2017-10-06 16:08:00

Mwenyeheri Padre Arsenio da Triogolo, muasisi wa Shirika la Kitawa!


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 7 Oktoba 2017 katika Ibada ya Misa Takatifu, huko Jimbo kuu la Milano, Italia, anamtangaza Padre Arsenio da Trigolo, O.F.M, wa Shirika la Wakapuchini kuwa Mwenyeheri. Hii ni furaha na shukrani kubwa kwa Mwenyezi Mungu kwa Shirika la Watawa wa Bikira Maria Mfariji, kuona jina la muasisi wa Shirika lao likiandikwa kwenye kitabu cha watakatifu. Hili ni Shirika ambalo limezamisha mizizi yake ya maisha na utume wake nchini Italia, China, Libia, Pwani ya Pembe, Burkina Faso, Brazil, Equador na hivi karibuni, limetua nanga ya matumaini nchini Angola.

Kardinali Angelo Amato katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, Mwenyeheri Padre Arsenio da Trigolo alikuwa ni Padre mwenye furaha katika maisha na wito wake kwanza kabisa kama Padre wa Jimbo, baadaye akajiunga na Wayesuit na hatimaye, akawa Mkapuchini, daima akiwa kwenye mchakato wa kutafuta ukamilifu na utakatifu wa maisha kwa ajili yake binafsi na jirani zake. Ni Padre aliyependa sana kusali, kusadaka maisha yake, akaonesha bidii, juhudi na ari kubwa katika kazi. Alikuwa gwiji wa maisha ya kiroho, mhubiri na mtoa mafungo mashuhuri sana kwa nyakati zake! Alijifunza sanaa ya kuunganisha na kuwa kweli chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake, wakati alipokuwa kwenye kiti cha maungamo!.

Pamoja na karama mbali mbali alizojaliwa na Mwenyezi Mungu, alibahatika pia kuwa ni mtu mnyenyekevu na mkarimu sana; nguzo msingi katika maisha yake ya utakatifu. Ni kiongozi aliyeishi, akawafundisha na kumwilisha tunu hizi katika maisha ya watawa wa Shirika lake, ili daima kujishusha kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu! Kwa njia ya unyenyekevu, mwamini anapata nafasi ya kuwaheshimu, kuwapenda na kuwahudumia wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kuwa ni chombo cha upatanisho na maridhiano kati ya watu kwa ajili ya upendo wa Mungu kwa binadamu.

Daima aliwahimiza watawa wake kuwa wanyenyekevu bila kuogopa wala kuwa na makunyanzi usoni! Mwenyeheri Padre Arsenio da Trigolo, alikuwa ni mtu aliyebarikiwa kuzunguza sana, akawahudumia wote kwa huruma na upendo; huku kila mtu aliyebahatika kukutana naye, akamwachia tabasamu la kukata na shoka! Alifanya kazi bila kuchagua, kiasi cha kuaminiwa na kuthaminiwa na jirani zake! Alikuwa kama chombo au bustani ambamo, watu walikwenda kutua mizigo yao ya maisha ya kiroho na huko wakapa faraja na utulivu rohoni na nafsini mwao! Alikuwa ni Baba mwenye huruma hasa kwa watawa walipokuwa wanarejea kutoka kwenye utume wao! Aliweka utaratibu wa kuwapatia mapumziko kidogo kabla ya kuendelea na shughuli nyingine.  Urithi mkubwa kutoka kwa Mwenyeheri Padre Arsenio da Trigolo ni mfano bora wa maisha na karama zake; changamoto na mwaliko wa kuwa waaminifu na wadumifu katika: utume, maisha na wito wa kila mwaminifu, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kutangazwa kwake ni ushuhuda wa uthabiti wa karama ya Shirika lao ambayo ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa zima kama ushuhuda wa utume wa upendo. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, kwa maombezi ya Mwenyeheri Padre Arsenio da Trigolo, Shirika lake, litaendelea kubarikiwa kwa kuwa na watawa: wema, watakatifu na wachapa kazi waaminifu katika Shamba la Bwana, tayari kutangaza na kushuhudia furaha na upendo wa Injili kwa watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.