2017-10-05 07:19:00

Utume wa Bahari: Uvuvi unao wajibisha na kudumisha utu wa binadamu!


Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, chini ya uongozi wa Kardinali Peter Turkson, kuanzia tarehe 1 hadi 7 Oktoba 2017, linaendesha Kongamano la XXIV la Kimataifa la Utume wa Bahari, huko Kaohsiung, nchini Taiwan. Kongamano hili limefunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyongozwa na Kardinali Peter Turkson na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, ukasomwa na Monsinyo Sladan Cosic, Afisa wa Ubalozi wa Vatican nchini Taiwan.

Baba Mtakatifu katika ujumbe aliomwandikia Rais wa Kongamano la XXIV la Kimataifa la Utume wa Bahari, anapenda kuchukua nafasi hii kuwatakia heri na baraka washiriki wote wa kongamano hili, kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa neema na baraka zake anazoujalia Utume wa Bahari kwa miaka mingi sasa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wajumbe wote wanaoshiriki katika kongamano hili wataimarishwa zaidi katika utume wao na wadau mbali mbali wanaotekeleza dhamana na utume wao baharini.

Kongamano hili kwa namna ya pekee kabisa, linajielekeza katika mahitaji msingi: kiroho na kimwili kwa watu wanaofanya kazi katika sekta ya uvuvi. Baba Mtakatifu anasema, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanayo mambo mengi wanayoweza kujifunza kutoka kwa wavuvi. Kanisa linapenda kutoa nafasi kwa ajili ya kutafakari Fumbo la Mungu ambalo linawaambata na kuwakumbatia watu wote kwa njia ya Mama Kanisa na hatimaye, kuwaelekeza wote kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka wavuvi pamoja na familia zao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya asubuhi na mlango wa Bahari!

Wajumbe wa kongamano hili wamepokea salam na matashi mema kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Taiwan, Baraza la Maaskofu Katoliki Taiwan na kusikiliza hotuba elekezi iliyotolewa na Kardinali Peter Turkson kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Tuwe watunzaji wa kazi ya uumbaji, walinzi wa jirani na mazingira”. Wajumbe wamechambua kwa kina na mapana vitisho vinavyowakabili wafanyakazi baharini na madhara yake katika sekta ya uvuvi duniani. Wamepata nafasi ya kusikiliza shuhuda mbali mbali kutoka kwa wafanyakazi wa Utume wa Bahari na familia zao, kwa kuzingatia mambo msingi ya kijamii na kichungaji.

Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na athari zake ni mada ambayo imechambuliwa na Askofu Marcelo Sanchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi pamoja na Sayansi Jamii. Amewafafanulia kwa kina na mapana, jitihada zinazofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa mapambano wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kongamano hili, limekuwa pia ni fursa ya kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 97 tangu Utume wa Bahari Ulipoanzishwa. Kardinali Charles Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon, nchini Myanmar, amewaelezea wajumbe wa Kongamano hili hali halisi ya wavuvi nchini Myanmar pamoja na mateso ya wananchi wa Rohingya, ambao wananyanyaswa na kudhulumiwa: utu na heshima na haki zao msingi kama binadamu. Haki msingi za wavuvi; changamoto mamboleo zinazo ukabili Utume wa Bahari; Uvuvi endelevu, tatizo la uharamia baharini, changamoto kubwa nchini Somalia. Biashara haramu ya watoto wadogo nchini Ghana; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, mada inayochambuliwa na Dr. Michel Roy, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.