2017-09-25 09:30:00

Papa Francisko: Michezo isaidie ujenzi wa amani na utulivu duniani


Michezo ya “Invictus” ni alama ya umoja, mshikamano na upendo kati ya watu unaopania kukuza na kudumisha utu na maisha ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Kardinali Thomas C. Collins, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Toronto, Canada, wakati huu wa michezo ya “Invivtus” iliyozinduliwa, Jumamosi, tarehe 23 Septemba na inatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 30 Septemba 2017.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake uliosomwa katika Liturujia ya kiekumene kwenye Kanisa kuu la “St. James”, Jimbo kuu la Toronto, Canada, hapo tarehe 19 Septemba 2017, amewatakia heri na baraka washiriki wote wa michezo hii pamoja na familia zao. Ikumbukwe kwamba, hawa ni wanamichezo wa kimataifa wanaotoka katika vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao wamepatwa na ulemavu katika maisha yao, wakati wakitoa huduma ya ulinzi, usalama na amani kwa nchi zao na familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa sadaka na majitoleo yao katika mchakato wa ulinzi, usalama na amani duniani.

Baba Mtakatifu anawataka washiriki wa michezo hii kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya kiutu, ambazo kwa neema ya Mungu wanaweza kuzionesha, kwa ujasiri, ari, moyo mkuu na ukakamavu wakati wote wa mashindano kama sehemu ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha ya mwanadamu. Michezo hii, iwe ni fursa ya kuimarisha umoja, mshikamano na mafungamano ya watu kutoka katika: mataifa, tamaduni na imani tofauti; daima maisha, utu na heshima ya binadamu vikipewa msukumo wa pekee. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa kiroho kwa njia ya sala zake. Michezo ya kimataifa ya “Invictus” ambayo imeingia sasa awamu yake ya tatu inawashirikisha wanamichezo walemavu 550 kutoka katika nchi 17 duniani, wanaoshindana katika michezo 12 tofauti tofauti! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, michezo itaendelea kusaidia ujenzi wa amani kwa familia ya Mungu duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.