua makazi mapya ya ubalozi wake Minsk, nchini Belarus


Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko, mmisionari wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa, hapo tarehe 4 Oktoba 2017, Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican alizundua makazi mapya ya Ubalozi wa Vatican nchini Belarus, tukio ambalo limehudhuriwa na viongozi wa Serikali, Kanisa na familia ya Mungu katuka ujumla wake. Tukio hili limekwenda sanjari na kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Belarus. Hii ni nafasi muhimu sana kwa Kanisa kuendelea kutekeleza utume wake kwa familia ya Mungu duniani.

Askofu mkuu Angelo Becciu ametumia fursa hii pia kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Belarus na kwamba, Ubalozi wa Vatican ni kielelezo makini cha uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu nchini humo! Ubalozi huu unazungukwa na maeneo muhimu ya kihistoria na kitamaduni kwa watu wa Belarus, changamoto ni kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, daima mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili yakipewa kipaumbele cha kwanza. Malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya ni changamoto ambayo kwa sasa inavaliwa njuga na Mama Kanisa kama sehemu utume wake kwa vijana.

Ni dhamana ya Wakristo nchini Belarus kujenga madaraja ya: umoja, mshikamano na udugu yanayofumbatwa katika majadiliano ya kiekumene, ili kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya: haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa dhati kabisa ikiwa kama watakuwa wameungana na kuwa kitu kimoja chini ya Kristo mchungaji mwema. Huu ndio mwelekeo wa diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anakazia ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kama ndugu; kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na dhana potofu ya usawa wa kijinsia inayokwenda kinyume kabisa cha mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu!

Askofu mkuu Angelo Becciu amekazia umuhimu wa Injili ya familia inayojikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu unaoshuhudiwa na watu wengi nchini humo! Licha ya maendeleo na mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini humu, lakini bado kuna madonda ya vita, chuki, utengamo na mauaji ya kimbari. Sehemu kuu ya makazi ya ubalozi wa Vatican mjini Minsk, Belarus imewekwa kwa ajili ya sala na tafakari ya Neno la Mungu; mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, kama ushuhuda uliotolewa na wafiadini wa Belarus. Vatican kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa inataka kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu; ustawi, maendeleo, mafao ya amani ya kweli. Wafanyakazi wa Vatican wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa huduma ya upendo pasi na makuu; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Ni fursa ya kutumia kikamilifu karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 







All the contents on this site are copyrighted ©.