Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maendeleo

Kardinali Nzapailanga: CAR: Inataka kujizatiti katika elimu na afya!

Wananchi wamechoka kwa vita wanataka amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati. - AFP

26/09/2017 13:50

Kardinali Dieudonnè Nzapalainga, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anasema, hatima ya ustawi, maendeleo, amani na utulivu wa wananchi wa Afrika ya Kati iko mikononi mwao wenyewe! Jumuiya ya Kimataifa inaweza kusaidia katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na maridhiano, lakini wao wenyewe ndio wenye dhamana ya kuhakikisha kwamba, makubaliano haya yanatekelezwa kwa ukamilifu. Umefika wakati wa ujenzi wa utamaduni wa amani kwa kuwajengea watoto fursa ya kwenda shule ili kujifunza kusoma na kuandika, tayari kupambana na changamoto za maisha kwa sasa na kwa siku za baadaye, badala ya kuwabebesha silaha na kuwapeleka mstari wa mbele. Vijana wanapaswa kufundwa barabara ili kuwa raia wema, wazalendo na watu wanaowajibika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi zao kwa kutambua kwamba, hakuna njia ya mkato katika kutafuta na kupata mafanikio. Juhudi, maarifa na bidii ya kazi ni mambo msingi yanamwezesha mtu kupata mafanikio ya kweli.

Vijana wasikubali kutumiwa na wanasiasa uchwara kuvuruga amani, usalama na mafungamano ya kijamii kwa ajili ya mafao ya watu binafsi, daima wazingatie ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa  Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kardinali Dieudonnè Nzapalainga analishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ambalo limekubali kugharimia ujenzi wa shule 10 za msingi Jimbo kuu Bangui, ili kuwajengea watoto na vijana nafasi ya kupata elimu kwa ajili ya maendeleo yao na kuwatangazia Injili ya matumaini inayomwilishwa katika huduma ya upendo, changamoto iliyofanyiwa kazi na Mababa wa Afrika katika mkutano wa Caritas Africa uliohitimishwa hivi karibuni.

Kardinali Dieudonnè Nzapalainga katika mahojiano maalum na Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, SIR anasema, kipaumbele cha kwanza kwa wakati huu ni huduma makini na endelevu katika sekta ya elimu na afya; itakayowawezesha watoto na vijana kushirikiana kwa pamoja ili kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa; kwa kuthamini tofauti zao kama utajiri mkubwa unaopaswa kukumbatiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Changamoto za elimu, zitawasaidia wazazi na walezi kukutana mara kwa mara kwa ajili ya kutathmini maendeleo ya watoto wao na kwa njia hii watajifunza kujenga madaraja ya kukutana na kufahamiana.

Tayari mjini Bangui, kumeanzishwa Chuo cha Kilimo kinachotoa: ujuzi, elimu na maarifa ya kilimo cha kisasa kinachopania kuwakwamua wakulima nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kutoka katika kilimo cha kujikimu na kuanza kuwekeza katika kilimo cha mazao ya biashara ili kuongeza pato lao litakalosaidia mchakato wa maboresho ya maisha. Sanjari na ujenzi wa Chuo cha Kilimo, Bangui inaendelea pia kuboresha sekta ya afya, ili kuwajengea watu uhakika wa usalama wa afya na maisha, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Maboresho ya huduma ya afya yanalenga pia kuwaondolea watu imani za kishirikina ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya watu na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Bangui inapania kuboresha maisha ya watu wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati linaendelea kushirikiana kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya mbinu mkakati wa majadiliano ya kidini yanayopania kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka ni mambo yanayowapelekea baadhi ya wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuendelea kupambana msituni na kusahau kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu!

Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa huduma endelevu ya binadamu linataka kuwajengea vijana uwezo, ili kuweza kupambana na changamoto za maisha yao kwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano. Kamwe, Kanisa halitakubali tena nchi kugeuzwa kuwa ni kichaka cha majambazi na uwanja wa vita na mapambano. Wanchi wanapaswa kutambua kwamba, hatima ya maisha, ustawi na maendeleo iko mikononi mwao! Majadiliano ya kidini na kiekumene yanapania pamoja na mambo mengine kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Kardinali Dieudonnè Nzapalainga anakaza kusema kwamba, wananchi wengi hawaridhishwi na utendaji kazi wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Umoja wa Mataifa, MINUSCA. Baadhi yao wanashtumiwa kwa kujihusisha na vitendo vya nyanyaso za kijinsi dhidi ya wasichana na wanawake nchini humo. Hata hivyo anasema MINUSCA imesaidia sana kulinda amani na usalama wa raia na mali zao; kuokoa maisha ya watu dhidi ya mashambulizi ya silaha! Kumbe, kuna haja ya kuthamini yale mema waliyotenda badala ya kutupa “mtoto na mbereko”. Matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha ya binadamu, zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu, ili hatimaye, nchi iweze kujijengea uwezo wa kuwa na vikosi vyake vya ulinzi na usalama. Familia ya Mungu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, haitaki kuona nchi yao inageuzwa kuwa ni kichaka cha mashambulizi dhidi ya Cameroon na Chad, watu wanataka kujenga utamaduni wa amani, haki na maridhiano, msingi wa maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

26/09/2017 13:50