2017-10-05 06:51:00

Kanisa linataka kuwasikiliza kwa dhati vijana na changamoto zao!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yatakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 19- 24 Machi 2018, tayawashirikisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hili ni tukio ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu pamoja na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha.

Kardinali Baldisseri anapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kuitisha maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu, tukio ambalo litawapatia vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kushirikisha mawazo yao, matumaini, shida na wasi wasi unaowazunguka katika ulimwengu mamboleo. Huu ni mwendelezo wa mapokeo ya maadhimisho ya Sinodi, kama ilivyojitokeza kunako mwaka 1987 kuhusu: Wito na Utume wa waamini walei Kanisani na Ulimwenguni na kama Kongamano la Kimataifa lililofanyika kunako mwaka 1991 kabla ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa Bara la Ulaya.

Katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu wamealikwa vijana wawakilishi kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia; watawa na majandokasisi; vyama vya kitume; Makanisa ya Kikristo pamoja na wawakilishi wa waamini wa dini mbali mbali duniani. Kutakuwepo na wawakilishi kutoka katika taasisi za elimu na utamaduni; kazi, sanaa na michezo; watu wa kujitolea, wataalam na mabingwa wa elimu, majiundo, malezi na makuzi ya vijana katika mchakato wa kufanya maamuzi katika maisha yao.

Kardinali Baldisseri anakaza kusema, maadhimisho haya yataboresha kwa kiasi kikubwa, maandalizi ya Hati ya kutendea Kazi sanjari na majibu kutoka kwa vijana sehemu mbali mbali za dunia, yanayoendelea kutolewa kwa njia ya mitandao ya kijamii. Nyaraka zote hizi zitafanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Hitimisho la maadhimisho haya itakuwa ni fursa kwa vijana kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, mwanzo wa Juma kuu kwa kuungana na Baba Mtakatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu pia ya maadhimisho ya Siku ya XXXIII ya Vijana Kimataifa kwa mwaka 2018, inayoadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo, kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Usiogope, Mariam, kwa maana umepata neema kwa Mungu”. Lk. 1:30.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.