2017-09-28 10:33:00

Papa Francisko azindua kampeni ya "Shiriki safari" na wahamiaji


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Septemba 2017 amezindua Kampeni ya Kimataifa ya Ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi inayoratibiwa na kusimamiwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis inayoongozwa na kauli mbiu “Share the journey” yaani “Shiriki safari” . Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha wema na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, kwa kushirikiana na mashirika mbali mbali ya misaada ya Kanisa Katoliki sanjari na vyama vya kiraia vinavyojielekeza katika huduma ya upendo kwa wahamiaji na wakimbizi.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa mstari wa mbele kushuhudia ukarimu ambao ni nguzo msingi katika maisha na utume wa Mama Kanisa anayewapokea na kuwakumbatia wote ili kuwaonjesha faraja na huruma ya Mungu wakimbizi na wahamiaji katika safari yao ya pamoja. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kushiriki safari hii ya matumaini inayomsukuma mtu kuacha nyumba, nchi, tamaduni na hata wakati mwingine, ndugu na jamaa ili kwenda kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kwake binafsi na kwa familia na watu wanaomtegemea.

Huu pia ni msukumo unaotoka katika undani wa wale wanaoonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji katika maeneo yao na hivyo kujenga madaraja ya watu kukutana, kufahamiana, kujadiliana na kusaidiana kwa hali na mali. Haya matumaini ni chachu ya pekee inayowasukuma waamini kushiriki safari hii pasi na woga wala makunyanzi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, wakimbizi na wahamiaji, wengi wao ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita na ghasia; ni waathirika wa majanga asilia kutokana na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; ni watu wanaoteseka na umaskini pamoja na ukosefu wa fursa za ajira kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko katika uzinduzi wa kampeni hii, amewashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, changamoto kwa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, kuwa mstari wa mbele katika kuwapokea, kuwakirimia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Caritas Internationalis, amewakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, umuhimu wa kuwapokea na kuwakirimia wageni, wakimbizi na wahamiaji kwani kwa kufanya hivyo wanatekeleza amri na maagizo ya Kristo mwenyewe anayejionesha kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Caritas Internationalis katika maisha na utume wake, inapenda kutekeleza kwa dhati kabisa Injili ya upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaohitaji huruma na faraja ya Mama Kanisa katika shida na mahangaiko yao ya ndani! Mchakato wa huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu, dhana inayosimamiwa na kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa vitendo ni mwaliko wa kusimama kidete, kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Nyuma ya idadi ya takwimu za wakimbizi na wahamiaji duniani, kuna watu halisi wenye historia, matumaini na changamoto zao katika maisha.

Kardinali Luis Antonio Tagle, anaendelea kufafanua kwamba, kuna mambo ambayo yamepelekea wimbi kuwa la wakimbizi na wahamiaji kuwa ni changamoto tete kwa Jumuiya ya Kimataifa: biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, utumwa mamboleo na mifumo yake yote; biashara haramu ya silaha duniani na athari zake kwa watu na mali zao; vita, ghasia na mipasuko ya kidini, kijamii, kisiasa na kikabila, bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi, Changamoto ya mambo yote haya ni kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Mama Kanisa anatekeleza yote haya mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu wa binadamu na mahitaji yake msingi. Kampeni hii inaweza kufanikiwa ikiwa kama waamini watafanya toba, wongofu wa ndani pamoja na mageuzi ya fikra, badala ya kuwaona wakimbizi na wahamiaji kuwa ni watu hatari sana katika maisha na kuanza kuwa na mwelekeo chanya, unao wathamini na kuwajali katika shida na mahangaiko yao ya ndani.

Dr. Michel Roy, Katibu mkuu wa Caritas Internationalis, amebainisha matukio makuu yatakayotekelezwa katika mchakato wa kushiriki safari ya wakimbizi na wahamiaji mara baada ya kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kuanzia mwezi Februari 2018 na kuendelea Caritas Internationalis itaragibisha majadiliano ya kina na serikali mbali mbali duniani, ili hatimaye, kuandaa muswada wa Kimataifa kuhusu Usalama wa wahamiaji na wakimbizi duniani.

Tarehe 20 Juni 2018 ni juma la utekelezaji wa sera na mikakati ya Caritas Internationalis kwa vitendo, hasa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018. Mwezi Septemba 2018, Caritas Internationalis itahamishia mchakato wa uragibishaji wa kampeni hii kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ili kuwza kupitisha miswada miwili ya kimataifa kwa ajili ya ulinzi, usalama na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji duniani. Mwishoni mwa mwaka 2019, Caritas Internationalis itakuwa inahitmisha kampeni hii ya Shiriki safari na wakimbizi pamoja na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.