2017-09-27 13:54:00

Utii wa kweli unafumbatwa katika: uhuru, upendo na matendo!


Mhubiri mmoja alitoa noti ya dola mia moja ya kimarekani na kuwauliza hadhira yake. ‘Nani anaitaka hii noti’. Basi wote waliokuwa wanamsikiliza wakanyanyua mikono juu, akauliza tena mara ya pili na mara ya tatu jibu likawa ni lile lile. Lakini kijana mmoja mdogo akajongea mbele na mhubiri yule akampatia ile noti. Mwaka mmoja uliopita Kanisa liliadhimisha Jubilei la Huruma ya Mungu. Ni kipindi cha neema ambacho sisi kama Wanakanisa tulipata fursa ya kuangaziwa na uso wa huruma ya Mungu. Fursa hii haikutujia tu bwerere bila kujishughulisha kama wengi walivyojidanganya bali ilitaka kila mmoja kwa nafasi yake kuijongea hiyo huruma ya Mungu. Hapo tulikumbushwa kwamba kukaa ndani ya maji si uhakika wa kutakata. Kila anayetaka kuwa safi anapaswa kujitakasa kwa kujisafisha na maji.

Masomo ya Dominika hii yanatuelezea juu ya huruma ya Mungu. Hii ni hamu ya kila mmoja kwani sote tu wadhambi. Hamu hii haipaswi kubaki katika mioyo yetu tu bali tunaalikwa kuchukua hatua ili kuipata hiyo huruma yake. Nabii Ezekieli anatuambia katika somo la kwanza kuwa “Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha njia yake na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa… bali mwovu akitubu “na kutenda  yaliyo halali na haki, ataponya roho yake nayo itakuwa hai”. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inatuwekea mbele yetu uchaguzi wa maisha: kuchagua haki ili kuishi au kuchagua uovu ili kufa. Mwanadamu anahukumiwa kadiri ya matendo yake na si kwa maneno tu. Mwenye haki mbele ya watu kwa maneno lakini moyoni anaighairi njia ya haki ataangukia kufa tu. Dawa ni kufanya toba ya kweli na kuishi.

Sehemu ya Maandiko inayotangulia Somo hili inatuhakikishia huruma ya Mungu. Kwamba Yeye afurahii kufa kwake mwovu. Daima anamwalika kuiacha njia yake mbaya. (Rej Ezek 18:23) Daima yupo mlango anagonga anataka umfungulie. Pamoja na kwamba Mungu ameweka uchaguzi na pamoja na ukweli kwamba Yeye anaheshimu uhuru wa utashi wa mtu lakini bado anaonesha hamu ya moyo wake, yaani kuifuata njia ya haki na kumrudia Yeye. Hapa ndipo tunaona kina cha Upendo wa Mungu.

Upendo una hulka ya kutafuta kuunganika na kile kinachopendwa. Mungu anatupenda sisi watoto wake. Siku zote yupo kwa ajili ya kututafuta, kututoa dhambini ili kujiunga naye. Dhambi inakinzana na upendo wa Mungu bali njia ya haki inaustawisha upendo wake kwetu, naye anakuja kwetu na kukaa pamoja nasi.

Kumrudia Mungu ni tendo la moyoni na si tendo la mdomoni tu. Toba ya kweli inajidhihirisha katika kugeuza mwenendo wako kwa vitendo na si kwa maneno. Mfano wa vijana wawili katika Injili unatupatia nafasi ya kutafakari namna ya toba yetu mbele ya Mungu. Leo tunaulizwa juu ya viapo vyetu mbele ya Mungu. Ni vipi viapo hivyo vinapingana na matendo yetu halisia? Tunamwambia Mungu kuwa tunakupenda na tunaiacha njia za dhambi lakini kwa ndani tunaendelea kuifurahia dhambi na kutokuwa tayari kuacha kabisa uovu wetu. Tunajionesha kwenda katika ibada na hata wakati mwingine kujikinai tu wakarimu lakini ndani tumejawa na ukinzani wa upendo wa Mungu na tunatenda kinyume na ahadi yetu ya upendo kwa Mungu.

