Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Papa Francisko: Wakristo ni vyombo na mashuhuda wa matumaini!

Papa Francisko anawakumbusha waamini kwamba wao ni vyombo na mashuhuda wa matumaini ya Kikristo.

04/10/2017 14:12

Mwezi Oktoba umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari, moyo na mwamko wa maisha na shughuli za kimisionari. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Oktoba, sanjari na maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyebahatika kuwa ni kati ya wamisionari wa matumaini, amefafanua umuhimu wa wamisionari wa matumaini kwa nyakati hizi! Mama Kanisa ni Nabii anayetumwa kutangaza na kushudhia: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kiini cha imani, faraja na matumaini ya Kikristo.

Injili ya Kristo Yesu haikamiliki kwa Ijumaa kuu, bali inakwenda mbali zaidi kwa kuangalia jinsi ambavyo Mitume wa Yesu walivyokuwa wamenyong’nyea baada ya mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Jiwe lililowekwa mbele la mlango wa kaburi la Yesu, liliziba ari, mwamko na shahuku waliyokuwa nayo Mitume wa Yesu kwa muda wa miaka mitatu ya kuishi bega kwa bega na Kristo Yesu, Mwalimu wao. Yote walidhani kwamba, yamekwisha na baadhi yao wakaingiwa na hofu na woga, wakaghafirika na kuanza kutafuta njia mbadala ya maisha kwa kuondoka kutoka Yerusalemu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ulileta mageuzi makubwa katika akili na mioyo ya Mitume wa Yesu, kiasi cha kuwapatia dira na mwelekeo mpya, kwani ufufuko wa Kristo unavishirikisha na kuviambata viumbe vyote. Mitume waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, wakajazwa na nguvu, ari na ushupavu wa kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia kwamba Kristo Yesu amefufuka, Habari Njema kwa watu wote wa Mataifa, kuanzia kwa mitume wenyewe.

Nguvu ya Kristo Mfufuka inawaimarisha wafuasi wake na kuwapatia ushuhuda wa maisha mapya. Yesu anawataka mashuhuda na vyombo vya matumaini; watu wanaotabasamu, wanafurahi na kupenda pasi na mipaka! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo ya Kristo kwa waja wake. Kumbe, Wakristo wanayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba wanawarejeshea watu matumaini ya maisha mapya na baraka. Hawapaswi kuwa ni watu wenye kutoa litania ya maombolezo, chuki na hasira, bali kwa kutambua kwamba baada ya usiku wa giza kuna siku mpya inayofumbatwa katika mwanga; na kwamba, hata mdhambi anayo nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu; chuki na uhasama unashindwa kwa njia upendo usiokuwa na mipaka.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuonya kwamba, kuna wakati hata Mitume wa Yesu iliwabidi kulipa gharama kubwa, kwa kuyamimina maisha yao, daima wakimtumainia Mwenyezi Mungu. Hawa ndio mashuhuda wa imani, matumani na mapendo kutoka Mashariki ya Kati. Ni Wakristo wasiokuwa na mawaa ndani mwao, kwani wamebahatika kupewa neema ya kukumbatia ufufuko wa Kristo wanaoendelea kuutumainia. Mashuhuda wa imani wa nyakati zote, wamekuwa ni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake! Ukosefu wa haki msingi za kijamii si hatima ya maisha ya mwanadamu.

Kwa njia ya Kristo Mfufuka, Wakristo wanaweza kuendelea kutumainia, daima wakitembea na Kristo Yesu, bega kwa bega pasi na woga usiokuwa na mashiko. Kutokana na mwelekeo kama huu, Wakristo si rahisi sana kuweza kupokelewa na watu wengine. Mtume Paulo anamhimiza Timotheo kupiga vita kiaminifu kwa ajili Injili kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu hakuwapatia Roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Hata pale wanapoanguka, wale na ujasiri wa kusimama tena na kusonga mbele.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni anakaza kusema, hii inatokana na ukweli kwamba, Mkristo ni mmisionari wa matumaini, kwa njia ya neema ya Kristo Yesu, kwani mbegu ikianguka ardhini, itaoza na kutoa matunda yake. Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa mfano wa maisha yake, awasaidie vijana kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; imani na matumaini katika kupambana na changamoto za maisha na awasaidie wanandoa wapya kujenga familia katika msingi wa upendo.

Baba Mtakatifu akizungumza na mahujaji kutoka Misri, amekumbuka kwa namna ya pekee, hija yake ya kitume nchini mwao, bado anaendelea kuhifadhi moyoni mwake ukarimu kutoka katika Nchi ambayo Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilipata hifadhi. Msiri ni asili ya: Manabii, Watakatifu, wafiadini na watu wa haki; ni mahali ambapo historia na tamaduni zinakutana na kubusiana. Mwenyezi Mungu awalinde na kuwakinga dhidi ya mwovu shetani na vitendo vyote vya kigaidi! Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kusali Rozari kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuomba msamaha ili kukumbatia huruma na upendo wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

04/10/2017 14:12