2017-10-06 15:34:00

Papa Francisko: Aibu ya dhambi iwasaidie waamini kutubu na kuongoka


Waamini wanapaswa kufanya toba na wongofu wa ndani kwa kutambua haki na huruma ya Mungu katika maisha yao; kwa kuona aibu kutokana na dhambi iliyotendwa na watu mbali mbali na kwamba, hakuna hata mtu mmoja anayeweza kujidai kuwa hana dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. Watu wamemwasi Mungu na wametenda maovu mbele yake, kiasi cha kushindwa kutii Amri na Maagizo yake wala kutembea katika njia zake! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 6 Oktoba, 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican.

Anaendelea kufafanua kwamba, watu wote wametenda dhambi na kutindikiwa kwa sababu ya kukosa utii kwa Mwenyezi Mungu. Watu wameasi na kushindwa kusikiliza Amri na Maagizo yake. Mwenyezi Mungu amezungumza na mtu binafsi na wakati mwingine kwa njia ya wazazi, walezi, viongozi wa Kanisa na hata jamii katika ujumla wake, lakini bado mwanadamu amekuwa na shingo ngumu! Waamini wamesikiliza mahubiri yanayotolewa Kanisani mara ngapi, lakini bado wameendelea kutembea gizani? Anahoji Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa bahati mbaya, mwanadamu katika maisha yake, amejikuta akiendelea kumwasi Mwenyezi Mungu na kufuata njia inayomwelekeza kwenye kutenda maovu! Matokeo yake, anasema Nabii Baruku katika Somo la kwanza, mwanadamu ameonja kipigo kutoka kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuandamwa na laana. Haya ni mambo yanayojificha katika wivu, chuki na hasira, matusi na kinyongo pamoja na mapambano ya kutaka kuwaangamiza wengine. Matendo yote haya anasema Baba Mtakatifu ni kwenda kinyume cha Mwenyezi Mungu ambaye ni mwema na mpole, changamoto na mwaliko wa kuona aibu, tayari kutubu na kumwongokea Mungu kwani aibu ni neema ya kutambua udhaifu na dhambi inayomwandama mwanadamu!

Aibu anasema Baba Mtakatifu ni lango la toba na uponywaji wa ndani, changamoto na mwaliko kwa waamini kujisikia aibu mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kumkimbilia kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia huruma, upendo na msamaha wake wa daima. Aibu inayosimikwa katika: unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani inamsukuma Mwenyezi Mungu kuwakimbilia waja wake, kuwakumbatia na kuwasamehe dhambi zao. Nabii Baruki, amewaonesha waamini njia ya kufuata ili kutubu na kumwongokea Mungu, kwani amependa kuonesha uwezo na nguvu zake kwa njia huruma na msamaha wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.