2017-10-02 09:04:00

Maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika: Neno, Ekaristi na Maskini!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili, tarehe 1 Oktoba 2017 baada ya kukutana na kuzungumza na ulimwengu wa wasomi, Jimbo kuu la Bologna, ambako amekazia: haki ya utamaduni, haki ya matumaini na haki ya amani; Jioni, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, ili kufunga rasmi, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kijimbo kwa kukazia umuhimu wa Neno la Mungu linalowasha moto wa mapendo katika nyoyo za watu, ili kuwawezesha kujisikia kwamba, wanapendwa na kufarijiwa na Mwenyezi Mungu.

Neno la Mungu ni sawa na upanga wenye makali kuwili, kwani linapenyeza katika undani wa moyo wa mwanadamu na kufunua siri zilizofichika katika sakafu ya maisha ya mwanadamu pamoja na kinzani zake. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXVI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa imekuwa ni fursa ya kutafakari mifano ya wale watoto wawili waliotoa majibu yaliyomwacha Baba yao akiwa ameshika tama!

Mmoja aliombwa na Baba yake kwenda shambani, akakataa kwa macho makavu kutokana na uvivu, lakini baadaye akatubu na kwenda kutekeleza mapenzi ya Baba yake, akashinda tabia ya uvivu kwa kufanya kazi. Kijana wa pili alikubali kwenda shambani, lakini jibu lake lilikuwa ni la kinafiki, kwani hakwenda shambani kutekeleza mapenzi ya Baba yake. Ni kijana aliyejikita katika maneno matupu bila matendo licha ya kutambua umuhimu wa kazi kama utilimifu wa maisha ya binadamu! Lakini akabaki “kichwa maji”. Huu ndio unafiki unaoweza kuwakumba waamini katika safari ya maisha yao, kwa kushindwa kusikiliza sauti ya Mungu inayozungumza nao kutoka katika undani wa maisha yao, yaani kwenye dhamiri nyofu.

Kwa vile binadamu ni mdhambi, si rahisi sana kwake kusema kwa maneno na kutekeleza kwa matendo! Lakini, hapa Baba Mtakatifu anasema, waamini wanapewa uwezo wa kusuka au kunyoa! Kuamua kuwa wadhambi wanaotembea huku wakimsikiliza Mwenyezi Mungu kwa dhati, na mara wanapoanguka dhambini, wako tayari kusimama tena kwa toba na wongofu wa ndani, tayari kuomba msamaha na kukumbatia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kama alivyofanya yule mtoto wa kwanza, mvivu, lakini, msikivu, mwenye moyo wa toba! Pili, waamini wanaweza kuamua kuendelea kuwa wadhambi, waliobweteka, ambao wako tayari kuhalalisha matendo yao kwa maneno matupu ambayo hayawezi kamwe kuvunja mfupa!

Hawa ni watu geugeu kama kinyonga au bendera fuata upepo! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mfano huu ulitolewa na Kristo Yesu kwa viongozi wa dini wa nyakati zake, waliokuwa na maisha ya kinafiki, maisha ya undumila kuwili! Ni watu waliokuwa na ufahamu mkubwa wa mambo ya kidini, wakayafafanua kwa kina na mapana, kiasi cha kuwaacha wasikilizaji wao wakiwa wameshika tama! Lakini, kwa bahati mbaya hawakuwa na fadhila ya unyenyekevu wa kusikiliza kwa makini, ujasiri wa kujiuliza maswali na nguvu ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Hapa, Kristo Yesu, anaonesha ukali wake kwa kuwaambia kwamba, hata watoza ushuru watawatangulia mbele kwenye Ufalme wa Mungu. Hili ni kalipio kali sana kwa kutambua kwamba, watoza ushuru walikuwa ni wala rushwa, mafisadi na wasaliti wa nchi!

Viongozi hawa walijikinai kuwa ni watu wema na watakatifu katika mawazo na maneno yao, lakini matendo yao yalikuwa ni kinyume kabisa, kiasi cha kusahau kwamba maisha kadiri ya Mwenyezi Mungu ni safari inayojikita katika unyenyekevu kwa kujiweka wazi mbele ya Mungu, toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza tena maisha mapya kwa neema ya Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maisha ya Mkristo ni safari inayojikita katika unyenyekevu kwa kutambua umuhimu wa ujenzi wa mahusiano mema na Mwenyezi Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kutambua umaskini na unyonge wake, ili kuvuka vikwazo vya unafiki, maisha ya undumila kuwili; utekelezaji wa sheria usiozingatia huruma na upendo, matokeo yake ni ukatili unaowatenganisha viongozi wa Kanisa na waamini wao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wazo kuu ni toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuachana na ukaidi wake wa kusema hapana kwa Mungu na kuanza kukubali kutekeleza mapenzi yake kwa ndiyo ya kweli! Kwa kuachana  na dhambi pamoja na nafasi zake, ili kuambata upendo wa Mungu katika maisha! Mwenyezi Mungu anamfunulia mwamini utashi wake kwa njia ya dhamiri nyofu, changamoto kwa kila mwamini kutambua kwamba, ni mdhambi anayepaswa kutubu na kumwongokea Mungu, vinginevyo, atajikuta kuwa ni mdhambi ambaye ni mnafiki! Mwenyezi Mungu anawataka watu wenye moyo mweupe na wala si wale wanaonekana wenye haki kwa nje, lakini kwa  ndani, “ni makaburi yanayonuka”!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kudumisha mahusiano mema kati ya watoto na wazazi wao; kwani kuna mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo ambamo watoto wanadai uhuru zaidi kutoka kwa wazazi wao, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita! Kuna dalili za kuasi kwa vijana wa kizazi kipya! Kumbe, kwa sasa kuna haja ya kujenga utamaduni wa kukutana na kusikilizana kwa dhati, ili kuleta uwiano bora zaidi katika maisha! Huu ndio mwelekeo mpya unaopaswa kuvaliwa njuga ndani ya: Familia, Kanisa na Jamii katika ujumla wake, ili kujenga utamaduni wa majadiliano, ili kutafuta njia za kuweza kutembea kwa pamoja.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mambo makuu matatu yanaweza kuwasaidia waamini kutekeleza dhamana hii kwa dhati kabisa! Kwanza ni Neno la Mungu ambalo ni dira na mwongozo wa maisha dhidi ya malimwengu;  Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Hapa ni mahali pa kukutana na Kanisa, kwa kushiriki chakula cha uzima wa milele, kinachowawezesha waamini kujitambua kwamba, ni wadhambi, lakini bado wanapendwa na Mwenyezi Mungu na hivyo wanapaswa kutamani hata wao kupenda kama anavyopenda Mungu, kama utambuzi wa waamini kuwa wao ni sehemu muhimu sana ya Kanisa kama ilivyotangazwa na kushuhudiwa katika maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kijimbo! Tatu, anasema Baba Mtakatifu ni mshikamano na maskini ambao hata leo hii, wanatindikiwa mahitaji muhimu katika maisha yao kama binadamu! Lakini, ikumbukwe kwamba, kuna hata maskini wanaokosa joto la upendo! Hao ndio ambao Kristo Yesu, amejinyenyekesha kiasi hata cha kuutwaa ubinadamu, na kuwa kama mtumwa! Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashirikishana mkate wa uzima wa milele, bila kusahau kuwahudumia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha! Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Maskini ni chachu ya maisha ya waamini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.