2017-09-30 10:39:00

Tafakari ya Neno la Mungu: Zawadi ya wokovu na uhuru wa binadamu!


Kanisa ni chombo cha Kristo na ni Sakramenti ya wokovu wa watu wote, ambayo kwayo Kristo Yesu anadhihirisha na kutekeleza upendo wa Mungu kwa ajili ya watu; ni alama ya ushirika kati ya Mungu na binadamu. Kristo Yesu ni ishara ya utii wa hali ya juu kabisa kwa Baba yake wa mbinguni uliofunuliwa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Kwa njia ya utii na unyenyekevu uliooneshwa na Yesu katika Familia Takatifu, anaonesha utakatifu katika maisha ya kila siku ndani ya familia sanjari na utekelezaji wa dhamana na majukumu ya kila mwamini katika maisha yake.

Mama Kanisa anatukumbusha kwamba, uhuru wa kweli unakwenda sanjari na wajibu. Kumbe, kuna haja kwa waamini kulea na kukuza dhamiri nyofu itakayowawezesha kufanya maamuzi katika ukweli na wema. Uhuru hupata ukamilifu wake unapoelekezwa kwa Mwenyezi Mungu, ustawi, mafao na maendeleo ya jirani! Uhuru ndiyo msingi wa sifa njema au lawama; mastahili au shutuma! Katika mambo yote haya, ubinadamu wetu unaguswa na kutikiswa sana kama inavyojionesha katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXVI ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ndiyo maana, Mama Kanisa anatualika daima: kutubu na kumwongokea Mungu ili kuwaza na kutenda kadiri ya utashi na mapenzi yake! Tema inayoongoza tafakari yetu ni zawadi ya wokovu na uhuru wa binadamu!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXVI ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa inaonesha kwa karibu sana uwajibikaji wa mtu binafsi katika kupokea na kukumbatia zawadi ya wokovu inayotolewa na Mwenyezi Mungu na kwamba, hili ni tunda la juhudi za binadamu kuipokea zawadi hii inayotolewa kwa wote. Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa anasema, Mwenyezi Mungu amateuumba kwa sura na mfano wake bila ridhaa yetu, lakini, hauwezi kutukomboa bila ridhaa na ushiriki wetu! Kumbe, wokovu ni juhudi za mtu binafsi.

Alama ya ushirikiano huu wa dhati katika mchakato mzima wa ukombozi ni toba na wongofu wa ndani; unaojikita katika dhamiri nyofu, inayomwezesha mwamini kuchagua kwa uhuru zaidi kufuata jambo jema na kulitenda pamoja na kuachana na matendo maovu. Dhamiri nyofu ni mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake, kutoka katika undani wa maisha yao. Ikumbukwe kwamba, mwanadamu amekirimiwa uwezo wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo kuweza tena kuandika historia ya maisha yake kwa usahihi zaidi, kama ilivyojitokeza kwenye Somo la kwanza na katika Injili ya leo!

Kila mtu ana uwezo wa kuboresha historia ya maisha yake kiroho kwa kuwa mtu mwema zaidi. Nabii Ezekieli anawataka Waisraeli kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuacha njia zao mbaya. Rej. Ez. 18:20. Mwanadamu katika safari yake ya maisha hapa duniani, amekirimiwa na Mwenyezi Mungu nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili hatimaye, aweze kuokoka na kuambata huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tunaambiwa kwamba, haitoshi kuwa ni mtoto wa Abrahamu, Baba yetu wa imani; “haifui dafu” kuwa Mkristo kama katika safari ya maisha yako ya kiroho, utashindwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuonja msamaha na huruma yake isiyokuwa na mipaka.

Kuna watu wanadhani kwamba, wao wana haki kuliko wengine; wanapendelewa kuliko watu wengine wote duniani na matokeo yake ni kubweteka kwa kudhani kwamba, wokovu wa Mungu unakuja kama “maji kwa glasi”. Wapagani, watu wa kuja, wadhambi na watu wa Mataifa wanaotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu wanajaliwa fursa ya kuingia na kushiriki katika Ufalme wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, wokovu ni zawadi ya Mungu kwa watu wote na wala si haki ya mtu! Mbele ya Mwenyezi Mungu, watu wote wanaweza kuhesabiwa haki kutokana na matendo yao mema! Uhuru binafsi ukitumiwa kwa hekima na busara una nguvu sana. Mwenyezi Mungu anatarajia kuona upendo wa dhati unaobubujika kutoka katika uhuru wa mtu! Kumbe, ni wajibu wa kila mmoja mtu kutumia vyema uhuru wake kwa kuchagua kutenda mema, ili kupata wokovu! Uhuru wa binadamu ni muhimu sana katika mchakato wa kumwilisha upendo na utashi wa Mungu katika matendo. Tunakumbushwa kwamba, si kila mtu asemaye Bwana! Bwana! Ataweza kuingia katika Ufalme wa Mungu, bali yule anayetenda kwa dhati mapenzi ya Mungu.

Tunaitwa kama Wakristo kutenda kazi katika shamba la Kristo, yaani Kanisa kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na adili. Hii ndiyo ile “Ndiyo” yetu tuliyoitoa wakati wa Ubatizo. Dhambi na ubaya wa moyo, vinampeleka mbali mwamini na wokovu wa Mungu. Ndiyo maana tunahimizwa kutimiza mapenzi ya Mungu kwa matendo yanayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu kama Kristo Yesu alivyofanya katika maisha yake. Tunahimizwa kuwa na huruma, umoja na mapendo pamoja na kuachana na ubinafsi, choyo na kutaka kujipatia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Utii wa Yesu kama anavyotufundisha Paulo Mtume katika somo la pili, utusaidie kuwa ni mashuhuda wa Injili ya huduma inayomwilishwa katika uhuru kamili, upendo wa dhatiutii, toba na wongofu wa ndani, kwa ajili ya kumpatia Mwenyezi Mungu sifa na mwanadamu kukirimiwa zawadi ya wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.