2017-09-26 10:52:00

Malezi makini katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia!


Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, Jumapili tareheĀ  24 Septemba 2017 imehitimisha mkutano wake wa mwaka, kwa kuendelea kujuzatiti kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kumshauri Baba Mtakatifu mbinu za kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazodhalilisha utu, heshima na makuzi yao kama binadamu! Wajumbe wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuwatia shime pasi na kukata tamaa kwamba, sasa ndani ya Kanisa hakutakuwepo tena na uvumilivu kwa wale wote watakaojihusisha na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kuendeleza mchakato wa utamaduni wa ulinzi, usalama, kanuni na maadili yanayotolewa na Mama Kanisa katika ujumla wake. Sr. Hermenedild Makoro, kwa niaba ya wajumbe, alimshukuru Baba Mtakatifu Francisko, kwa imani na matumaini aliyowaonesha wajumbe hawa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao. Katika mkutano huu, wajumbe wamesikiliza shuhuda za watu walionyanyaswa kijinsia; wakabainisha miongozo kwa ajili ya kuwalinda: watoto, vijana na watu wazima wanaoweza kutumbukizwa katika nyanyaso hizi kwenye Makanisa Mahalia.

Wajumbe wamekazia umuhimu wa elimu na malezi mintarafu ulinzi wa watoto wadogo. Mpango kazi kwa wakati huu ni kuendeleza mchakato wa uponyaji wa wahanga wa nyanyaso za kijinsia; habari na elimu pamoja na kuendelea kutekeleza sera endelevu za ulinzi wa watoto. Tume inaundwa na jopo na watu 15 kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kwa mara ya kwanza ilianza kutekeleza dhamana yake kunako mwaka 2014 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.