2017-09-27 11:08:00

Mchango wa Vatican katika masuala changamani ya Jumuiya ya Kimataifa!


Vatican inapenda kupembua matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza katika Jumuiya ya Kimataifa kwa mwanga wa Injili, Mafundisho Jamii ya Kanisa; mintarafu dhamana na utume wa Kanisa kwa familia ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pasi na ubaguzi. Vatican inapania kuendeleza uhuru wa kidini na kuabudu; utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazofumbatwa kwa namna ya pekee katika Injili ya amani na utulivu, chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu ya binadamu.

Pale ambapo walimwengu wamegeuzia kisogo ushauri uliotolewa na Mababa wa Kanisa, Jumuiya ya Kimataifa imejikuta ikitumbukia katika vita ambayo imesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao kama ilivyojitokeza katika Vita Kuu ya Kwanza ya dunia sanjari na Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Walimwengu bado hawajajifunza kinagaubaga madhara ya vita duniani. Vatican katika diplomasia yake inakazia zaidi majadiliano katika ukweli na uwazi, changamoto ambayo imevaliwa njuga kuanzia na Papa Pio XII, Leo XIII na hata Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, kwa kushirikiana na wasaidizi wake katika sehemu mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Mababa wa Kanisa wanasema, vita ni balaa na njia isiyofaa kutatua na kumaliza matatizo na migogoro inayozuka kati ya mataifa, ni mauaji ya kinyama yasiyo ya lazima. Ikumbukwe kwamba, hakuna kinachoweza kupotea kwa kudumisha amani, lakini yote yanaweza kupotea wakati wa vita. Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu kutatua matatizo na changamoto zake. Jambo la kusitikisha anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kuona kwamba, Mataifa yanaendelea  kuwekeza katika biashara ya silaha na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia ni kwa ajili ya mafao ya baadhi ya wawekezaji wakuu. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na ujasiri wa amani ili kukataa kishawishi cha vita; kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga jamii inayofumbatwa katika misingi ya udugu, haki na amani!

Haya ni kati ya mambo makuu yaliyochambuliwa hivi karibuni na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, wakati alipokuwa anatoa hotuba yake kwenye Chuo Kikuu cha Fordham, huko New York, Marekani. Baba Mtakatifu Francisko katika  barua yake kwa “Chancellor” Angela Merkel wakati wa mkutano mkuu wa G20 huko Hamburg, Ujerumani, alikazia umuhimu wa kutenga muda, sera na mikakati ya kupambana na baa la umaskini duniani; kujenga umoja na mafungamano ya kimataifa badala ya kuendekeza misuguano na utengano, ili kutoa majadiliano katika ukweli na uwazi kushika mkondo wake.

Utu na mahitaji msingi ya binadamu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa. Mahusiano na mafungamano ya watu Kimataifa yanapaswa kufungamanishwa katika: haki, mshikamano na upendo kwamba, amani ni chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu ya binadamu. Mababa wa Kanisa wanawaalika wakristo kuhakikisha kwamba wanashiriki katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kuonesha uzalendo kwa tamaduni na nchi zao. Waamini wanaalikwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Sheria za kimataifa zifuatwe na kutekelezwa na wote na kwamba, amani ya kweli kama ilivyofafanulia na Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa kitume: “Pacem in terries” yaani “Amani duniani” inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu!

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni utajiri mkubwa katika utume wa Jumuiya ya Kimataifa, ikizingatiwa kwamba, mikataba na itifaki mbali mbali zinazopitishwa na Jumuiya ya Kimataifa zimekuwa hazitekelezeki kwa urahisi sana. Vatican imeendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwa kutia sahihi na kuridhia mikataba na itifaki mbali mbali za kimataifa!. Kanisa linapinga vita kama njia ya kupata suluhu ya kimataifa. Ujasiri wa amani, utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza katika medani za kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.