Tunaweza kuona pia utii huu tunaoweza kuubatiza utii wa maneno kwa Mungu katika viapo vyetu mbalimbali tumfanyiavyo. Katika maisha ya ndoa tuliahidi kuwa waaminifu, kusaidiana, kutotengana iwe kwa sababu yeyote ile na tuliahidi hivyo mbele ya Mungu lakini maisha halisi yanaakisi tofauti. Tunashabikia nyumba ndogo au vidumu, hatujali familia zetu na hakuna utii wala uvumilivu wa kweli. Wengine katika maisha ya wakfu kama Watawa au Makasisi wameweka ahadi ya kumtumikia Mungu na kujitoa kwa moyo wote na hata ahadi ya usafi wa moyo lakini maisha ya kawaida ni tofauti. Wengi awapo tayari kuhudumia kwa moyo kundi wanalokabidhiwa na wengine kukurupusha viapo vyao na kuwa kikwazo kwa kundi. Hawa nao ni sawa na hawa wasemao ndiyo lakini moyoni wanasema hapana.

Tukirudi katika tendo la toba tunapata njia ya kupitia ili toba yetu kuwa na tija katika safari yetu ya ukombozi. Mama Kanisa Mtakatifu sana anatupatia kama nyenzo ya msaada katika kuijongea Sakramenti ya Upatanisho. Tujikumbushe tena leo hii hatua hizo kwani pengine wengi wetu tumeshazisahau kwani ni muda mrefu umepita tangu kufanya katekesi kwa maandalizi ya kuipokea Sakramenti hii au pengine hatutilii maanani tu umuhimu wake na matokeo yake wengi wetu tunajikinai kuwa tupo safi na tumeungama dhambi zetu lakini hakuna matunda katika maisha yetu ya kiroho. Sakramenti ya Upatanisho ni safari ya kuelekea wokovu. Ni tendo ambalo linapaswa kuonesha kupiga hatua katika kuelekea utakatifu.

Hatua ya kwanza inamtaka mmoja kujikubali kuwa yu mdhambi na kuzitambua waziwazi dhambi zake. Hatua hii inampeleka katika kujuta au kuona uchungu kwa makosa yake. Haitoshi tu kutambua kuwa ni mdhambi bali upate uchungu na hivyo utaweza kuingia katika hatua ya kukusudia kuachana na hali hiyo ya dhambi. Kwa kuumia mithili ya kidonda cha kawaida mwilini kutamfanya mmoja kutengeneza miundombinu ya kuepuka njia hiyo. Baada ya hatua hizi tatu mmoja sasa anapaswa kupiga hatua na kumwendea Mungu ili kutubu dhambi zake na kuomba ondoleo na dhambi na hatua ya mwisho ni kufanya matendo ambayo ni malipizi kwa madhara uliyosababisha kwa uovu wako.

Matendo yote haya katika ujumla wake yanatudai paji la unyenyekevu. Unyenyekevu ndiyo unatuwezesha kuitambua nafasi yetu mbele ya Mungu, kuitambua huruma yake, kuutambua ukuu wake na umuhimu wake katika maisha yetu. Unyenyekevu ndiyo unatupatia Mungu na kutufanya kutembea katika ukweli lakini kiburi kinatufungia na kujiona tupo bora na wasafi zaidi. Mtume Paulo anatuambia “msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake”. Kukosekana kwa unyenyekevu mara zote hutuvuta katika kutenda si katika ukweli bali kutenda mambo kadiri ya vionjo na majigambo ya kidunia. Kwa bahati mbaya sana mambo haya huingia hata katika mambo matakatifu.

Ni fursa kwetu leo hii kuangalia imani yangu. Ni namna gani ninakimbilia huruma ya Mungu: je, ni kwa toba kutoka moyoni au kwa ajili ya kuonekana mbele ya wengine? Wahenga wanatuambia kuwa “tusiiache mbachao kwa msala upitao”. Ni wakati wa kuacha kutenda kwa ajili ya kuonekana bali tutende kwa ajili ya kumpatia Mungu utukufu. Maneno na matendo yetu ya kwamba tunampenda Mungu yabubujike kutoka ndani ya mitima yetu. Tuzitumie vyema nafasi za neema zinazowekwa mbele yetu ili kujitakasa. Tukumbuke kwamba si kwamba ukikaa ndani ya maji ndiyo hakika umetakata.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.