2017-10-03 13:51:00

Papa Francisko: waamini tafuteni wasaa wa kutafakari upendo wa Kristo


Yesu katika Injili ya leo, anakata shauri kuelekea Yerusalemu ambako atakumbana na Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na hatimaye, ufufuko wake, hapo atakapoinuliwa juu! Yesu alijizatiti kweli kweli kuhakikisha kwamba, anatekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni kwa kujisadaka Msalabani ili kuweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Yesu akiwa njiani kuelekea mjini Yerusalemu, anawafunulia wafuasi wake siri kubwa iliyokuwa imefichika katika maisha na utume wake.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 3 Oktoba 2017. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliomba mara moja tu kwa Baba yake wa mbinguni kumwepushia kikombe cha mateso, lakini ikiwa kama anapenda mapenzi yake yatimizwe! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Yesu alisali sala hii alipokuwa pale Bustanini Getsemani. Utii pasi na shuruti ndio ambao Mwenyezi Mungu anautaka kutoka kwa waja wake kama Yesu alivyoamua na kujizatiti kuyatekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, sehemu hii ya Injili inamwonesha Kristo Yesu akijinyenyekesha, kielelezo makini kwa wafuasi wake, kinachonesha hija ya maisha ya kiroho si tu kwa ajili ya kuteswa na kufa Msalabani, bali kuliendea Fumbo la Kifo kwa unyenyekevu sana. Katika safari ya Kristo Yesu, kuelekea Yerusalemu; kwenye Fumbo la Pasaka, Mitume walikuwa wametangulia mbele ili kumwandalia mahali atakapopita ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Wakati mwingine anasema Baba Mtakatifu, Mitume wa Yesu hawakufahamu au hawakupenda kujitaabisha kufahamu kile kilichokuwa kinatokea katika maisha ya Kristo Yesu, walishikwa na woga na walitapanya mawazo yao, ili wasilikumbuke Fumbo la Msalaba! Lakini, Yesu alijizatiti peke yake na kuelekea Yerusalemu ili kukabiliana na Fumbo la Kifo na wala hakubadilisha mawazo! Maandiko Matakatifu yanaeleza kwamba, Yesu alipokuwa Bustanini Getsmane, wakati wa mateso yake, alifarijiwa na Malaika! Mitume walitokomea gizani na Petro, Mtume akamkana mara tatu na Yuda Iskarioti akamsaliti kwa vipande thelathini vya fedha.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujitaabisha kwa kutafuta muda na fursa ya kuingia katika undani wa maisha, ili kumtafakari Kristo Yesu, aliyewapenda watu wake, akawapenda upeo! Yesu aliyethubutu kutembea peke yake, kulielekea Fumbo la Msalaba. Inasikitisha kuona kwamba, waamini wana mambo mengi yanayowasumbua katika maisha yao, lakini hawana hata muda wa kukaa na kutafakari kidogo kuhusu upendo wa Kristo katika maisha yao! Kristo Yesu anaonesha fadhila ya uvumilivu kama binadamu na Mungu.  Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo; anavumilia kiasi hata cha kumwondolea mja wake dhambi na mapumgufu yake ya kibinadamu. Waamini wana wajibu wa kumshukuru Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusadaka kidogo muda wao ili kukaa mbele ya Msalaba na kutafakari kuhusu uamuzi wa Yesu kwenda Yerusalemu ili kukabiliana na Fumbo la Pasaka na kumwomba ujasiri na neema ya kumfuasa kwa karibu zaidi katika maisha ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.