2017-10-03 15:19:00

Mchango wa Kanisa katika kukuza Sinema kama njia ya mawasiliano


Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican, tarehe 2 Oktoba 2017 amezindua Onesho la Picha za Mababa Watakatifu wa Kufikirika katika maonesho ya Sinema huko kwenye Mkoa wa Lombardia, Kaskazini mwa Italia. Hili ni onesho ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican, Wizara ya Mali asili, utamaduni na utalii, Jimbo kuu la Milano pamoja na taasisi kadhaa za sinema na maonesha ya sanaa. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali na Kanisa kutoka mkoani Lombardia. Katika hotuba yake ya uzinduzi wa onesho hili, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, amekazia kuhusu umuhimu wa sinema kama chombo kinachomwezesha mtazamaji kupanua wigo wa uelewa wake! Anasema, sinema ni zawadi kubwa kwa binadamu lakini inawajibisha sana na kwamba, ni tukio linalowawezesha wahusika kujisikia kuwa karibu sana na jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 50 ya Upashanaji habari ulimwenguni sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu alisema, huu ulikuwa ni muda muafaka wa kutafakari kuhusu mawasiliano na huruma. Kimsingi, Kanisa likiwa limeungana na Kristo Yesu, umwilisho wa huruma ya Mungu linaalikwa kwa namna ya pekee kumwilisha huruma kwa uwepo na matendo. Kanisa liwe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu inayojionesha kwa namna ya pekee katika upendo, wema na huruma ya Mungu kwa wote.

Upendo kwa asili ni mawasiliano yanayojielekeza katika kuwashirikisha wengine na wala si kujifungia katika ubinafsi. Ikiwa kweli waamini watakuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, mawasiliano yao yatakuwa ni chombo kinachobeba nguvu ya Mungu. Monsinyo Dario Edoardo Viganò anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, amebainisha mambo msingi katika mawasiliano ya kijamii, kama zawadi inayowajibisha, inayojenga uhusiano wa karibu na kuwafanya watu kukutana na huruma ya Mungu.

Tema ya mawasiliano ni kati ya changamoto ambazo zimefanyiwa kazi na Mama Kanisa katika maisha na utume wake, kiasi hata cha kujenga uhusiano wa karibu kati ya Mababa Watakatifu na Sinema, tangu wakati wa Papa Leo XIII, onesho la Sinema lilipokuwa linaingia katika macho ya watu. Tangu wakati huo, Kanisa limeguswa sana na wazo la sinema kwani lilikuwa linagusa moja kwa moja kwenye dhamiri za watu, kuzuia hisia na hata kugusa sakafu ya maisha ya watu. Papa Pio XI akaanza kunusa harufu ya matatizo ya kisiasa na kijamii yaliyokuwa yanafumbatwa katika Sinema pamoja na athari zake katika maadili na utu wema. Sinema ikaanza kutumika kama chombo cha propaganda za kisiasa.

Papa Pio XI katika Waraka wake wa kitume, “Vigilanti cura” wa Mwaka 1936 aliwataka waamini wa Kanisa Katoliki kushiriki kikamilifu katika chombo hiki kipya cha mawasiliano ya kijamii na hivyo kuchangia katika upembuzi yakinifu kwa picha zilizokuwa zinarushwa kwenye majumba ya sinema. Papa Pio XII alikazia kwa namna ya pekee kabisa, uwajibikaji wa watengenezaji na watazamaji wa sinema; ili kuwasaidia waamini kupata mafundisho makuu ya Kanisa sanjari na kusaidia kufunda dhamiri zao, ili hatimaye, waweze kujikita katika maadili na utu wema. Kunako Mwaka 1959 Mtakatifu Yohane XXIII akaanzisha kitengo cha Sinema mjini Vatican na huo ukawa ni mwanzo wa Sinema zilizojikita katika Injili!

Monsinyo Dario Edoardo Viganò anakaza kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Sinema kwa kukutana na kuzungumza na wacheza sinema wenyewe; akakazia umuhimu wa watazamaji kuwajibika barabara na kile walichokuwa wanakitazama, kwani huu ulikuwa ni utamaduni mpya ulioanzishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, kwani lugha yake ilikuwa tayari ni sehemu ya utamaduni mamboleo.

Katika mchakato wa mageuzi haya, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, alikiri dhamana na mchango wa sinema katika kukuza na kudumisha uzuri unaobubujika kutoka katika kipaji cha ubunifu ambacho Mwenyezi Mungu amemkiria mwanadamu! Sinema ilikuwa na uwezo wa kugusa sakafu ya maisha ya binadamu, hisia na unyeti wake, kiasi hata cha kuibua ndoto na matumaini ya kupanua wigo wa uelewa na dhamana ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, anakazia njia za mawasiliano ya jamii, kusaidia mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wacheza sinema maarufu wa nyakati hizi na kwamba, ni kiongozi anayependa kuangalia sinema kwani hii ni katekesi ya kweli katika ubinadamu. Sinema, kimsingi inasaidia kutunza, kufariji, kuganga na kuponya, kusindikiza na hatimaye, kusherehekea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.